Habari za Punde

Taarifa Rasmi ya Serikali kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mzee Aboud Jumbe Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akitoa taarifa rasmi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya pili Mzee Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea leo Mji Mwema Dar es Salaam na kuzikwa kesho katika viwanja vya nyumbani kwake Migombani Unguja.[Picha na Ikulu.]15/08/2016.

Kwa masikitiko makubwa, naomba kuwaarifu kuwa, leo tarehe 14 Agosti 2016, Mzee wetu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia. Kama mnavyofahamu, Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa Zanzibar awamu ya pili, ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na umri wake.

Msiba huu umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Dar es salaam. Maziko ya marehemu yatafanyika kesho tarehe 15 Agosti 2016 saa 7.00 mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar, Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani.

Kufuatia mchango  na juhudi mkubwa ambazo marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga Zanzibar pamoja na nafasi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi yetu imekabiliwa na msiba mkubwa kwa kifo cha kiongozi huyu mahiri.  

Kutokana na msiba huu mkubwa kwa nchi yetu, natangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia kesho tarehe 15 Agosti 2016.  Katika kipindi hicho chote bendera zote zitapepea nusu mlingoti.  Kadhalika utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe marehemu aliutoa wakati wa uhai wake.

Tunaungana na wanafamilia wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba.  Naomba kutumia nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit marehemu mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin.


Inalillahi wainnailaihi rajiun 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.