Habari za Punde

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                           23.08.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Kampuni ya simu ya ZANTEL  kupitia Kampuni ya “Millicom Group” kuimarisha utoaji huduma zake ili kuweza kupata mafanikio zaidi katika ushindani wa kibiashara.

Dk. Shein aliyasema hayo katika mazungumzo kati yake na uongozi wa Kampuni ya ZANTEL ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya “Millicom Group” akiwa pamoja na Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya “Millicom Group” na Mwenyekiti wa Bodi ya ZANTEL Rachel Samren pamoja na Mtendaji Mkuu wa ZANTEL Benot Janin.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa kufanikiwa kwa Kampuni hiyo ya simu ya ZANTEL katika utoaji huduma zake ndani na nje ya nchi ndio njia moja wapo ya kuitangaza Zanzibar kimawasiliano sambamba na kuinua uchumi wa Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa Kampuni nyingi za simu ambazo zimekuwa zikitoa huduma kwa wananchi Kampuni hiyo ya ZANTEL ina kila sababu ya kuimarisha huduma zake ili iendelee kuwa kivutio KWa wananchi katika kupata huduma bora za mawasiliano ya aina zote hapa nchini.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Kampuni hiyo ya ZANTEL kwa kuendelea kuwa na makao makuu yake hapa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na Kampuni hiyo ambayo Serikali ina hisa zake kwa lengo la kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliitaka Kampuni ya Millicom iendelee kujikita katika kuiwezesha ZANTEL kukuza na kuimarisha ukuaji na upanuzi wa shughuli zake hapa nchini.

Kwa upande wa Mkonga wa Taifa, Dk. Shein aliueleza uongozi huo haja ya kufuata taratibu zilizowekwa ili kila upande upate mafanikio pamoja na matarajio waliyojiwekea katika kuimarisha mawasiliano hapa nchini.

Nae Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya “Millicom Group” Mauricio Ramos, alimueleza Dk. Shein kuwa Kampuni hiyo itahakikisha ZANTEL inapata mafanikio zaidi kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa.

Alieleza kuwa juhudi mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha ZANTEL inaendelea kupanua soko lake sambamba na kuimarisha miundombinu yake ili kuweza kutoa huduma za uhakika.
Mtendaji Mkuu huyo wa Kampuni ya “Millicom Group” alimueleza Dk. Shein kuwa ZANTEL itahakikisha inakuwa mstari wa mbele katika kuimarisha huduma zake ikiwa ni pamoja na kupanua mtandao unaotumia 4G ambayo inarahisisha mawasiliano.
Sambamba na hayo, uongozi huo ulipongeza mashirikiano mazuri inayoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ina asilimia 15 za hiza za ZANTEL na kuahidi kwa upande wao kuendelea kuzidisha ushirikiano huo kwa lengo la kutoa huduma kwa jamii sambamba na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Kampuni ya Millicom ilitangaza kuanza utekelezaji wa mpango wa uwekezaji katika Kampuni ya ZANTEL ambao unajumuisha uimarishaji wa huduma za mtandao wa Kampuni hiyo ambapo Kampuni ua “Millicom Group” ilinunua asilimia 85 ya hisa za ZANTEL.
  
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.