Habari za Punde

Balozi Seif atoa misaada mbalimbali jimboni

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini  “B”  Nd. Issa Juma kushoto yake wakikaguwa maendeleo ya ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Fujoni.

 Haiba ya muonekano wa Jengo la Msikiti wa Ijumaa Fujoni  unavyoonekana nje ukiendelea ujenzi wake ambao unatarajiwa kuezeskwa mapema wiki ijayo.
  Balozi Seif kati kati akifafanua jambo wakati wa hafla ya kukabidhi Hundi kwa ajili ya kugharamia uendelezaji wa ujenzi wa jengo la Maabara la Skuli ya Sekondari ya Kitope.Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wiaya ya Kaskazini B Nd. Issa Juma na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Maandalizi na Msingi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Safia Ali Rijali.

Kulia ya Balozi Seif ni Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Suleiman Juma Makame na Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo la Maabara ya Skuli za Fujoni na Kitope Nd. Yasir De Costa.

Msimamizi wa Ujenzi wa Majengo ya Maabara ya Skuli za Fujoni na Kitope Nd. Yasir De Costa wa kwanza kushoto akitoa ufafanuzi wa ujenzi wa majengo ya Maabara ya skuli hizo.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Viongozi na washirika wa maendeleo katika Sekta ya Elimu kuzijengea uwezo zaidi wa miundombinu skuli mbali mbali Nchini ili ziwe na uwezo kamili wa kuhimili ushindani wa kitaaluma uliopo katika kiwango cha Kitaifa na Kimataifa.

Alisema wakati wa sasa ni ule wa sayansi uliobadilika kabisa Kiteknolojia tofauti na uliopita kiasi kwamba jamii inapaswa kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira yanayokubalika kivifaa pamoja na walimu waliobobea.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa kumbusho hilo wakati akikabidhi Hundi ya shilingi Milioni 13,078,000/- kwa ajili ya ukamilishaji wa Jengo la Kisasa la Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Kitope iliyomo ndani ya Jimbo la Mahonda.

Katika hafla hiyo fupi ambayo pia alikabidhi hundi ya shilingi Milioni  1.7 kukamilisha gharama za ujenzi wa Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Fujoni kwa msimamizi wake Nd. Yasir De Costa Balozi Seif aliahidi kutoa vifaa vyote vya Maabara kwa Skuli ya Sekondari ya Kitope mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

Balozi Seif  alisema Zanzibar kama Nchi nyengine yoyote Duniani inahitaji kuwa na wataalamu wa kutosha katika kusimamia majukumu ya Serikali na hilo litawezekana na kupatikana iwapo watoto wa Taifa hili watajengewa msingi imara wa Taaluma wawapo maskulini.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda alieleza kwamba Uongozi wa Jimbo hilo daima utakuwa kamini na imara katika kuhakikisha watoto wote wa Jimbo hilo wanapata elimu ya msingi hadi Sekondari kutegemea uwezo halisi wa mwanafunzi husika.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Suleiman Juma Makame alisema msaada huo ni faraja kubwa itakayozaa mafanikio yanayotarajiwa kupatikana katika kipindi kifupi kijacho.

Mwalimu Suleiman alisema Skuli  hiyo ilikuwa ikipata changamoto kubwa la kupoteza fedha zaidi ya shilingi Laki sita hadi Saba kufanya  maandalizi ya vifaa kwa ajili ya matayarisho ya mitihani ya wanafunzi wa Darasa la Kumi na Mbili     { yaani Form IV}.

Kwa upande wake  Msimamizi wa ujenzi wa Majengo ya Maabara ya Skuli za Sekondari Fujoni na Kitope Ndugu Yasir De Costa alisema Jengo la Fujoni limeshakamilika ujenzi wake na tayari lina uwezo wa kutoa huduma ya Maabara kwa kiwango kinachokubalika.

Nd. De Costa aliahidi kwamba ukamilishaji wa jengo la Maabara la Skuli ya Sekondari ya Kitope unaotarajiwa wakati wowote kuanzia sasa utachukuwa takriban wiki Nne.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Maandalizi na Msingi Bibi Safia Ali Rijali  kwa niaba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  alimpongeza Balozi Seif Ali Iddi kwa jitihada anazochukua katika kusaidia sekta ya Elimu hasa Vikalio, Kompyuta pamoja na vifaa vya Maabara.

Mkurugenzi Safia alisema jitihada zinazochukuliwa na Viongozi, wahisani pamoja na wananchi katika kuunga mkono mapambano dhidi ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu zinatoa mwanga wa kusaidia Watoto ambao ndio wasimamizi wa Taifa la sasa na lijalo.

Wakati huo huo Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif  alikagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa unaojengwa katika Kijiji cha Fujoni na kuridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo.

Fundi Mkuu wa Ujenzi wa Msikiti huo Bwana Mbarouk Said alimueleza Balozi Seif  kwamba uchimbaji wa Kisima pamoja na usogezwaji wa huduma za Umeme zimekamilika na hatua za uwezekaji  zinatarajiwa kuanza wiki ijayo.

Msikiti wa Kisasa wa Ijumaa wa Fujoni utakuwa na uwezo wa kusaliwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu  zaidi ya elfu moja kwa wakati mmoja wa sala kwa mujibu wa utafiti wa wataalamu wa masuala ya majengo ya Ibada.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.