Na Mwanaisha
Mohammed-Maelezo.
Wazara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeshauriwa kuanzisha mitaala
itakayowafundisha wanafunzi mbinu za kujiepusha na vishawishi vya ngono
vinavyoweza kuwaletea madhara na mbimba za umri mdogo.
Mjumbe wa
Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Fatma
Iddi Ali, amesema mafunzo hayo ni muhimu ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya
watu waovu.
Ushauri huo
ameutoa wakati akiwasilisha mada kwenye warsha ya mafunzo kuhusu vitendo vya
udhalilishaji inayofanyika katika ukumbi wa Idara ya watu wenye ulemavu
Kikwajuni mjini Zanzibar.
Fatma
ametaja madhara yatokanayo na mimba za umri mdogo ikiwemo vifo vya mama na watoto
na kuharibika kwa mfumo wa uzazi.
Alieleza
kuwa kuathirika kwa kizazi husababisha mama kutolewa fuko la uzazi na hivyo kumfanya asiweze kubeba ujauzito kabisa.
Aidha amewakumbusha
wazazi wajibu wa kukaa na kuzungumzana watoto ili waweze kufahamu matatizo waliyonayo
na kutafuta njia za kuyatatua mapema.
Mjumbe huyo
wa ZAFELA pia amekumbusha jukumu la wazazi na wanajamii kurejesha malezi ya asili
na kushirikiana katika kuwalea watoto ili wakue katika maadili mazuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Saada Salum Issa,
amewahimiza wazazi kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao maskulini,
hasa katika masomo ya ziada (Tuitions) kwani baadhi yao huitumia fursa hiyo kujiingiza
katika vitendo viovu.
“Pamoja na
hayo, wazazi pia wanapaswa kutowadekeza mno watoto wao kwani kufanya hivyo kutawapa kiburi na kuvuka
mipaka ya nidhamu,” alisema.
Katika hatua
nyengine, Mwenyekiti huyo amewaomba wazazi na walezi wasiwape simu watoto
wakiwa wanafunzi, akisema teknolojia hiyo inachangia katika kuwapotosha kwa
vile wanaitumia vibaya badala ya kujifunza mambo ya maana yaliyomo ndani yake.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI MAELEZO
No comments:
Post a Comment