Habari za Punde

Msifanye malipo bila ya kudai Risiti - Wito

Hassan Khamis, Pemba

WANAVIKUNDI kisiwani Pemba, wametakiwa kutokubali kufanya malipo katika taasisi za serikali, bila ya kupewa risiti halali kwani kufanya hivyo wanaikosesha serikali mapato.

Wito huo umetolewa na afisa elimu wa Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA) Shuwekha Abdalla Omar katika Shehia ya Kinyikani Wilaya ya Wete Pemba katika muendelezo wa mikutano ya kutoa elimu ya rushwa na uhujumu wa uchumi kwa shehia za Unguja na Pemba.

Shuwekha amewataka wanavikundi hao kutolipa katika risiti ambazo hazitambuliki serikalini kwani kufanya hivyo serikali inakosa fedha muhimu ambazo zingeweza kuendeleza miradi muhimu ya  maendeleo.

Nae Afisa kutoka mamlaka hiyo Saumu Ramadhan  Haji  aliwataka wanavikundi hao kutokubali kutoa, kupokea au kushawishi kutoa rushwa kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Saumu ameeleza kuwa ukosefu wa elimu ya rushwa kwa wanavikundi hao unasababisha ongezeko la rushwa katika jamii kwani baadhi yao wamekua wakitoa fedha hata kwa mambo wanayostahiki kupata bila ya kutoa fedha za aina yoote.

Kwa upande wa Mussa Suleiman Said amewaomba maafisa hao kutoa elimu maalum kwa wananchi wote ili kuweza kuzitambua risiti halali na zisizo halali ili waweze kuwaepuka watoaji risiti wasiojali maendeleo ya nchi na kujali maslahi ya maisha yao tu.


Jumla ya vikundi 10 vilipata elimu hiyo ambavyo ni “jiwezeshe, jikomboe, mkataa umoja, bora juhudi zeru, baada ya dhiki faraji, mtarazaki hachoki, tumekusudia, bado tuko hai, mwanzo mgumu na tuimarike vyote kutoka shehia ya Kinyikani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.