Habari za Punde

Na hizi zinazoimbwa miaka hii, pia zinaitwa kaswida?


Na Haji Nassor, Pemba
MADRASA kadhaa za Qur-an katika miaka ya hivi karibuni, zimekuja na mtindo wa kuanzisha madufu yenye kuambatana na vinanda, ngoma na michanganyo mengine, ambayo hunogesha hilo linaloitwa dufu.
Kwenye madrasa hizo, waalimu hujiona kama vile hawajatimia baadhi yao, kama hawajanzisha burudani walioipa jina la dufu, na ndani yake mukiwa na maneno matamu yaliopewa jina la kaswida.
Inawezeka wako sahihi au kinyume chake, kuziita kaswida na wengine tukiziita nyimbo, huku bwana Mtume Muhammad (S.A.W) akitajwa ndani yake, hata kama wanafunzi walivo vaa wanajielewa wenyewe.
Kilichonipa kuutumia ukurasa huu, ni kuuliza ili nitoke ujinga, hizi zinazoimbwa siku hizi kwenye madufu yaliofanana na ngoma za kawaida ni sahihi nazo kuziita kaswida?
Nauliza hivyo kwanini, maana kidogo… ametajwa Allah, kisha hiyo inayoitwa kaswida… imezungurushwa akitajwa mtu mwengine ambapo kwa wasio na masikio husema hapa wanafunzi na waalimu wao wanakufuru.
Pengine kwa wasomi waliojaa karne hii ya 21, kwamba bado dufu na kaswida zao zinazopigwa miaka hii, zikawa ni sahihi ijapokuwa kwa wengine ndani ya kaswida hizo hasa za kileo zikawa na shubha.
Mbona zipo kaswida zina maneno yenye shaka kama vile ‘kujimwaya mwaya’, ongelea vyema bi harusi kwa mumeo, yuwapi mamae harusi aje uwanjani…. tusema kaswida hizi ndio zile zilizosomwa wakati wa bwana Mtume (S.A.W)?
Nimeshatungulia kusema kwamba, karne hii waalimu, masheikh, wanazuoni na maustadhi wameshakuwa wengi, na pengine kwao ni halali na wala hakuna shubha (shaka),  kuzisikia kaswida zenye mfano wa nyimbo kwenye hilo wanaloliita dufu.
Unaweza kujiuliza, dufu la miaka hii na kaswida zake, ndilo ambalo lilikuwepo wakati ule kiongozi mkuu wa waislamu wakati alipopokewa na watoto akiingia mji mtakatifu?
Leo tunashuhudia madufu yakiwa na nyimbo kama zinazofanana na miondoko ya kitaarab na hip hop..tena cha ajabu zaidi zikikusaanya vijana wa makamu wa jinsia zote, wakicheza hadi kupandisha mdadi.
Kwani sio sahihi kwamba upigaji wa dufu wa enzi hizo, ulipigwa na watoto wadogo na kaswida ya ‘twalaal-badrua alainaa’, sasa leo hatujakuza mambo ya kaswida zetu na aina ya upigaji wa dufu?
Eti wanaopiga dufu wa karne hii, kwanza wanafunzi wa kike waanze kuingia saluni, kung’arisha nywele na midomo kwa vipodozi vya bei ya juu, kama vile bi harusi, sasa je hayo ndo maelekezo sahihi?
Sisemi kwamba, madufu yapo kwa ajili ya kutega shilingi kwenye kodi za harusi na mikutano ya wanasiasa na sherehe za kitaifa, la hasha, nauliza tena hizi zinazoimbwa miaka hii nazo ni kaswida?
Wapo wanafunzi hawajahifadhi hata juu moja kwenye madrassa, lakini anazonyimbo zaidi ya kumi na tano, ambazo wamechukulishwa mazoezi makali ndani ya wiki mbili kwa ajili ya kujaza albamu, je hapo ni sahihi?
Kama hizi zinazoimbwa miaka hii kwenye hayo yaliopewa jina la dufu, nazo ni kaswida, sasa sisi tutatofautishaje na nyimbo za kizazi kipya kama Al-kiba, Dayamond, au wakongwe akina Abdalla Issa, Omar Kopa na mama yake, ambazo baadhi yao huzisikia vipande vikipyezwa kwenye hizo eti zinazoitwa kwaswida.
Kwa hili waalimu wa madrassa litazameni upya, maana mmebeba uuma mkubwa wa wanafunzi, maana kama ni sihihi, basi ndio tuombavyo na kama kinyume chake wakulibeba hilo ni nyinyi.
Lakini hata masheikh wetu wakuu, haya pia ni miongoni mwa mambo ya kukutana na kuyatolea kauli, sio tusubiri aliekula mchana wa ramadhani au waliovaa vimini ndio tujitokeze hadharani.
Ofisi yetu tegemezi ya Mufti, sasa lazima muibuke hadharani na muwaambie waislamu kwamba, wawe na shaka au kama hayo ni sahihi yanayofanywa na baadhi ya madrassa zetu yaendelee kunoga.
Mbona hata muislamu mmoja mmoja, nae pia analojukumu la kutaka kujua iwapo hizi zinazoimbwa miaka hii kwenye madufu yaliofanana na ngoma pia kama ni kaswida.
Kila kitu kinawezekana iwapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo huku akijua kuwa kila mmoja ni mchunga.

                  hajinassor1978@gmail.com      

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.