Habari za Punde

Dk Shein, Azungumza na Watendaji wa Wizara ya Fedha Ikulu Zanzibar leo.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                          19.10.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Fedha na Mipango iko vizuri katika ukusanyaji wa mapato.

Dk. Shein aliyasema hayo,   Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati yake na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango mara baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya Utekelezaji wa Kazi za Wizara  hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajiweza na iko vizuri katika ukusanyaji wa mapato yake hali ambayo inatoa mwanga wa mafanikio katika kuendeleza shughuli zake za maendeleo na kukuza uchumi.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendesha vizuri matumizi ya kawaida kwa Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuziwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Taasisi za ukusanyaji wa mapato katika Wizara hiyo kwa kuendelea kukusanya mapato ipasavyo na hatimae kusaidia na kukuza uchumi wa nchi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kutenga bajeti maalum kwa ajili ya utafiti hapa Zanzibar kwani maendeleo ni utafiti.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema mpango wake wa kazi katika utekelezaji wa Bajeti ya Julai hadi Septemba mwaka 2016-2017 na kusisitiza haja kuongeza juhudi katika kufanya tafiti mbali mbali ndani ya Wizara hiyo.

Mapema Kaimu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Salama Aboud Talib alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango ina jukumu la kusimamia masuala ya Fedha za Umma kama ilivyoelezwa ndwani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Sura ya Saba.

Alisema kuwa  miongoni mwa majukumu hayo ikiwemo kukusanya rasilimali fedha za Serikali, kuzigawa rasilimali hizo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali na kusimamia matumizi yake.

Aidha, alisema kuwa Wizara inatekeleza majukumu na shughuli zake kwa kufuata miongozo na sheria mbali mbali za Wizara zinazohusu masuala ya usimamizi wa fedha na Mipango ya Kitaifa.

Pamoja na hayo, uongozi huo wa Wizara ya Fedha ulitoa pongezi kwa Rais kwa kuendelea kuwapa miongozo mizuri ambayo imekuwa chachu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.