Habari za Punde

Hotuba ya Balozi Seif alipoahirisha mkutano wa tatu wa Baraza la tisa la Wawakilishi

HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA TATU WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI SIKU YA IJUMAA TAREHE 30 SEPTEMBA, 2016
----------------------


1.     Mheshimiwa Spika, awali ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwingi wa Rehma kwa kuendelea kuiweka nchi yetu hii katika hali ya amani, utulivu, umoja na mshikamano mkubwa.  Hali ambayo imeiwezesha Serikali na wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila ya mtafaruku wa aina yoyote. Aidha, nawaomba wananchi waendelee kuitunza na kuithamini amani iliopo nchini.

2.     Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa tukiwa katika hali ya uzima na afya njema na kutuwezesha kufanikisha vizuri Mkutano wa Tatu wa Baraza hili Tukufu la Tisa la Wawakilishi, ulioanza tarehe 21 Septemba, 2016. Nimefarijika kuwa kazi zote zilizopangwa katika ratiba yetu tumezikamilisha kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

3.     Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi maalum kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kusimamia amani na utulivu hapa nchini pamoja na kutekeleza kwa vitendo na umahiri mkubwa Ilani ya Chama  Cha Mapinduzi.  Mheshimiwa Rais amekuwa muhubiri mkubwa wa amani na utulivu wa nchi yetu.  Amefanya hivyo kwa kujua kuwa amani ni chachu ya maendeleo, bila ya amani hakuna maendeleo.  Nawaomba Wajumbe tuungane na Rais wetu katika kuhubiri amani katika Majimbo yetu.

4.     Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kutoa pole kwa familia, Serikali  na Wananchi wa Zanzibar na Tanzania  kwa ujumla kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  wa  Awamu ya Pili na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea tarehe 14 Agosti, 2016  na kuzikwa tarehe 15 Agosti, 2016.  Marehemu Mzee Jumbe atakumbukwa kwa michango yake mikubwa kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hasa kwa kuimarisha demokrasia ikiwemo kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, kuanzisha Baraza la Wawakilishi pamoja na kuimarishwa mihimili mitatu ya dola, ndiyo maana leo tunafurahia demokrasia aliyotuachia kupitia chombo hiki tukufu.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Aboud Jumbe mahala pema peponi – Amin.

5.     Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufanikisha kwa wakati ahadi alizozitoa kwamba ifikapo tarehe 20 Septemba, 2016  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari itakuwa  imeshanunua  ndege mbili mpya,  ni  ukweli usiopingika tayari ndege mbili aina Bombadier Dash – 8 Q400 zimeshanunuliwa na kuwasili nchini Tanzania.  Hii imeonyesha imani na upendo wa dhati  alionao kwa wananchi wake wa Tanzania anaowaongoza,  pia ndege hizi ni chachu ya kukuza uchumi wa Tanzania, na zitasaidia usafiri wa uhakika wa Watanzania.  Nawaomba watakao kabidhiwa dhamana ya kuziendesha ndege hizi chini ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) waziendeshe ndege hizo vizuri pamoja na Shirika lenyewe, ili ziweze kutuhudumia kwa muda mrefu.

6.     Mheshimiwa Spika, naomba pia kuchukua nafasi hii kuwapa pole wananchi  wa Tanzania, Mkoa wa Kagera, kwa madhara waliyoyapata kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea tarehe 10 Septemba, mwaka huu lililosababisha vifo na majeruhi pamoja na kuathiri miundombinu na makaazi ya watu pamoja na sekta muhimu za kijamii. Natoa shukrani za dhati kwa Watanzania wote waliopo ndani na nje ya Tanzania, pamoja na raia wengine wa nchi za nje wakiwemo wa nchi jirani kwa kuonesha imani kubwa kwa waliopatwa na maafa hayo kwa misaada yao ya hali na mali. Natoa wito kwa wananchi wote wa ndani na nje  ya Tanzania kuendelea kuchangia kwa hali na mali ili kurejesha hali ya Mikoa iliyoathirika katika sura mpya.

7.     Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 15 Februari, 2016 Serikali ilitoa uamuzi wa kuwahamisha wafanya biashara wa makontena Darajani na wale wa jengo la treni na kuwahamishia eneo la Saateni.  Zoezi hilo lilifanyika kuanzia tarehe 15 Februari, 2016.  Uamuzi huo umetokana na haja ya kubadilisha mandhari na haiba ya mji wetu na sio kuwakomoa wafanya biashara hao kama inavyodaiwa na baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar.   Aidha, napenda kutoa taarifa kwamba zoezi hili ni endelevu ambalo litaendelea katika maeneo mengine ambayo wafanya biashara wameyavamia na kufanya biashara zao bila ya mpango maalum.  Serikali ina nia ya dhati ya kuuletea mji wa Zanzibar haiba inayostahili.  Tunawaomba wananchi waliunge mkono zoezi hili.

8.     Mheshimiwa Spika, nachukua furasa hii kwa niaba ya Baraza lako Tukufu kutoa masikitiko yetu na pole zetu nyingi kwa wananchi wa Pemba waliokatiwa vipando vyao vya mikarafuu na miti ya matunda pamoja na kubomolewa nyumba zao bila ya sababu zozote za msingi.  Tunakilaani kwa nguvu zetu zote kitendo hicho kwani hakikuwa cha kiungwana wala ustaarabu bali kilikuwa kitendo cha kifisadi tu.

9.     Mheshimiwa Spika, katika kikao hiki jumla ya Maswali ya Msingi 74 na maswali ya nyongeza 181 yaliulizwa na yalijibiwa. Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe kwa kutumia nafasi yao ya kuihoji Serikali pia natoa pongezi kwa Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa namna walivyojibu maswali hayo na kutoa ufafanuzi fasaha.  Nawapongeza sana Mawaziri hao wote.

