Habari za Punde

Hotuba ya Bahame Tom Nyanduga, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Kuazishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (TKU),Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam, Tarehe 21 OKTOBA, 2016

Mhe. Angellah Kairuki,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Mzee Alhajj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Pili
Mhe. Mwakilishi wa Familia ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa,
Mhe. Mzee Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa,
Waheshimiwa viongozi wastaafu, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Awamu ya Pili,
Mhe. Joseph Butiku, Katibu Mtendaji,Taasisi ya Mwalimu Nyerere,  Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere,
Waheshimiwa Makamu Mwenyekiti, Makamishna, na Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,  
Mhe. Jaji Mstaafu Amir Manento, Mwenyekiti Mstaafu na Makamishna wataafu wa THBUB,
Waheshimiwa wawakilishi wa familia ya Wenyeviti, Makamishna na Makatibu wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, Waheshimiwa Mzee Malika na Mzee Guvette,
Mheshimiwa Balozi Katarina Rangnitt, Balozi wa Sweden hapa Tanzania,
Waheshimiwa Mabalozi mliohudhuria,
Waheshimiwa wageni wetu: Mhe. Caroline Sokoni, Rais wa International Ombudsman Institute, Kanda ya Afrika, na Mwenyekiti Tume ya Uchunguzi Jamhuri ya Zambia,
Mhe. Dk. Mohamed Rukara, Tume ya Uchunguzi, Jamhuri ya Burundi na Mhe. Dk. Otiende Amollo, Mwenyekiti Tume ya Utawala wa Sheria, Jamhuri ya Kenya, Katibu wa AOMA, na Mwakilishi wa Rais wa AOMA (AOMA ni Umoja wa Taasisi za Tume za Uchunguzi Afrika),
Mhe. Jaji Ahmed Abuzaid Ahmed, Rais wa Taasisi ya Uchunguzi, Jamhuri ya Kiislam ya Sudan,
Ndugu Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia, Waandishi wa habari, Mabibi na Mabwana,

Aslaam Alyekum.

Napenda kuchukua wasaa huu kuwakaribisha katika maadhimisho ya miaka hamsini ya kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (TKU) iliyoanzishwa mnamo mwaka 1965. Mchakato wa kuanzisha Tume ya Kudumu ya Uchunguzi ulianza mwaka 1965 ukakamilika mwaka 1966. Kwa hiyo leo hii tunaadhimisha mafanikio ya mchakato huo.

Nianze kwa kunukuu maneno ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika ukumbi huu,  tarehe 12 Oktoba 1965, na kazungumzia umuhimu wa kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi;
“…..[t]he other piece of constitutional machinery for which proposals will be submitted to Parliament is in connection with the Permanent Commission of Inquiry which must be established under chapter VI of the Interim Constitution of Tanzania. I have already stated my intention to appoint Chief Erasto Mang’enya as Chairman of this very important Commission. Parliament has yet, however, to prescribe the duties and powers of this Commission in so far as they are not laid down in the Constitution. I am confident that when the Bill is submitted to this House all Members will consider it carefully and seek to help Government make the Commission effective. We all know that there have been cases of abuse of power by persons in responsible positions. We must all be conscious, too, that while these continue our people do not live in conditions of complete freedom and justice such as they and we desire. I believe that through the work of this Commission the number of these abuses can be reduced, and that where they do occur the perpetrators can be discovered and disciplined and the sufferers relieved. If we succeed in this intention one further guarantee of freedom for our people will be instituted, without there being any possibility of licence hindering our national unity and development.”[1]

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa muumini wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora. Aliamini katika haki na umuhimu wa kuweka taasisi za uwajibikaji. 
 
Mwaka 1963 alipounda Tume ya Rais ya kuangalia namna ya kuanzishwa kwa demokrasia ya chama kimoja, Mwalimu Nyerere alitoa waraka ulioelekeza Tume hiyo kuzingatia masharti ya kazi yao, na  miongozo kadhaa katika kupendekeza jinsi Katiba za Tanzania, na ya chama cha TANU, zitakavyobadilishwa ili mfumo wa chama kimoja uzingatie demokrasia.

Akizungumzia Maadili ya Taifa, katika ibara ya 13 ya waraka huo, Mwalimu Nyerere aliainisha misingi minane ya maadili ya Taifa,  ambayo baadhi yake nitainukuu. Alisema yafuatayo;
“Kuna baadhi ya misingi ya maadili iliyo kiini cha Taifa la Tanganyika, na mipango yote ya Serikali kuhusu siasa, uchumi na ujamaa ni lazima vielekezwe katika kutimiza misingi hiyo ya maadili kwa haraka.
1)    Usawa wa binadamu wote na haki ya kila mtu kustahili heshima.
2)    Kila raia wa Tanganyika ni sehemu kamili ya taifa na anayo haki ya kushiriki kama wengine katika kazi za Serikali za mitaa, mikoa na Serikali Kuu.
3)    Kila raia anayohaki ya uhuru wa kusema, wa kwenda atakako, wa dini, na kwa kushirikiana kwa mujibu wa sheria, mradi adumishe uhuru kama huo wa raia wote.
...
8)    Taifa la wa-Tanganyika linapinga kabisa vitendo vya mtu kumdhulumu mwenzie, au taifa moja kudhulumu jingine, na kikundi chochote kudhulumu kingine…”

Mwalimu Nyerere aliongeza yafuatayo katika ibara ya 14 ya waraka wake kwa Tume;
“Katika kuifuata misingi hii lazima yapatikane maongozi ya kuleta kiunzi cha shughuli za siasa, uchumi na za ujamaa, nayo ni haya yafuatayo;
i)      Madhumuni ya Serikali yatakuwa ni kuimarisha usawa kamili wa kupewa nafasi kwa raia wote wa Tanganyika popote watakapoonyesha juhudi yao;
iv)   Raia wote wa Tanganyika watakuwa sawa chini ya sheria za nchi, na hakuna mtu yeyote, hata cheo kiweje katika siasa, au mbele za watu, au katika uchumi atakayeweza kuepuka sheria hizo.”[2]

Tunakutana hapa leo, miaka hamsini tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, ikiwa pia imepita miaka 17 tangu kifo cha Baba wa Taifa, ili kuadhimisha kumbukumbu ya kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, ikiwa ni taasisi ya kwanza ya “Ombudsman” kuanzishwa barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara.

Katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo kuna mambo makuu matatu, ambayo tutayakumbuka na kuyatafakari.

Jambo la kwanza ni kumuenzi  Baba wa Taifa, kwa kuanzisha taasisi hii ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, kama taasisi ya kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma kwa wananchi, nchini Tanzania. Msingi mkuu wa taasisi hii ni kuhakikisha kwamba watumishi wa umma, katika Serikali kuu, Serikali za mitaa na mamlaka zote zilizoko chini ya Serikali, wanatenda majukumu yao kwa kuzingatia sheria, haki, maadili na taratibu bila kutumia madaraka au mamlaka yao vibaya.

Ndiyo sababu Tume iliamua kuwa maudhui ya maadhimisho haya yabebwe na kauli mbiu ya “Utawala wa Sheria ndiyo msingi wa utawala bora.”  
Jambo la pili ni  kujikumbusha kwa kupitia mada zitakazotolewa, huko tulikotoka, na kujifunza kutokana na kazi za Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, changamoto zilizoikumba, mafanikio iliyoyapata, na mwelekeo unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba dhana ya uwajibikaji na utawala bora inaendelezwa nchini Tanzania, kwa kuzingatia misingi aliyotuachia Hayati Baba wa Taifa.

Ni kwa msingi huu basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliamua kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika kutayarisha maadhimisho haya.

Napenda kushukuru Bodi na uongozi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, kupitia Mwenyekiti wake, Dk. Salim Ahmed Salim, na Katibu Mtendaji, Mzee Joseph Butiku, na wajumbe wa Bodi walioko hapa, kwa kukubali ombi letu.

Jambo la tatu linahusu umuhimu wa maadhimisho haya siku hii ya leo tarehe 21 Oktoba. Kama nilivyosema pale awali, Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa haki za binadamu. Katiba ya TANU, na hata miongozo aliyoelekeza Tume ya Rais mwaka 1963, kuhusu kazi yao ya kupendekeza mfumo wa demokrasia ya Chama kimoja, zinaonyesha jinsi ambavyo alilielewa Azimio la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948.

Haki za Binadamu ziliingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, wakati wa awamu ya uongozi wake mwaka 1984.

Leo hii tunaadhimisha pia siku ya Haki za Binadamu ya Afrika. Ni siku ambayo Mkataba wa Afrika na Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981, ulipoanza kutumika hapo mwaka 1986, Tanzania ikiwa imeuridhia tarehe 18 Februari, 1984.

Tumebahatika kuwa pamoja na viongozi wastaafu ambao walihusika moja kwa moja katika kuanzisha na kusimamia utendaji au utekelezaji wa maamuzi ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi.

Napenda nitambue, kwa niaba ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, na Taasisi ya Mwalimu Nyerere,  uwepo wa Mzee wetu, Mhe. Al Hajj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya pili. Tumefarijika kuwa nawe Mzee wetu. Pia tunafarijika kuwa na mwakilishi wa familia ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Pia nichukue nafasi kutambua uwepo wa viongozi mbalimbali wastaafu wa Kitaifa. Tumebahatika kuwa na wageni kutoka nchi za nje na marafiki na wadau wa Tume.

Napenda nimtambue Balozi Katarina Rangnitt, Balozi wa Sweden hapa Tanzania atakaye tupa historia fupi ya jinsi taasisi za Ombudsman ziivyoanza huko Sweden. Tunaye pia Mhe. Caroline Sokoni, Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi ya Zambia, ambaye pia ni Rais wa International Ombudsman Institute (IOI), Kanda ya Afrika.

Mhe. Dk. Otiende Amollo, Mwenyekiti wa Tume ya Utawala wa Sheria wa Jamhuri ya Kenya, ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Taasisi za Ombudsman wa Afrika, Mhe. Dk. Mohamed Rukara, Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi ya Burundi, na Mhe. Ahmed Abuzaid Ahmed, Rais wa Tume ya Uchunguzi ya Jamhuri ya Kiislam ya Sudan. Wote hawa wamekuja kuadhimisha kumbukumbu hii ya miaka hamsini, kwa niaba ya wenzetu wa nchi takriban 45 za Afrika zilizoanzisha taasisi kama hii.

Mheshimiwa Waziri, Mhe. Mzee Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Viongozi mbalimbali, waheshimiwa wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Katika ratiba yetu mtaona kuna watoa mada na hotuba kadhaa, wakiwemo  Mheshimiwa Jaji Mstaafu Damiani Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye atatueleza uzoefu wake wa kufanya kazi ndani ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi. Amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, na pia Waziri wa Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na baadaye Jaji wa Mahakama ya Rufaani, na sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tulifurahi alipokubali kuzungumza siku ya leo, kwani mbali ya kumbukumbu zake ndani ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, Mhe. Lubuva ni picha halisi ya maadili mema katika utumishi wa Umma.

Tutapata pia salaam kutoka kwa Balozi Katarina Rangnitt wa Sweden, huko kwao ndiko taasisi ya Ombudsman ilikoanzia na ndiko alikoitoa Mwalimu Nyerere. Wageni wetu toka IOI na AOMA pia watatoa salaam zao. Mada zitatolewa na Jaji Mstaafu Gad John Kimweri Mjemmas, ambaye alifanya kazi kwenye Tume ya Kudumu ya Uchunguzi na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, na kutoka kwa Prof. Palamagamba Kabudi, na uchambuzi wa matarajio hapo siku za usoni kutoka kwa Mwalimu wetu, Msomi na Gwiji wa masuala ya Katiba nchini Prof. Issa Shivji.

Napenda pia nitamke kwamba tunao wawakilishi kadhaa wa familia za Wenyeviti, makamishna na Makatibu wa iliyokuwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi. Nitataja majina ya Wenyeviti wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kati ya mwaka 1966 na 2002.
1.    Chifu Erasto A.M. Mang’enya (1966 – 1970 na 1972 –  1973)
2.    Jaji Mark P.K. Kimicha (1970 – 1972)
3.    Col. Selemani J. Kitundu (1974 – 1978)
4.    Balozi Ackland L.S. Mhina (1978 – 1983)
5.    Nd. Antony R. Mbelwa (1984 – 1989)
6.    Nd. Abdalla M.R. Nungu (1989 – 1995)
7.    Nd. Ibrahim S.A. Kajembo (1995 – 1997)
8.    Prof. Joseph Mbwiliza (1998 – 2002).

Tunao Makatibu wawili na wafanyakazi wengi tu waliotumikia Tume ambao wapo hapa leo. Tunafurahi kuwa nao katika kuenzi mchango wa wazee wale waliofanikisha Tume ya Kudumu ya Uchunguzi kufanya kazi ya ki-historia na ya kujivunia. Nitambue uwepo wa Mhe. Mzee Fredrick Malika na Mzee Anastas Guvette ambao waliwahi kuwa Makatibu wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi.

Tunawaenzi na kuwapongeza wenyeviti, makamishna, na makatibu wote hawa. Kwa wale waliotuacha, tunapenda kutoa salaam zetu kupitia wawakilishi wa familia zao ambao tunao hapa. Wapo watumishi waliokuwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, bado wako kwenye utumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Tunawapongeza.

Sitapenda kusema mengi ila kuwakaribisha. Mambo mengi yataelezwa katika hotuba na mada zitakazotolewa hapo baadaye, yatalenga kauli mbiu ya maadhimisho haya yaani ‘Utawala wa Sheria ni Msingi mkuu wa Utawala Bora.’

Baadaye kidogo, nitamkaribisha Mhe. Joseph Butiku, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, aseme machache kwa niaba ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Shukurani
Kabla sijamkaribisha Mzee Butiku napenda nitoe shukurani zangu za dhati kwa wafuatao:
Napenda niwashukuru viongozi wote waliofika hapa. Namshukuru Mgeni Rasmi, Mhe. Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  ambaye anamwakilisha Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli, namshukuru Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Wawakilishi wa Familia ya Mwalimu Nyerere, asanteni sana.

Pia nawashukuru viongozi wastaafu, Mzee Joseph Sinde Warioba, Mzee Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye tutamsikia hivi karibuni. Tume inawashukuru wajumbe wa Bodi na uongozi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa ushirikiano wao wa hali na mali katika kufanikisha maadhimisho haya.

Napenda kutoa shukurani za dhati kwa uongozi wa Mfuko wa Pensheni wa watumishi wa Serikali, GEPF, kwa msaada wao wa hali na mali kwa kufanikisha shughuli hii.

Napenda nitoe pia shukurani zangu za dhati kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kutuwezesha kutumia Ukumbi na viwanja hivi vya Karimjee, ambavyo ni vya kihistoria kwa ajili ya maadhimisho haya. Asanteni sana.

Nawashukuru wageni wetu wote kuhudhuria maadhimisho haya. Nawashukuru watoa mada wote.

Nimalizie kwa kuwashukuru kwa kunisikiliza.

21 Oktoba 2016.

[1] Uk. 98, Address by President Julius Kambarage Nyerere, Opening of the New National Assembly, in Nyerere, Freedom and Socialism. pg 86. OUP 1968.
[2] Taz. Uk 3, Sehemu ya Kwanza, Tume na Kazi Yake, Ibara III, Uongozi kutka wa Rais; Taarifa ya Tume ya Rais juu ya kuanzishwa kwa Serikali ya Kidimokrasia ya Chama kimoja  cha siasa. Kimepigwa chapa na Mpiga Chapa wa Serikali Dar es Salaam, 22 Machi 1965.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.