Habari za Punde

Onesho la Kusaidia Kuchangia Wagonjwa wa Maradhi ya Kensa Zanzibar Kufanyika Oktoba 8 Zanzibar.

 
Mbunifu wa Mavazi nchini Kurwa Mkwendule, akizungumza na waandishi jinsi ya maandalizi ya onesho hilo la aina yake linalotarajiwa kuwashirikisha warembo wanawake wanene Zanzibar na kuwataka wananchi kijitokeza katika shoo hiyo na kuchangia.
Mdhamini wa Maonesho ya Mavazi kuchangia Wagonjwa wa Kensa Zanzibar Bi Wahida Walid, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matayarisho ya shoo hiyo inayotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa hoteli ya Grand Palace Malindi Zanzibar na kuwahamasisha Wanawake kujitokeza katika onesho hilo litakalowasirikisha Wanawake wanene kuonesha mitindo ya mavazi siku hiyo. 
Nadya Jamishad, wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena Inn, juu ya matayarisho hayo.

Na Abdi Shamnah
Zaidi ya asilimia 45 ya wanawake  waliopo Zanzibar, ikiwemo wanaojifahamu na wasiojifahamu, wanaishi na aina tofauti za ugonjwa wa Saratani, ikiwemo ya matiti na aina nyenginezo.

Changamoto hiyo imetolewa na Mdhamini wa harambee ya kuhamasiha uchangiaji wa fedha, kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa saratani ya matiti ‘Breast Cancer Awareness’, Nadya Jamishad, wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena Inn, mjini hapa.

Mbunifu wa Mavazi nchini Kurwa Mkwendule kwa kushikiana na Titi Ngazi, wameandaa onyesho maalum la ubunifu wa mavazi na onyesho la wanawake wanene ‘Marashi ya Pwani Size Fashion show, litakalofanyika Oktoba 8 mwaka huu, katika ukumbi wa Grand Palace Malindi Zanzibar, Kongwe, kwa lengo la kuchangisha fedha kusaidia wagonjwa wanaoishi na saratani ya matiti Zanzibar.

Alisema tafiti zilizofanywa zimebaini kuwa  Wazanzibari an Watanzania kwa ujumla wanaguswa kwa namna moja au nyengine na kuwepo kwa ugonjwa huo, hata hivyo tatizo kubwa liliopo ni ukosefu wa uwelewa na namna ya kuukabili ugonjwa katika hatua za awali.

Alisema wengi wa wagonjwa wanaofika hospitali kupatiwa matibabu, hufanya hivyo wakati ugonjwa ukiwa umewatopea katika viwiliwili vyao.

‘‘Mi mwenyewe ni muathirika miongoni mwa saratani, wengi wa wagonjwa kutoka Zanzibar hukimbilia Ocean Road, kati yao wengi wanauguwa saratani ya matiti na kensa ya kizazi’, alisema.

Aidha alisema tatizo la uwelewa juu ya ugonjwa huo, hususan kwa wananchi kisiwani Pemba, ni tatizo linalohitaji kuchukuliwa hatua madhubuti, ili jamii iweze kufahamu namna ya kuukabili na kuchukua hatua za haraka pale wanapoonesha dalili za kuwa na ugonjwa huo.

‘‘ Hali hii pia inatokana na Hospitali ya Mnazi Mmoja kutokuwa na kitengo cha kufuatilia mwenendo wa maradhi hayo pamoja na utaratibu wa kupima wananchi kila badaa ya kipindi fulani’’, alisema.  

Alibainisha miongoni mwa vyanzo vya maradhi ya saratani ya aina zote, hutokana na jamii kubadili mfumo wa vyakula kutoka vile vya asili na kujikita katika ulaji wa vyakula vyenye kemikali.

Mdhamini huyo alisema kupitia onyesho hilo, wamekusanya nguvu ili kuishajiisha jamii ya Wazanzibar kutoa michango yao kwa ajili ya kuwasadia watu wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

Nae Wahida Walid aliwataka wafanyabiashara na watu wote nchini kujitokeza kuchangia kwa hiari, ili kufanikisha juhudi za kuwasaidia watu wanaoguwa ugonjwa huo.

Alisema harambee hiyo, ambapo baadhi ya wasanii mashuhri watashiriki kwa lengo la kutia hamasa, imepata baraka zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Mapema Mbunifu wa mavazi Kurwa Mkwendule, alisema katika onyesho hilo wanamitindo maarufu an wanaochipukia kutoka Tanzania na Bara na Zanzibar, watashiriki, sambamba na wasanii, akiwemo Khadija Koppa, Jaffar Bhai na Wastara. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.