Na Salum
Vuai, MAELEZO
Katika azma
ya kuuenzi mchango wa msanii na mwanaharakati mashuhuri wa Zanzibar marehemu Siti
binti Saad, kumeandaliwa harambee kubwa kwa lengo la kukusanya fedha za kujenga
jengo la kumbukumbu yake.
Mwenyekiti
wa taasisi ya Bibi Siti Bint Saad Nassra Mohammed Hilal, amesema katika mkutano
na waandishi wa habari kwamba harambee hiyo imepangwa kufanyika Septemba 24,
katika hoteli ya Park Hyatt mjini Zanzibar.
Amesema mgeni
rasmi katika harambee hiyo itakayoambatana na chakula cha usiku, anatarajiwa
kuwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye atawaongoza waalikwa
mbalimbali kutoa michango.
Bi. Nasra
amesema tayari taasisi yake imeshapatiwa eneo la kujenga nyumba hiyo katika
kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi B, alikozaliwa marehemu Siti Binti Saad
mwaka 1870.
Mbali na
harambee hiyo, Mwenyekiti huyo amesema Septemba 18 kutafanywa ziara ya
kutembelea eneo hilo la Fumba, ambayo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Ayoub Mohammed Mahmoud, na Septemba 20, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel
Thomas, ataongoza ziara katika nyumba za wazee Sebleni na Welezo.
Aidha
amesema mnamo Septemba 21, mwaka huu, taasisi yake imeandaa ziara katika eneo
alilozikwa marehemu Siti hapo Rahaleo, mkabala na mkunazi, ambapo Meya wa
Manispaa ya Zanzibar Abdulrahman Khatib atakuwa mgeni rasmi.
Siti binti
Saad aliyefariki dunia mwezi Juni 1950 alikuwa msanii wa kwanza mwanamke kuimba
taarab hadharani na kuitangaza Zanzibar kimataifa, ambapo pia nyimbo zake
zilikuwa zikitetea hadhi ya mwanamke na kupiga vita dhuluma na udhalilishaji.
Kiasi cha
shilingi bilioni mbili na milioni tano zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba hiyo itakayokuwa na sanaa za aina mbalimbali, pamoja na sehemu za
kufanyia tafiti za utamaduni.
No comments:
Post a Comment