Habari za Punde

Kumbukumbu ya Hijja na athari zake - 2

Naam Mina ni Masha’aril Haraam mojawapo katika sehemu takatifu kwa Waislamu ni sehemu ambayo ukiomba kwa Allaah ‘Azza wa Jall hutakabaliwa du’aa yako. Nilijitahidi kuomba na kila Muislamu ninaemuona yumo katika maombi, au dhikr au anasoma Qur’aan mpaka nafsi inanisuta mbona siku zote ulikuwa hufanyi Ibada kama hivi? Nikaijibu nipo katika sehemu takatifu na nimekuja kwenye mafunzo ya vitendo nafsi we. Naam nikajaaliwa kuzisali sala za Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha pamoja na Alfajiri Jamaa kwa kupunguza Sala zenye rakaa nne kama alivyofanya Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam alipohiji.

Tulipoamka Alfajiri siku ya pili ya mafunzo, Siku ya Arafah siku adhimu katika masiku ya dunia, siku muhimu kwa mwenye kuhiji kwani ndiyo nguzo kuu ya Hajj ambayo ikikosekana basi aliyefanya safari hii hana Hajj, tulijiandaa kuelekea Arafah asubuhi na mapema kutoka Mina.

Tulipowasili viwanja vya ‘Arafah, nilihakikisha nipo katika mipaka yake ili Ibada yangu ikamilike. Tulibahatika mwaka huu siku ya ‘Arafah kuangukia Ijumaa kama ilivyokuwa kwa kipenzi chetu Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam miaka 1435 iliyopita hivyo tukapata fursa mbili za kuweza kukubaliwa duaa, maombi, shida na matlaba yetu – fusa ya ‘Arafah na fursa ya Ijumaa.

Ilipofika muda wa kuanza ‘Arafah (baada ya Zawaal yaani jua kutenguka) tulisali Adhuhuri na Alasiri jamaa ya kutanguliza na kupunguza kwa kuzisali rakaa mbili mbili. Kisha tukatangaziwa kwamba ule muda ambao shetani anaukasirikia kadri ya kukasirika umefika wa kupeleka maombi yetu, shahada zetu, maelezo yetu, CV zetu kwa Allaah ‘Azza wa Jall umeanza.

Siku ambayo Mtume wetu Swalla Allaahu ‘Alayhi wasallam ambaye tayari ameshasamehewa madhambi yake yaliotangulia na yatakayokuja alisimama kuanzia adhuhuri mpaka kuzama kwa jua akiomba tu huku mikono yake akiwa ameinyanyua kwa masaa takriban sita. Nikajiuliza wapi mimi na Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam?  Nikajiambia kimoyomoyo nijaribu kuiga mwenendo wake nikatoka nje ya hema nikaelekea qiblah na kuanza kuomba kila dua ninayoijua au niliyobahatika kuisikia na kuihakikisha si miongoni mwa dua zilizokuwa na walakini.

Ni siku ambayo niliingiwa na simanzi, mwili nikausikia una joto na huku chozi likinitoka ninamuomba Allaah ’Azza wa Jall kwani niliwahi kuisikia hadithi ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam inayosema jicho litalotoa machozi kwa ajili ya Allaah halitogusa moto siku ya kiama! Naam licha ya jitihada zangu sikumfikia au kuifikia rekodi ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi Wasallam.

Kulikuwa na joto lakini sikujali, kwani sikuwa pekee yangu kwenye jua, mamilioni ya waislamu tulikuwepo ‘Arafah sote tukifanya jambo moja tu; Kuomba. Joto ni kitu gani mbele ya joto la moto wa Jahannam!

Naam ‘Arafah ni siku adhimu, ‘Arafah ni siku pekee ambayo haina mfano wake kwani hakuna siku katika masiku ya dunia ambayo Allaah ‘Azza wa Jall huwaachia huru waja wake na moto kwa wingi kama siku ya ‘Arafah. Ndio maana shetani huichukia.

Allaah ‘Azza wa Jall katika siku hii huwa karibu na Malaika na kuwauliza: “Wanataka kitu gani waja wangu hawa?” Allaahu Akbar.

Naam ikiwa ‘Allah ‘Azza wa Jall amewasamehe waja wake siku hii hata na mimi nilipokuwa nimesimama ‘Arafah nilimhakikishia Allaah ‘Azza wa Jall kwamba nimewasamehe wote walionikosea. Kwanini nisiwasamehe wakati nimehakikishiwa ikiwa Hijja yangu itakubaliwa basi nitarudi kama ndio kwanza nazaliwa? Nilipozaliwa sikuwa na niliemkosea wala alienikosea.

Kwanini nisiwasamehe wakati Mtume Swalla Allaahu ‘alayahi wasallam alipofika Makkah na kuikomboa aliwasamehe Maquraysh wote licha ya madhila, mateso na kila baya walilowatendea waislamu na aliwauliza: “Mnadhani nitakufanyeni nini leo?” Wakamjibu ‘Ndugu yetu uliye karimu , mtoto wa ndugu yetu aliye karimu’. Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi wasallam akawaambia: “Nendeni nyote mko huru” Hili ni darsa muhimu la kujifunza ndugu yangu tuwe ni wenye kusameheana kwa ajili ya kupata radhi zake Allaah ‘Azza wa Jalla. Kama angelikuwa Allaah ‘Azza wa Jall si mwenye kusamehe basi dunia hii isingelikalika ndio maana amejinasibu kuwa Yeye ni Ghaafir – mwingi wa kusamehe na pia Ghaffaar - anaendelea kusamehe (kila tukifanya makosa basi turudi kwake tuombe msamaha)


Ndugu yangu katika imani unaeusoma waraka huu, ukitaka upate mafunzo yatakayobadilisha mwenendo mzima wa maisha yako, jihimu uende Hijja na ukasimame ‘Arafah. Ukitaka ujihisi upo karibu na Allaah ‘Azza wa Jall na huku akisikia maombi na duaa zako, jihimu uende Hijja na umuombe Allaah ‘Azza wa Jall siku ya ‘Arafah. Ukitaka kuachiwa huru na moto, jihimu uende Hijja na uwepo katika viwanja vya ‘Arafah ukimuomba Allaah ‘Azza wa Jall maombi yanayotoka ndani ya moyo wako, yaliyojaa Ikhlaas na kumthibitishia Allaah ‘Azza wa Jall kwamba ni yeye pekee ndiye mwenye kupokea na kuyakubali maombi yote yawe makubwa au madogo.

Itaendelea...

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.