Habari za Punde

Hotuba ya Mhe. Angellah Jasmin Kairuki (MB),Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Tume ya Kudumu ya Uchaguzi,Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam,Oktoba 21, 2016

                                                         

Mhe. Othman Chande, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania;

Mhe. George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali;                                                                     

Mhe. Jaji (Mstaaf)  Damian Lubuva; Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa
Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mhe. Bahame Nyanduga, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora;
Wahe. Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
Ndugu Joseph Butiku, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere
Mwakilishi wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania;
Mhe Amiri  R. Manento (Jaji Kiongozi Mstaafu), Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
Wahe. Viongozi wa Serikali na Wawakilishi wa Vyama vya Siasa mliopo hapa;
Wawakilishi wa Asasi mbalimbali za Kiraia;
Viongozi na watumishi mbalimbali mliopo hapa;
Ndugu Wana Habari;
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

Habari za Asubuhi!

Napenda nianze, kwa kutoa salamu kutoka kwa Mhe. Dr John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ndiye alitegemewa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho haya siku ya leo, lakini  kutokana na majukumu yake mengi ya kitaifa ameniagiza nimuwakilishe.

Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wageni waalikwa kutoka nje ya Nchi waliokuja nchini kwa ajili ya maadhimisho haya, poleni na safari ndefu na karibuni sana Dar es Salaam. Niwapongeze nyote mliofika mahali hapa naamini mmefanya hivi kutokana na sababu moja tu kubwa, nayo ni kwamba; kila mmoja wenu anathamini na kujali umuhimu wa kujenga taasisi za uwajibikaji na utawala bora. Binafsi nimefurahi kujumuika nanyi na kuwa sehemu ya washiriki wa tukio hili muhimu na la kihistoria. Ni matumaini yangu kuwa wageni wetu mkiwa hapa mtapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyoko Nchini mwetu, kama vile mbuga za wanyama, mji wa kihistoria wa Zanzibar, mlima mrefu kupita yote Afrika Mlima Kilimanjaro na ni matumaini yangu kuwa mtafurahia vivutio hivyo na kuwa kumbukumbu katika safari na maisha yenu.

Niwashukuru Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (The Mwalimu Nyerere Foundation) kwa jitihada zao kubwa za kuandaa, kuratibu na hatimaye kufanikisha Maadhimisho haya. Hongereni sana!

Ndugu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, waheshimiwa viongozi na wageni waalikwa, Ni heshima kubwa kwa Taifa letu  kuadhimisha kumbukumbu ya miaka hamsini katika kushughulikia malalamiko ya Wananchi waliohisi wameonewa kupitia  Tume ya Kudumu ya Uchunguzi hapo nyuma na hivi sasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Historia inatukumbusha kuwa, baada ya kupatikana uhuru mwaka 1961, taifa letu likiwa changa Serikali ilichukuwa hatua mbali mbali za kuunda vyombo vyake ili kuwahudumia Wananchi wake.  Kwa nia njema kabisa, moja ya hatua hizo ilikuwa kuunda chombo chenye madaraka ambacho kitasimamia utendaji wa Viongozi waliokuwa katika Chama, Serikali na Mashirika ya Umma.  Hivyo pendekezo la kuundwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi lilitokana na Taarifa ya Tume ya Rais iliyoundwa Mwaka 1964 ili kukusanya maoni kuhusu Muundo wa Serikali ya Kidemokrasia ya Chama kimoja cha siasa.

Katika taarifa yake ambayo ilitolewa mnamo tarehe 22 Machi, 1965 Tume hiyo kwa kifupi ilishauri kuundwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kama chombo ambacho kitadhibiti matumizi ya madaraka waliopewa Viongozi na wakati huo huo kutetea Wananchi ambao haki zao zitakuwa zimevunjwa au ziko katika hatari ya kuvunjwa.

Chama na Serikali vilikubali pendekezo hilo na Tume ya Kudumu ya Uchunguzi ikaingizwa rasmi kwenye Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Interim Constitution) ya Mwaka 1965.  Mwaka 1966 Bunge lilipitisha Sheria (Act No. 25 of  1966) ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi iliyoiwezesha kutekeleza shughuli zake za kila siku. Kwa kuwa chombo hicho kilikuwa cha Muungano, Mwaka 1980 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliridhia Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kufanya kazi zake Zanzibar.

Ndugu
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Mwaka huu (2016) Tanzania inaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (TKU) au kwa neno maarufu “Ombudsman”. Neno “Ombudsman” ni neno lenye chimbuko la lugha ya Sweden likiwa na maana ya “Mlinzi” au “Mtetezi wa haki za jamii”.  Neno hilo lina asili ya Sweden kwani ndio nchi ya kwanza duniani kuanzisha  taasisi ya “Ombudsman” mwaka 1807. Nchi zingine za Ulaya kama Uingereza zina mtambua Kiongozi wa taasisi hiyo kama “Kamishna wa Haki”.