10.  Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukurani na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna anavyosaidia katika kutoa ufafanuzi wa kisheria kila lilivyojitokeza jambo ambalo lilihitaji ufafanuzi wa kisheria, amefanya kazi kubwa na nzuri na ameonesha umahiri mkubwa katika fani yake ya sheria.

11.  Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo yaliyojitokeza katika mkutano huu ni harambee ya kuchangia pesa kwa ajili wananchi waliopatwa na maafa ya tetemeko katika Mkoa wa Kagera na Mikoa jirani. Baada ya kujadiliwa na Baraza lako Tukufu, Waheshimiwa Wajumbe kwa pamoja walikubali kuchangia posho ya siku moja kwa kila Mjumbe wa Baraza lako Tukufu ili liwasilishwe katika Mikoa iliyopatwa na maafa ya tetemeko.  Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote kwa uamuzi wao huo na wale wote waliofanikisha zoezi hili.  Michango hiyo ilionyesha mshikamano wetu Watanzania kila maafa yanapotokea katika nchi yetu.

12.  Mheshimiwa Spika, aidha katika mkutano huu, jumla ya Miswada Minne (5) imejadiliwa na kupitishwa kuwa Sheria na Baraza lako Tukufu.  Miswada yenyewe ni:-
i        Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Taasisi ya Elimu ya Zanzibar na Mambo mengine Yanayohusiana na Hayo.
ii       Mswaada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria  ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Nam. 8 ya 1999 kama ilivyorekebishwa na Sheria Nam. 11 ya mwaka 2009 na Kuwekwa Masharti Bora Pamoja na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
iii                Mswada wa Sheria ya Marekebisho  ya Sheria  mbali mbali na kuweka  Masharti yaliyo Bora kuhusiana na mambo hayo.
 iv      Mswada wa sheria ya mafuta (utafiti na uchimbaji)  na gesi asilia.
 v.      Mswada wa Sheria wa kufanya marekebisho ya 11 ya Katiba ya Zanzibar inayohusu kifungu cha 66.  Kwa kupitishwa Mswada huu, Rais kwa sasa ataweza kuzitumia nafasi zake 10 bila ya kuwepo kwa masharti magumu ya Kikatiba na hasa kuhusiana na nafasi mbili kwa ajili ya upande wa upinzani.

13.  Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba Miswada hiyo mitano tuliyoipitisha itasaidia kwa kuweka misingi bora ya utendaji na pia  kukuza uchumi wa Zanzibar.  Ni ukweli  usiopingika kwamba kupatikana kwa mafuta na gesi kutaiwezesha nchi yetu kukua kwa haraka kiuchumi, kwa  kuiongezea mapato Serikali na wananchi kwa ujumla, na pia kuongeza ajira kwa wananchi wetu.

14.  Mheshimiwa Spika,  yote hayo yataweza kufikiwa iwapo Sheria tulizozitunga katika Baraza hili tutashirikiana  katika kuifanya kazi kama inavyotakiwa, hata hivyo napenda kutanabahisha kwamba tulichokuwa nacho hivi sasa ni sheria na sio mafuta na gesi. Baada ya kukamilika kwa utafiti ndipo itajulikana kiwango gani cha mafuta na gesi asilia kilichopo nchini.

15.  Mheshimiwa Spika, kupitishwa kwa Mswada wa mafuta na gesi asilia ni jambo la historia kwetu.  Hivyo, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amekubali kuiweka saini Sheria hiyo mbele ya Vyombo vya Habari pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria ya Baraza la Wawakilishi na Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi.

Nawaahidi Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kuwa haitochukua muda mrefu kitendo hicho kufanyika.  Nawapongeza Wajumbe kwa kuipitisha Miswada hiyo kwa sauti moja.

16.  Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hofu waliyonayo  baadhi ya wananchi juu ya mikataba ya masuala ya mafuta na gesi.  Kwa kulitambua hilo Serikali imejipanga vyema kuwa na mikataba bora ambayo italeta tija kwa nchi yetu na watu wake.  Aidha, mikataba yote itakayohusiana na mafuta na gesi asilia itafanywa kwa uwazi.  Lengo ni kuwa na uwazi ambao utaipatia heshima nchi yetu na kupunguza malalamiko na minong’ono isiyokuwa ya lazima. 

17.  Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wale wote waliotuwezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi kwa ufanisi mkubwa.  Pongezi hizo zaidi ziwafikie watendaji wote wa Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu, Ndugu Raya Issa Msellem.  Ni ukweli usiofichika kwamba tumeanza vizuri na ninaamini tutaendelea vizuri.  Mungu libariki Baraza hili, Mungu zibariki Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.  Pia nawapongeza wakalimani wetu wa lugha ya alama ambao wamewawezesha Waheshimiwa Wawakilishi wenye ulemavu wa kusikia kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Baraza.  Vile vile nawashukuru Wanahabari kwa kufanya kazi ya kuwahabarisha wananchi wetu yale yaliyokuwa yakiendelea Barazani hapa.

Mwisho, Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe, Mhe. Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa kuliongoza vizuri na kwa ufanisi mkubwa Baraza hili.  Hekima na busara zenu zimesaidia sana katika kuumaliza mkutano huu salama.

18.  Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niwatakie Waheshimiwa Wawakilishi kila la kheri na mafanikio mema katika kuwatumikia wananchi wao Majimboni mwao.  Aidha, nawatakia safari njema na ya salama ya kurudi Majimboni mwao, na hasa Wawakilishi wenzetu kutoka Pemba kwa sababu wao wana safari ndefu zaidi kuliko wenzao wa Unguja.

19.  Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 23 Novemba, 2016, saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.


20.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.