Habari za Punde

Chaani walia na barabara mbovu ya Mkwajuni

Fatma Makame/ MCC
                                                    
Wananchi wa kijiji cha Chaani  Wilaya ya Kaskazin ‘A’ Unguja wamelalamikia ubovu wa barabara inayoelekea Mkwajuni ambayo imekuwa kero kubwa kwao na wananchi wengine wanaotumia barabara hiyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Bi. Neema Mchezo Bakari amesema tatizo hilo ni la muda mrefu  na bado halijapatiwa ufumbuzi jambo ambalo linapelekea usumbufu katika harakati zao za kutafuta maendeleo.

Amesema wananchi wanapata usumbufu mkubwa kutokana na kuwepo mashimo katika barabara hiyo na kupelekea baadhi ya madereva kukataa kupita na wengine  kuendesha gari kwa kasi bila kujali mashimo hayo na kusababisha ajali.

“Inafika wakati wajawazito kujifungulia njiani kwenye gari wakati wanapopelekwa hospitali kutokana maumivu wanayoyapata kutokana na  mashimo yaliyomo katika barabara hiyo”,  amefahamisha mwananchi huyo.

Nae  Chum  Juma Simai amesema ubovu wa barabara hiyo umechangia  baadhi ya madereva wa  gari za abiria kutoza nauli kubwa kinyume na taratibu zilizowekwa na serikali na kuitaka mamlaka husika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

 Nae Mkandarasi Mkuu wa Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara Nd. Jafeti amesema serikali tayari inalishughulikia tatizo la barabara hiyo  na ujenzi utaanza baada ya kukamilika  hatua za kumpata mkandarasi na kuwataka wananchi kujenga subira na ustahamilivu.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.