Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar Yapokea Vifaa vya Kutendea Kazi kutoka Shirika la TPHS.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dk Malik Juma Akili, akipokea Vifaa vya Kutendea Kazi kwa Ajili ya Matumizi ya Hospitali ya Mnazi Mmmoja Zanzibar kutoka kwa Meneja wa Taasisi inayopiga Vita Maambukizo ya  Ukimwi Tanzania (TPHS) Frida Godfrey, makamidhiano hayo yamefanyika katika viwanja vya Wizara ya Afya Mnazi Mmoja leo 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya akitoa shukrani kwa Taasisi ya TPHS baada ya kupokea msaada wa komputa, Printer na UPS katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
 Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

Na Miza Kona/Mwanaisha Mohamed - Maelezo Zanzibar.                                                             
Taasisi inayopiga vita maambukizi dhidi ya maradhi ya ukimwi Tanzania (TPHS) imeikabidhi Wizara ya Afya  msaada wa vifaa vya kutendea kazi kwa ajili ya matumizi  ya wadau wa afya kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Vifaa vilivyokabidhiwa vikiwa na  thamani ya sh. milioni 27,820,000 ni pamoja na komputa 10, Printer saba  na UPS.

Akikabidhi msaada huo Meneja wa Taasisi hiyo Frida Godfrey Radegunda katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, amesema lengo  ni kuimarisha vitendea kazi  katika kutoa huduma bora za Afya kwa jamii.

Amesema Taasisi hiyo kwa kushirikana  na Wizara ya Afya itaendelea kutoa  huduma na kuwawezesha wananchi kuelewa njia za  kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi ya ukimwi

“Taasisi yetu inashirikiana na wizara ya Afya kupambana na madawa ya kulevya katika vituo vya afya na kutoa elimu ya ukimwi na madhara ya kujidunga sindano, ” amefahamisha Meneja huyo.

Aidha amewataka wadau wa Afya kuvitumia vyema vifaa hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu ili kufikia lengo lililokusudiwa la kutoa huduma  bora kwa wananchi.

Katibu Mkuu Wizara ya  Afya Dkt Malik Juma Akili ameishukuru Taassisi ya TPHS kwa msaada huo pamoja na  kuisaidia kutoa elimu kwa jamii dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.

Amesema vijana wengi wanaathirika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na kupelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la maambukizi ya ukimwi kwa kujidunga sindano ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

“Vijana wasikilize yale wanayoelekezwa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi kiwango cha maambukizi ni kikubwa Unguja ni asilimia 1.2 na Pemba ni 0.3 tusjiachie tujitahidi katika kupunguza,” alisisitiza Dkt. Malik.

Aidha Katibu Mkuu  ameishukuru Taasisis hiyo kwa kufanikiwa kuifanyia matengezo Maabara kuu ya Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa lengo la kuboresha  huduma kwa jamii pamoja na kukisaidia kituo cha huduma ya kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya  kupata nafuu (Methodone Clinic ).

Mapema Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad amesema kitengo cha Mfamasia Mkuu kilikuwa na upungufu  wa vitendea kazi lakini  msaada huo utasaidia  kutoa huduma  kwa ufanisi zaidi.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa Tume ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bohari Kuu ya dawa pamoja na Hospitali ya Mnazi Mmoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.