Habari za Punde

Afikishwa mahakamani baada ya kupatikana na madawa ya kulevya

Hassan Khamis, Pemba

KIJANA Saleh Iddi Ali (32) mkaazi wa Jadida Wete, ametupwa rumande kwa muda wiki mbili baada ya kupandishwa katika kizimba cha mahakama ya Wilaya hiyo, akikabiliwa na tuhuma za kupatikana na madawa ya kulevya.

Mwendesha mashtaka kutoka Jeshi la Polisi Ali Ahmada alidai mahakamani hapo kuwa, Mei 27,mwaka huu majira ya saa 2:30 asubuhi Mtemani mtuhumiwa alipatikana na kete 37 za unga unaosadikiwa kuwa ni madawa ya kulevya aina ya “kokeni” zikiwa na uzito wa gramu 0.830 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kupatikana na unga wa madawa ya kulevya ni kosa kinyume na kifungu cha 16(1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009 sheria ya kuzuia uingizaji na matumizi ya madawa ya kulevya sheria ya Zanzibar.

Mara baada  ya mtuhumiwa kupandishwa kizimbani hapo  na  kusomewa shtaka lake mbele ya hakimi Makame Nyange, alitakiwa kutojibu kitu chochote na alifahamishwa kuwa dhamana yake haipo wazi kwani shtaka  lake lilipaswa kusikilizwa katika mahakama ya Mkoa.

Alielezwa kuwa, kutokana na dharura ya hakimu wa mahakama ya Mkoa ndio maana shtaka hilo lilisikilizwa katika mahakama ya Wilaya.


Kutokana na mahakama hiyo kutokua na uwezo kisheria kusikiliza shauri hilo, mtuhumiwa amepelekwa rumande hadi Oktoba 10, mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa katika mahakama ya Mkoa wa kaskazini Pemba iliyopo Wete,

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.