Majukumu ya taasisi hizi za “Ombudsman” ni kumlinda na kumtetea mwananchi mnyonge, kutokana na kuonewa na mifumo ya kiutawala au matumizi mabaya ya madaraka ya watendaji wa Serikali. Kulingana na maudhui ya taasisi ya “Ombudsman” Mwananchi anayepeleka malalamiko hupata huduma bila malipo, tofauti na mfumo wa kutafuta haki wa mahakama ambao umewekewa utaratibu unaohitaji malipo pale mtu anapotaka kufungua kesi.  Ofisi za “Ombudsman” hazina vikwazo (technicalities) katika kuwasilisha malalamiko na kuyafanyia uchunguzi .

Nina furaha kusema kuwa lengo kubwa la Serikali kuanzisha Tume ilikuwa ni kumlinda Mwananchi na liliweza kufikiwa kwa kupitia takwimu za malalamiko yaliyopokelewa katika kipindi cha miaka 35 ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi yaliyoshughulikiwa na kukamilishwa kwa kupatikana haki. Katika kipindi cha kuanzishwa kwake, jumla ya malalamiko 39,000 yalishughulikiwa.  Aidha malalamiko yaliyopokelewa katika kipindi cha miaka 15 (2001-2016) ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni 32,000 na hivyo kufanya idadi ya malalamiko yote katika miaka 50 kufikia 71,000. Idadi hiyo inaonesha jinsi vyombo hivi vilivyo na manufaa kwa Wananchi wanyonge. Baadhi ya  malalamiko yaliyopokelewa yalihusu masuala yafuatayo:-
·         Vitendo vya unyanyasaji,
·         Masuala ya Utumishi/malipo/mafao
·         Kuchelewa kutekeleza wajibu
·         Kukataliwa kuomba rufaa
·         Kutofuata taratibu za kisheria
·         Mirathi
·         Matumizi mabaya ya Mali ya Umma
·         Migogoro ya ardhi n.k.

Matokeo ya uchunguzi na mapendekezo ya Tume yalikuwa yanafanywa bila woga wala upendeleo na yanawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa maamuzi.

Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Yapo mafanikio mengi Nchi yetu inajivunia kwani pamoja na Wananchi kupata mwamko na kuwasilisha malalamiko yao kwenye Tume, zilianzishwa pia taasisi mpya za uangalizi (watch dog) kama Taasisi ya Kupambana na  Rushwa ambayo baadaye ilibadilika kuwa Taasisi ya Kuzuzia na Kupambana na Rushwa- TAKUKURU na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambazo zote ziliundwa kulinda utawala wa Sheria, uwajibikaji, maadili na demokrasia.

Napenda nichukue nafasi ya kipekee kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuanzisha Tume ya Kudumu ya Uchunguzi. Napenda pia kuwaenzi na kuwapongeza Wajumbe wa Tume iliyopendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi. Napenda pia nitumie nafasi hii kutoa pongezi za kipekee kwa Wenyeviti, Makamishna, Makatibu, na Watumishi wote waliotumikia Tume ya Kudumu ya Uchunguzi. Kwa wale waliopo nasi leo nawapongeza sana. Kwa wale wote waliotangulia mbele ya haki, pongezi hizi ziwafikie ndugu zao kwa niaba yao kwani mchango wao uliwezesha Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kuanzishwa kama taasisi ya kwanza ya “Ombudsman”, barani Afrika, Kusini mwa  jangwa la Sahara na kuendelea kutumikia Umma wa Watanzania kwa miaka 35 kama Mlinzi au Mtetezi wa Umma.

Wakati chombo hiki kikiendelea kufanya kazi kwa ufanisi kwa miaka zaidi ya 35,  dhana ya  haki za binadamu ikiwa sehemu muhimu ya Utawala wa Sheria, iliingizwa   katika Katiba za mataifa mengi duniani.  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu huo ilianzisha mchakato wa kurekebisha Katiba kwa kuingiza pamoja na mambo megine, masuala ya haki za binadamu.  Hivyo kutokana na mabadiliko ya Katiba ya 13 ya Bunge  la Katiba la mwaka 2000 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliingizwa kwenye Katiba. Kulingana na mabadiliko hayo majukumu ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi yaliunganishwa na majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, taasisi ambayo imeendelea na uchunguzi wa malalamiko dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka ambayo kama tulivyo ona yalikuwa yanashughulikiwa na Tume ya Kudumu ya Uchunguzi.

Nitoe wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kuyaenzi yale yote yaliyofanywa na Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kwa kuwa kazi zake bado zinahitajika sana katika jamii. Serikali itaendelea kushirikiana na Tume na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kutetea misingi ya Utawala Bora na kulinda haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

Aidha, napenda kutoa wito kwa Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi kuwahudumia Wananchi wote kwa usawa na kwa wakati ili kuleta ufanisi katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia Sheria za Nchi.

Kwa upande wa jamii ya Watanzania kwa ujumla natoa wito kwamba Utawala wa Sheria unamtaka mtu binafsi, taasisi za Umma, taasisi za Kitaifa, na Sekta Binafsi  kuheshimu misingi yote ya Utawala Bora, kama ilivyobainishwa na kauli mbiu ya maadhimisho haya kwamba “Utawala wa Sheria Ndio Nguzo Kuu ya Utawala Bora.”

Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima natamka kuwa; Kongamano la wadau kuadhimisha Miaka 50 ya ‘Ombudsman,’ sasa limefunguliwa rasmi.


Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.