Habari za Punde

Dk Shein akamilisha vikao vya kupitisha Mipango ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE

    Zanzibar                                            13 Septemba, 2016


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kukamilisha vikao vya kupitisha Mipango ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 vilivyoanza wiki iliyopita.

Katika kikao hicho Dk. Shein aliwapongeza viongozi na watendaji wa Ofisi hiyo kwa kufanyakazi kwa ushirikiano (team work) ambao alisema umekuwa msingi wa mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Saba, Ofisi hiyo ilitekeleza vyema majukumu yake ya kutekeeleza Ilani lakini ametoa wito kwa viongozi na watumishi kuongeza kasi katika kipindi hiki cha pili cha Utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2015-2020.

Katika mnasaba huo ameitaka Ofisi hiyo kuhakikisha kuwa kila idara ya Ofisi hiyo inakuwa na watumishi wa kutekeleza majukumu ya idara kisiwani Pemba ili kuwe na uwiano sahihi wa utekelezaji wa Ilani Unguja na Pemba.

Katika hatua nyingine Dk. Shein ameitaka Kurugenzi ya Mawasilianao Ikulu kubuni njia nyingi na rahisi zaidi za kuwasiliana na wananchi ili kuendelea kuwaweka karibu serikali.

Dk. Shein amebainisha kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa kuwapatiwa wananchi taarifa mbalimbali kuhusu shughuli za serikali kupitia njia mbalimbali za mawasiliano lakini ipo haja ya kubuni njia nyingine rahisi ambazo zitapanua wigo wa mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.

Alisisitiza kuwa taarifa muhimu za Serikali hazina budi kuwafikia wananchi kwa wakati na kwa uhakika ikiwezekana kutumia mfumo wa utawala  kupitia kwa masheha ambapo baadhi ya machapisho yanaweza kuwasilishwa kwao na kugawanywa kwa wananchi.   

Katika kikao hicho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alihimiza pia kuharakishwa kwa mchakato wa matayarisho ya Sera ya Diaspora ili iweze kutumika kwa faida ya wanadispora na nchi kwa jumla.

Akizungumza wakati wa majumuisho ya kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alimshukuru mheshimiwa Rais na viongozi wengine waliohudhuria kwa michango yao na kuahidi kuzingatia ushauri wao ili kuboresha mpango huo kwa minajili ya kufikia malengo yaliyowekwa.

Aidha Waziri Gavu alieleza kuwa mchakato wa kuunda Sera ya Diaspora umo katika hatua za mwisho kukamilika baadaya kupitishwa katika Kikao cha Makatibu wakuu na kwamba hivi sasa inasubiri kuwasilishwa katika Baraza la Mapinduzi hivi karibuni.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Vikao vya kupitisha Mipango ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 -2020 vilianza Jumatatu tarehe 5 Septemba, 2016 ambapo kikao cha kimehitimisha idadi ya wizara 13 ziliwasilisha mipango yao na kujadiliwa.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.