Habari za Punde

Wasiokuwa na uraia wa nchi yoyoyte nao wajadiliwe - Tanzania

WASIOKUWA NA URAIA WA NCHI  YOTE YOTE  NAO WAJADILIWE-TANZANIA


Na Mwandishi Maalum, New  York

Tanzania  imeitaka jumuiya ya  kimataifa   kujadili  tatizo  la  uwepo wa watu  ambao si raia wa nchi  yoyote ile.

Pendekezo hilo limetolewa siku ya  Jumanne na Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Dkt. Augustine Mahiga ( Mb)    katika  mkutano     wa  Kilele wa  viongozi  kuhusu wakimbizi.


Mkutano huo  uliandaliwa na  Rais wa Marekani Barack Obama  kwa  ubia na nchi za  Ethiopia, Jordan, Mexico, Sweden, Canada  na Ujerumani  ambapo nchi  60  zilialikwa,45 kati ya zilizoalikwa ikiwamo   Tanzania    zilitoa ahadi ya  namna moja ama  nyingine. 

Nchi  hizo ni zile ambazo kwa namna moja ama nyingine   zimekuwa zikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi,  zimekuwa nchi za mpito kwa wakimbizi, au zimekuwa  zikitoa misaada   ikiwamo ya  hali na mali pamoja na kuwapatia uraia, ajira na  misaada ya kibinadamu.

Lengo kuu la mkutano  huo wa  viongozi kuhusu wakimbizi lilikuwa ni kwa nchi kutoa ahadi mpya ambazo  kwayo  zitasaidia katika  kuwapatia fursa za ziada  wakimbizi ili  pamoja na mambo mengine kuwapunguzia changamoto zinazowakabili na kuwafanya wajisikie na kujiona  kuwa  nao ni  binadamua kama  binadamu  wengine.

Akizungumza kwa  niaba ya Serikali,   Waziri Mahiga, amesema, Tanzania  kutokana na jiografia ya nchi hiyo  ilivyo imejikuta  mara kwa mara ikiwa ni kimbilio  la wakimbizi kutoka  nchi jirani.

Akawaeleza  washiriki wa mkutano huo, kwamba, suala la  Tanzania  kuwahifadhi  wakimbizi ni la kihistoria na  halikuanza  jana au juzi.

“ Tanzania kutokana na jiografia yake imejikuta  ikiwa ni kimbilio wa watu wanaotafuta salama ya maisha yao. Tumekuwa  tukiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi  tangu miaka  ya 60.  Na  tunatekeleza   jukumu hilo kwa kuzingatia sheria  za kimataifa na mikataba ya kimataifa, na sheria zetu za ndani” akasema Mahiga.

 Na kuongeza kwamba, Tanzania itaendelea na jukumu hilo pale itakapopashwa  kufanya   hivyo kwa  kufuata na kuzingatia sheria  za nchi na  sheria za kimataifa.

“Tumekuwa  tukitiliza mkazo na kujadili mara kwa mara   tatizo  la wakimbizi na  changamoto wanazokabiliana nazo. Na mshukuru Rais Obama kwa kuitisha mkutano huu. Lakini  kuna jambo jingine   muhimu   na ambalo  tunatakiwa  tulijadili pia . Na  hili linahusu uwepo na kuendelea kuongeza wa idadi ya watu hususani vijana ambao hawana uraia wa  nchi yoyote ile ( stateless people).
Waziri wa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  akielezea zaidi  kuhusu changamoto hiyo ya uwepo wa  watu ambao hawana uraia wa nchi  yoyote ile.  Amesema  tatizo hilo  linaonekana zaidi katika eneo la Kusini na  Eneo la  Maziwa Makuu.

“ Tunapo jadili namna ya kuwasaidia wakimbizi, ni vema  pia tukatambua kwamba kuna tatizo kubwa la uwepo wa watu ambao hawajasajiliwa na hawana uraia  wa nchi  yoyote. Na tatizo hili ni kubwa  na linazindi kuongezeka na lipo zaidi kwa kizazi cha  sasa, hawana uraia. Tunatakiwa kulijadili tatizo hili”. Akasisitiza Waziri Mahiga.

Na kubainisha  kuwa Tanzania, ikiwa  ni   mwanachana wa  SADC na  EAC itaangalia uwezekano   wakuipekea  mezani  ajenda hiyo kupita  Taasisi hizo mbili.

Kwa pande wa ahadi  za ama nini  zaidi Tanzania itawafanyia wakimbizi , Waziri amesema  pamoja na  ahadi ya kuendelea kuwapokea wakimbizi pale inapobidi kufanya hivyo, Tanzania pia  kupitia sheria zake  itawasaidia watoto wakimbizi  kupata huduma za jamii  zikiwamo za elimu na afya,   na   kwa wakubwa fursa za kujiajili  hususani katika sekta ya kilimo iliwe waweze kuzalisha  chakula na kujiajili kupitia kilimo.

 Ahadi nyingine ni  pamoja na kutowarudisha   kwa nguvu wakimbizi katika nchi walizotoka.

Katika mkutano huo ambazo uongozi wa Juu wa  Serikali ya  Obama  ulikuwapo  kuanzia  Makamu wake Joe Biden na Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry, Rais Obama kwa  upande wake alitoa  ahadi za kuongeza idadi ya wakimbizi watakaoingia  nchini Marekani pamoja na  kuongeza misaada ya kifedha kwaajili ya misaada na huduma za kijamii pamoja na kuzisaidia nchi zinazobeba mzigo wa wakimbizi.

Barack Obama ambaye anaelekea ukingoni mwa uongozi wake, amesema jumuiya ya kimataifa haipashwi kufanya kazi kwa mazoea na hasa katika eneo hilo la   wakimbizi  eneo ambalo anasema linahitaji ushiriki na ushirikiano wa kila nchi bila ya kujali ukubwa  au udogo wake,ajiri au  umaskini wake.

 Mkutano  huo   mbali ya Marais, Wafalme, Mawaziri Wakuu na  Mawaziri kuzungumza pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye alizungumza pamoja nna Mkuu wa Banki  ya Dunia.

Ni mkutano ambao ulikuwa ni mwendelezo wa majadiliano ambayo yalifanyika siku ya  Jumatatu kuhusu ajenda ya wakimbizi  na wahamiaji kama changamoto ya dunia  hivi sasa.

Licha ya machafuko na vita, suala ya umaskini, uongozi mbovu na  watu kutokuwa na matumaini  ni maeneo ambayo yameelezwa kuchangia  katika  uongezeko la wakimibizi.

Pamoja na  kuandaa na kushiriki mkutano  wa viongozi  kuhusu wakimbizi, Rais wa Marekani Barack Obama siku hiyo ya jumanne alilihutubia kwa mara ya mwisho  Baraza Kuu la  71 la Umoja wa Mataifa,  ambapo aliainisha masuala mbalimbali yanayoikabili dunia  hivi sasa yakiwamo ya ugaidi, mabadiliko ya tabia nchi, ukiukwaji  wa haki za binadamu, ukiukwaji wa  utawala wa sheria na demokrasi, milipuko ya magonjwa kama  vile Ebola na  Zika,  matumizi ya  diplomasia katika kutafutia ufumbuzi masuala magumu likiwamo la mchakato wa kuidhibiti Iran dhidi ya  silaha za  nyukilia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.