Na Salmin Juma, Pemba
Mkuu wa Wilaya ya Chake –chake, Salama Mbarouk Khatib amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vikundi vya wajasiriamali kwa lengo la kuwainua kiuchumi wajasiriamali hao .
Amesema serikali imeandaa sera na mikakati ya kuwapatia mikopo isiyo na riba katika kuwarahisishia kuboresha bidhaa zao na kupata nafasi nzuri ya kukopa na kurudisha kwa wakati .
Ameyasema hayo huko Ukumbi wa uwanja wa Gombani alipokuwa akifunga mafunzo ya siku moja ya taaluma ya matumizi bora ya mikopo kwa wajasiriamali waliokwishajaza fomu za mikopo ya bishara zao.
Akitoa maelezo ya kufanyika kwa mafunzo hayo kaimu Mratibu wa Idara ya Mikopo , wizara ya wanawake na watoto Pemba Haji Khamis Haji amesema lengo ni kuwajengea uwezo katika kuitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka kupata hasara katika shughuli zao.
Naye afisa mikopo kutoka Idara ya mikopo wizara ya wanawake na watoto Shuwena Hamad Ali amesema ili wajasiriamali waweze kufanikiwa kibiashara lazima wayajuwe malengo makuu ya masoko ilikiwemo kuwatambua wateja wao na mahitaji ya soko katika kupata faida
Nao baadhi ya wajasiriamali hao wameitaka serikali kutafuta wafadhili wengine watakaosaidia kupatikana kwa fedha zaidi zitakazoweza kupewa wahitaji wengine wa mikopo na kuondoa usumbufu wa kusubiri wengine warudishe na wengine wapewe .
Jumla ya shilingi milioni 76.6 zinatarajiwa kutolewa mkopo kwa vikundi 48 vya wajasiri amali waliojaza fomu na kufanyiwa uhakiki wa kupatiwa mikopo hiyo.
No comments:
Post a Comment