STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.10.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Mazingira ikiwa ni pamoja na azma ya kuupandisha
hadhi msitu wa Masingini kuwa msitu wa hifadhi.
Hayo aliyasema leo katika
kikao maalum kilichofanyika, Ikulu mjini
Zanzibar ambapo Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Mazingira ilipowasilisha
Taarifa yake ya Utekelezaji wa Mpango Kazi
wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai
hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuziimarisha
sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutambua umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo
ya nchi pamoja na wananchi wake.
Dk. Shein alisisistiza
haja ya kuendeleza mchakato wa kuanzisha kiwanda cha matreka hapa nchini kama
ilivyoamua Serikali, kwani tayari hatua za awali zimeshafanyika kwa kuzingatia
kuwa kilimo huimarika panapokuwa na huduma za matrekta.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuwepo Baraza moja la
kilimo ambalo litakuwa na nguvu kubwa ya kufanya kazi huku akitilia mkazo kuongezwa
nguvu katika maendeleo ya mifugo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza haja kwa uongozi wa Wizara hiyo kuendelea na juhudi za kuulinda msitu
huo wa Masingini ili kuepuka kuja kuvamiwa kwa ujenzi huku akitumia fursa hiyo
kuitaka Wizara hiyo kusimamia na kudhibiti vyema maliasili zisizorejesheka ili
kuepuka athari zaidi za hapo baadae.
Mapema Waziri wa
Kilimo, Malisili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohamed alisema kuwa sekta ya
kilimo inajumuisha sekta ndogo za mazao, mifugo, uvuvi na misitu bado inaendelea
kuwa ni mhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar na inatoa mchango wa moja kwa moja
katika kujikimu kimaisha.
Alisema kuwa sekta
hiyo imekuwa ikitoa ajira rasmi kwa wastani wa asilimia 40 na zaidi ya asilimia
70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo kwa njia moja au nyengine katika
kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.
Alisema kuwa muelekeo
wa Wizara hiyo ni kuendeleza mageuzi ya sekta ya kilimo kwa lengo la
kukibadilisha kilimo kutoka cha kujikimu kuwa cha kibiashara pamoja na kuongeza
tija na kipato kwa wazalishaji na kupunguza kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.
Akieleza miongoni mwa
mafanikio yaliopatikana Julai hadi Septemba mwaka huu, Waziri huyo alieleza
kuwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wafugaji wa ngombe wa kisasa, kufundisha
mabwana mifugo binafsi wa vijijini, kuimarika huduma za ugani, kuongezeka kwa
uzalishaji wa mayai, kuendeleza miundombinu ya utafiti na mengineyo.
Pamoja na hayo, Waziri
huyo wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alieleza kuwa Wizara kwa
kushirikiana na uongozi wa Mikoa, Wilaya, Shehia na Jumuiya za wakulima
inaendelea kuhamasisha wakulima wachangine kwa wakati huduma za matrekta ili
kuwahi msimu wa kilimo cha mpunga.
Uongozi huo pia,
ulieleza azma yake ya kuupandisha hadhi msitu wa Masingini kuwa msitu wa
hifadhi kwani sifa zote za kuwa msitu wa hifadhi na umekuwa kivutio kikubwa cha
watalii kutokana na vivutio vilivyomo ndani yake.
Nae Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, aliipongeza Wizara hiyo kwa kuwasilisha
vyema Mpangokazi wake na kusisitiza haja ya kuendelea na mikakati ya kudhibiti
misumeno ya moto kwa mashirikiano ya pamoja.
Dk. Katibu Mkuu wa
Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alielza
haja y kwa uongozi wa Wizara hiyo kuwahamasisha wananchi katika matumizi ya
majiko ya gesi ili kuepuka matumizi ya kuni na makaa.
Aidha, aliupongeza
uongozi wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wake kwa matayarisho mazuri ya
Mpangokazi huo huku akitaka juhudi za makususdi ziendelee kuchukuliwa katika
kulipatia ufumbuzi suala la bei ya kilimo cha mwani.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment