Habari za Punde

Serikali kuhakikisha fedha zilizoahidiwa kwenye bajeti zinapatikana


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                    27.10.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezihakikishia Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika upatikanaji wa fedha kwenye vifungu vya matumizi ya Bajeti za Wizara hizo ili zifanye kazi kwa ufanisi zaidi.

Dk. Shein aliyasema ha yo leo Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati yake na uongozi wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ilipowasilisha Taarifa yake ya  Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa hatua kubwa imefikiwa katika upatikanaji wa fedha kwa kila Wizara katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na mikakati maalum iliyowekwa ambayo hatimae imeleta mafanikio makubwa.

Dk. Shein alisema kuwa juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuondoa matumizi yasio ya lazima yakiwemo maposho, safari na mambo mengineyo zimesaidia kwa kiasi kikubwa na ndio maana lengo litafikiwa la kuwaongezea hata mishahara wafanyakazi wa sekta ya umma.

Aidha, Dk. Shein  alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wote wa Wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi wao.

Mapema Kaimu Waziri wa Wizara hiyo,  Issa Haji Ussi Gavu akisoma  taarifa ya Mapango Kazi huo alisema kuwa jukumu la msingi la Ofisi hiyo ni kusimamia masuala yanayohusu utawala wa sheria na utumishi wa umma pamoja na kuimarisha upatikanaji bwa haki.

Aidha, Waziri Gavu alisema kuwa Ofisi ina jukumu la kusimamia na kuratibu utekelezaji wa misingi ya utawala bora katika taasisi za umma.

Kaimu Waziri huyo, alisoma malengo ya Wizara hiyo, pamoja na madhumuni ya taarifa, utekelezaji kifedha ambapo miongoni mwa malengo ya Wizara hiyo ni kusimamia utoaji na upatikanaji wa haki, kukagua hesabu za serikali, kuwajengea uwezo watumishi wa umma, kusimamia mali za Wakfu, kukusanya Zaka, Sadaka na Misaada ya kheri na kuigawa kwa wanaostahiki pamoja na malengo mengineyo.

Mapema Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee nae alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa uwasilishaji mzuri wa Mpango Kazi wake.

Katika maelezo yake Dk. Mzee alisema kuwa licha ya ukubwa wa Wizara hiyo lakini imeuweka vizuri mpangilio na uwasilishwaji wa kazi hiyo huku akitoa wito kwa Wizara hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi kwa kutambua kuwa Wizara hiyo ni kioo kwa Wizara nyengine za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nao uongozi wa Wizara hiyo, ulitoa pongezi za pekee kwa Dk. Shein kwa kupatiwa fedha za kutosha katika vifungu vya matumizi kwenye Bajeti yao pamoja na Bajeti za Wizara zote za Serikali hatua ambayo imezidi kuwapa ari katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.

Uongozi huo ulimuhakikishia Dk. Shein kuwa haotomuangusha na umeahidi kutekeleza vyema majukumu yao na kusisitiza kuwa utaendelea kuchapa kazi ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Asha Ali Abdulla alitumia fursa hiyo kusoma taarifa ya utekelezaji wa mpango Kazi kwa robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba mwaka 2016  pamoja na muhtasari wa upatikanaji wa fedha  kwa kipindi hicho kwa Taasisi zote za Wizara hiyo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.