Hassan Khamis, Pemba
JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini
Pemba, linamshikilia mama wa miaka (44) baada ya kukamatwa na lita 66. 5 za
ulevi wa kienyeji aina ya gongo na bangi nyongo 61 pamoja na furushi moja kijiji
cha Bungala Wilaya ya Wete Mkoani humo.
Kaimu
kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, ambae pia ni Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba Issa Juma Suleiman amemtaja mama huyo kua ni Rehema Mikwaba
Mabanga mkaazi wa Bungala Wete.
Ameongeza
kuwa Septemba 27, mwaka huu majira ya saa 7:15 mchana kijijini hapo, mama huyo
alipatikana na madumu matatu yenye ujazo wa lita 20 kila moja, na chupa moja ya
drop yenye ujazo wa lita moja na nusu ndani yake ikiwa na ulevi wa kienyeji
aina ya gongo.
Kamanda Issa
amefafanua, mara baada ya askari kufika nyumbani kwa mama huyo, wakiongozwa na
sheha wa shehia ya Kinyasini na kufanikiwa kukamata gongo hiyo, waliendelea na
upekuzi na walifanikiwa pia kupata nyongo 61 pamoja na furushi moja la bhangi.
Alisema
waligundua madawa hayo yakiwa yamehifadhiwa katika mfuko wa plastiki uliokuwepo
ndani ya nyumba ya mama huyo.
Kamanda Issa
alifafanua kuwa, askari walipata taarifa kutoka kwa raia wema, kuhusu taarifa
za mama huyo kujishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya na pombe za
kienyeji na kuamua kumuwekea mtego ambao ulifanikiwa.
“Ni taarifa
za raia weme ndio ambazo zilitusaidia sisi kumkamata mama huyu, na hivi ndio
ambavyo huwa tunawataka wananchi washirikiane na Jeshi letu kwa ajili ya
kufichua uhalifu’’,alifafanua.
Ametoa wito
kwa wananchi kushirikiana na jeshi la Polisi ili kupinga biashara ya madawa ya
kulevya na kutoa taarifa polisi ili kuwafichua wale wote wanaojishughulisha na
biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Hata hivyo
alisema kuwa mama huyo anatarajiwa kufikishwa mahakani mara tu upelelezi wa
shauri lake utakapokamilika.
No comments:
Post a Comment