Ilipofika
magharibi mafunzo yetu yakaendelea kwa kwenda viwanja vya Muzdalifah kutekeleza
moja katika mambo yaliyo wajibu katika Hijja.
Muzdalifah
nimekutana na mafundisho kadhaa kama la kutakiwa kulala nje tena chini kwenye
jangwa lisilo na kitu chochote. Ni fundisho kubwa sana kwani hapo kila
aliyekuja Hijja bila ya kujali uwezo wake, ulwa wake, cheo chake anatakiwa
kulala chini kama alivyolala Mtume wetu Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam na
akatukumbusha kwamba: “chukueni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj”. Ndiyo nina
kitanda cha sita kwa sita nyumbani lakini Muzdalifah nimelala chini kwa ajili
ya kutekeleza Manaasik ya Hijja.
Muzdalifah
hukutanika Mahujjaaj wote wakiwa dhalili wakiwa na shuka mbili tu licha ya
utajiri waliojaaliwa nao, wakilala sehemu ya ardhi isiyokuwa na tandiko zaidi
ya zulia au busati kwa atakayejaaliwa licha ya neema ambazo Allaah ‘Azza wa
Jall amewajaalia baadhi ya waja wake. Yote ni kwa ajili ya kutufundisha
fundisho muhimu katika maisha kwamba tuondokane na kiburi na majivuni kwani
licha ya kujaaliwa kila tulichojaaliwa lakini utukufu ni wa Allaah ‘Azza wa
Jall pekee - Mwenye nguvu na mshindi na kuwepo kwetu Muzdalifah tunauthibitisha
utukufu huu kwa vitendo. Allaahu Akbar
Naam
tulipofika Muzdalifah tukasali Magharibi na Isha kwa kuzichanganya na kupunguza
Isha kwa kuisali rakaa mbili.
Kisha
tukatakiwa kuokota vijiwe vidogo tu saizi ya kokwa ya ubuyu kwa ajili ya kupiga
Minara ya Jamaraat. Nikaokota vijiwe sabini na kuongeza vichache. Kwa
nini sabini? Kwa sababu nitatakiwa kuvitumia kwa muda wa masiku matatu kama
sina haraka na kama nina haraka ningetumia kwa masiku mawili. Ndivyo alivyotupa
rukhsa Allaah ‘Azza wa jall katika Qur’aan.
Lakini
nilipovipitia vitabu vikanikumbusha kwamba kama nikitaka hasa kumfuata Mtume
Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam yeye aliokota
vijiwe saba tu Muzdalifah kwa ajili ya kupiga Jamaratul Kubra pekee ama vijiwe
vyengine aliviokota Mina. Mina pia kumeruhusiwa kuokota vijiwe.
Nikapanda
basi kurudi Mina nikitokea Muzdalifah huku nikiwapita maelfu na maelfu ya
Mahujjaaj waliokuwa wakielekea Mina kwa miguu.! Namshukuru Subhaana kwa
kujaaliwa usafiri lakini hapo nikajiuliza hivi Hijja yangu ni bora zaidi au
Hijja ya waendao kwa miguu?
Nikamkumbuka
Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam yeye alipohiji, alihiji akiwa juu ya
Ngamia. Kwa hivyo nikajikinaisha kwamba ninaetekeleza Sunnah ya Mtume wetu
Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam.
Itaendelea...
No comments:
Post a Comment