STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.09.2016
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali
itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa mazingira ya kazi pamoja na
maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya
habari vya serikali yanaimarishwa ili kurejesha hadhi ya taasisi hizo.
Dk. Shein ambaye alivitembelea vyombo vya
habari vya Redio pamoja na gazeti la Zanzibar Leo na kufanya mahojiano maalum
na Shirika la Habari na Utangazaji Zanzibar ZBC, alisema ameridhishwa na
utendaji wa kazi wa viongozi na wafanyakazi wa vyombo hivyo ambao amesema,
wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi vizuri licha ya changamoto kadhaa
wanazokabiliana nazo.
Amesema Serikali imedhamiria kulifanyia
marekebisho makubwa Shirika la Habari na Utangazaji Zanzibar na vyombo vyote
vya habari vya Serikali sio tu kwa kuinua viwango vya mishahara ya
wafanyakazi, lakini vile vile kuweza
kutoa tuzo maalum kila inapohitajika kufanya hivyo kwa wafanyakazi watakaofanya
kazi zao vizuri kuinua ari na motisha wa wafanyakazi.
Ameongeza kuwa mchakato unaendelea wa
kutayarisha na hatimaye kurejesha miundo ya utumishi “scheme of service” ambayo
kwa kiasi kikubwa nayo iterejesha heshima ya kazi ambayo ilionekana kupungua
siku za hivi karibuni ikilinganishwa na miaka iliyopita wakati ilipokuwa
ikitumika vyema.
Amefahamisha kuwa katika hatua za awali
kuelekea kuziimarisha taasisi za vyombo vya habari vya Serikali, Serikali
imeshatoa agizo kuitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuandaa
posho maalum kwa wafanyakazi ambao wanajulikana kuwa wanafanyakazi katika
mazingira magumu.
Akizungumzia baadhi ya wafanyakazi ambao
wameondoka kwenye vyombo vya habari vya Serikali kutokana na maslahi duni na
mazingira yasiyoridhisha, Rais wa Zanzibar alisema ana matumaini makubwa kwamba
wengi miongoni mwa wafanyakazi hao wataweza kurejea siku zijazo kama ambavyo
wamekuwa wakifanya wengine wengi kwenye taasisi mbali mbali.
“nyumbani ni nyumbani, naamini iwapo
tutaimarisha mazingira bora ya kazi watarejea, wengi tumewaona wakirejea
kutokana na mapenzi yao na nyumbani” alisema.
Amesema pamoja na ukweli kwamba katika
kipindi cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya saba
ilifanya mabadiliko makubwa ya mishahara ambayo hayajawahi kufanywa kabla, wapo
baadhi ya watumishi wa umma ambao kwao bado viwango hivyo vya mishahara
havijawaridhisha sana.
Hata hivyo Dk. Shein alielezea matumaini
yake kwamba katika kipindi cha miezi sita au saba ijayo, hali ya vyombo vya
habari vya Zanzibar itabadilika na kwamba watu wengi watavutiwa kufanyakazi
kwenye vyombo hivyo.
Kuhusu gazeti la Zanzibar Leo, Rais wa
Zanzibar alisema Serikali imeshanunua mitambo mipya ya kisasa ya uchapishaji
ambayo itatumika pia, kuchapishia gazeti
hilo badala ya kuchapishwa nje ya Zanzibar, jambo linalosababisha mrundikano
mkubwa wa deni la gharama za uchapishaji.
Nao wafanyakazi na watendaji wa vyombo
hivyo vya habari walitoa pongezi zao za dhati kwa Dk. Shein kwa kufanya ziara
yake hiyo ya hafla ya kuwatembelea pamoja na kuwasikiliza changamoto
walizonazo.
Jumamosi iliyopita, Rais wa Zanzibar
alikutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Uongozi
wa Shirika la Habari na Utangazaji Zanzibar (ZBC) pamoja na Uongozi wa Zanzibar
Leo kuzungumzia njia ambazo zatasaidia
kuimarisha zaidi matangazo ya Redio na TV za Shirika la Habari na Utangazaji
Zanzibar – ZBC.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment