Habari za Punde

Kilele cha Tamasha la Ngoma za Jadi kufanyika Tukuyu tarehe 7 na 8 ya mwezi huu

Tamasha kubwa la ngoma za jadi la Tulia litakalojumuisha zaidi ya vikundi vya ngoma 84 kutoka wilaya za Rungwe, Busokelo na Kyela linatarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 8 ya mwezi huu wa kumi katika viwanja vya Tandale wilayani Tukuyu.

Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza, litajumuisha zaidi ya ngoma za aina tisa huku baadhi ya ngoma zitakazoshiriki ni pamoja na Ipenenga, Ingo’ma na Maghosi.

Akizungumzia tamasha hilo, Naibu Spika wa Bunge na mwanzilishi wa tamasha hilo, Dkt. Tulia Ackson amesema lengo la tamasha hilo ni kukuza na kuendeleza tamaduni hasa za ngoma za asili.

‘Ngoma za asili zina sehemu kubwa katika utamaduni wetu, na ndio maana ni muhimu sana kama taifa tutakajikita katika kuhakikisha zinatambulika na pia zinaendelezwa’ alisema Dkt.Tulia.

Akielezea zaidi kuhusu ngoma hizo Dkt Tulia alisema lengo la tamasha la ngoma za jadi ni kuzifanya ngoma hizo zijulikane, na pia kuzipa umuhimu katika jamii na hivyo kuzifanya zisipotee.

‘Tamasha pia litatoa fursa ya kiuchumi kwa vijana watakaoshiriki tamasha hilo kwa wao kuanza kuzitazama ngoma kama chanzo cha kujipatia kipato’ alisema Dkt. Tulia.

Mashindano hayo yaliyoanza katika ngazi ya kijiji, kata, halmashauri na kanda, huku jumla ya vijiji 393 vikichuana kupata fursa ya kushiriki katika kilele cha matamasha hayo, yatahudhuriwa wageni mbalimbali kama mabalozi kutoka nchi mbalimbali pamoja na wakurugenzi na wawakilishi kutoka makampuni mbalimbali.

Mshindi wa kwanza wa mashindano hayo atarekodiwa albamu ya nyimbo zake kwenye DVD, pamoja na ufadhili wa kusomeshwa katika chuo cha Sanaa cha Bagamoyo.

Mshindi wa pili atapata mashine ya kusaga na watatu atapata zawadi ya bodaboda.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.