Habari za Punde

Dk Shein: Serikali imedhamiria kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazovikabili vyombo vya habari vya Serikali

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                            07 Septemba, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali imeuhakikishia uongozi wa wizara ya Habari, Utalii na Michezo kuwa changamoto zinazovikabili vyombo vya habari vya serikali zitatafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua hadi kufikia lengo la kuvifanya vyombo hivyo kuwa vyenye ubora zaidi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali inataka kuona katika ndani ya miaka miwili ijayo katika vyombo hivyo hususan ZBC TV na gazeti la Zanzibar Leo kuwe kumefanyika mabadiliko makubwa kuelekea kwenye ubora zaidi.

 “Serikali imewaamini kuwa mna uwezo wa kuleta mabadiliko hayo hivyo na hamna budi kujenga imani hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii bila ya kukata tamaa ili mtimize lengo la wizara”. Dk. Shein aliuambia uongozi wa wizara wakati wa kuhitimisha kikao cha kujadili Mpango wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2015-2020 kwa wizara hiyo.

Katika kikao hicho, Dk. Shein alihimiza matumizi sahihi na bora ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari vya Serikali ili viwe mfano wa matumizi ya lugha hiyo ambayo ndio lugha mama ya wananchi wa Zanzibar.

Aidha, katika kuendeleza utamaduni wa mzanzibari, alikumbusha wajibu wa wizara hiyo kudumisha michezo ya asili ya watoto ambayo ilikuwa na mafunzo mazuri na kuwajenga watoto na vijana lakini kwa sasa inaelekea kupotea kabisa.

Akiwasilisha Mpango wa Utekelezaji wa Ilani kwa upande wa vyombo vya habari Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Omar Hassan Omar alibainisha kuwa wizara hiyo itaimarisha matumizi ya TEHEMA na kuendeleza mageuzi ya sekta ya habari ili kuongeza ufanisi na weledi katika tasnia ya habari nchini.

Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed jana alikutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mpango wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa wizara hiyo.

Katika kikao hicho Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Dk. Khalid Salum Mohamed alikieleza kikao hicho namna Wizara yake ilivyojipanga kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

“Maeneo ambayo wizara yangu ilipaswa kuyazingatia ni pamoja na Kukuza Uchumi Ibara 68 (a, b,c na d), Mchango wa Sekta Binafsi, Ibara ya 69 (a na b), Kupambana na Umasikini Ibara 70(e), Sekta ya Miundombinu ya Kiuchumi, Ibara ya 88(a), Kuendeleza Makundi mbali mbali,Ibara ya 139(b)- na Hifadhi ya Jamii, ibara ya 141(a, b na c)” Dk. Khalid alibanisha.

Akifunga kikao hicho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliupongeza na kuushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa namna ya ilivyowasilisha mpango wake na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wake.

Vikao vyote viwili vilihudhuriwa pia na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wakati huo huo vikao vya kujadili Mipango ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Mwaka 2015-2020 viliendelea tena leo huko Ikulu chini ya uenyekiti wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Mapema asubuhi Dk. Shein alikutana na viongozi wa Wizara Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto. Baadae jioni alitarajiwa kukutana na viongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi; na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.