Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya Mbweni Dr. Haji Mwita Haji alipomuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein katika mahafali ya Pili ya Chuo cha Madaktari Zanzibar na yale ya 23 ya Chuo cha Taaluma za Sayanzi za Afya Mbweni.
Balozi Seif akisalimiana na wahadhiri walioendesha mafunzo ya Udaktari Zanzibar kutoka Chuo Kikuu cha Matanzas cha Nchini Jamuhuri ya Watu wa Cuba Tawi la Zanzibar hapo katika viwanja vya chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya wahitimu waliomaliza mafunzo ya Udaktari chuo cha Udaktari Zanzibar wakila kiapo cha utii katika kukabiliana na majukumu yao watakayopangiwa hapo baadaye.
Baadhi ya wahitimu waliomaliza mafunzo ya Udaktari chuo cha Udaktari Zanzibar wakila kiapo cha utii katika kukabiliana na majukumu yao watakayopangiwa hapo baadaye.
Mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Matanzas cha Nchini Jamuhuri ya Watu wa Cuba Dr. Zailit Gonzalet Cruiz akimuhudhurisha Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Udaktari katika chuo cha Udaktari Zanzibar.
Baadhi ya wahitimu wa fani ya Uuguzi wakila kiapo cha uaminifu mara baada ya kumaliza mafunzo yao hapo katika Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya Mbweni.
Balozi Seif akiwazawadia wanafunzi bora wa fani mbali mbali waliomaliza mafunzo yao ya Udaktari pamoja na Fani nyngine za Afya hapo Mbweni.
Balozi Seif akiwazawadia wanafunzi bora wa fani mbali mbali waliomaliza mafunzo yao ya Udaktari pamoja na Fani nyngine za Afya hapo Mbweni.
Balozi Seif akiwazawadia wanafunzi bora wa fani mbali mbali waliomaliza mafunzo yao ya Udaktari pamoja na Fani nyngine za Afya hapo Mbweni.
(Picha na – OMPR – ZNZ.)
Na Othman Khamis OMPR.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema dhamira ya Serikali Kuu ni kuona kwamba Wananchi wa Zanzibar wanakuwa na afya njema, wenye furaha, wakiishi kwa amani huku wakiwa na elimu, ujuzi na maarifa yanayohitajika katika kukabiliana na changamoto na mabadiliko ya karne hii ya 21.
Alisema licha ya kwamba Taifa hukumbwa na changamoto kadhaai za Kiuchumi ambazo baadhi ya wakati huzorotesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo lakini Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya sambamba na elimu kwa wananchi wake.
Akiyafunga Mahafali ya Pili ya Chuo cha Madaktari cha Zanzibar na ya 23 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Mbweni ikiwa ni ya mwisho kabla ya vyuo hivyo kuunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA }, Dr. Ali Mohammed Shein ambae Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali inafanya hivyo ikitambua wazi kwamba, maendeleo ya kweli ya Taifa hili yataletwa na nguvu kazi zenye afya bora na Elimu.
Dr. Shein alisema Serikali imekuwa ikiwekeza kiwango kikubwa cha fedha katika azma yake ya kuimarisha sekta ya Afya na Elimu akitolea mfano miundombinu inayoendelea kuwekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na ujenziwa Majengo Mapya ya Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Kisiwani Pemba ili kutoa huduma bora zinazokubalika katika kiwango cha Kimataifa.
Alisema muundo mpya wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar utahusisha Taasisi ya Uongozi wa Fedha Chwaka itakayokuwa Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu, Taasisi ya Maendeleo ya Utalii ya chuo Kikuu pamoja na Skuli ya Tiba na Sayansi za Afya ya chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.
Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba lengo la kuviunganisha vyuo hivyo ni kuweka utaratibu wa kisheria utakaoiwezesha Zanzibar kuwa na chuo Kikuu kimoja cha Serikali kitakachokuwa imara na chenye ubora na ufanisi katika matumizi ya rasilmali za Nchi.
“ Mswada wa kuviunganisha vyuo hivyo na chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar tayhari umeshapitishwa Tarehe 28 Septemba 2016 na tayari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametia saini na kuwa sheria kamili ”. Alisema Dr. Shein.
Rais Shein alisisitiza kwamba Wanafunzi wa Zanzibar kupitia Chuo hicho Kikuu cha Taifa { SUZA } wanapata mafunzo bora yatakayowawezesha kuwa na sifa zitakazokubalika katika nyanja ya taaluma na soko la ajira popote watakapoamua kufanya kazi iwe kitaifa au Kimataifa.
Dr. Shein aliwahimiza watendaji wote wa Serikali kuzitumia fursa mbali mbali za mafunzo zilizotayarishwa na Serikali kwa mashirikiana na Mataifa washirika na kuendeleza utafiti kwa ajili ya maendeleo ya Taifa ili zilete tija.
Akizungumzia malalamiko yanayotolewa na Wananchi kupitia vyombo vya Habari juu ya tabia iliyojengeka kwa baadhi ya wataalamu wa afya kukataa kufanya kazi Kisiwani Pemba na Vijijini Rais wa Zanzibar alikemea kwamba tabia hiyo ni mbaya, haivumiliki na ni hatari sana kwa afya za Wananchi.
Alisema vitendo hivyo vinavyosababisha watendaji hao kuchelewa kutoa huduma katika maeneo ya kazi wakati mwengine kutoonekana kabisa kwenye vituo walivyopangiwa vinakiuka mikataba waliyoiridhia inayoelezea watafanya kazi mahali popote Unguja na Pemba.
Dr. Shein aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar kuwachukulia hatua kali za kinidhamu Madaktari watendaji wote wa Afya kwa daharau na ukiukaji mkubwa wa mikataba ya kazi kwa vile wamekiuka misingi muhimu ya kazi zao na kuondosha mapenzi na uadilifu kwa wananchi wanaowahudumia.
Rais wa Zanzibar alionya kuwa watendaji hao wa Sekta ya Afya lazima wawe tayari kwenda kutoa huduma mahali popote watakapopangiwa na Serikali kwa kuzingatia sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma pamoja na vipengele vyote vya mikataba ya kazi.
Aliwataka daima kukumbuka kwamba tabia njema, huruma na mapenzi ni vazi la lazima la daktari na muuguzi yoyote Duniani. Hivyo vazi hilo wajivishe hata wanapokuwa majumbani kwa kuwa tayari kuwasaidia wananchi hata kama nje ya kazi pale panaohitajika kutoa msaada huo au kuokoa maisha ya watu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwapongeza wahitimu wote waliomaliza masomo yao pamoja na uongozi wa vyuo vyote viwili kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa makubwa yaliyopeklekea kupatikana mafanikio yanayoonekana.
Dr. Shein alitoa shukrani maalum kwa waalimu kutoka Jamuhuri ya Cuba na Serikali yao waliosaidia kutoa taaluma kwa Madaktari wazalendo sambamba na shukrani kwa Serikali ya Oman kwa kuendelea kuunga mkono katgika utyoaji wa elimu ya Tiba hapa Zanzibar.
Akisoma Risala kwa Niaba ya wahitimu wa chuo cha Udaktari na Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya Zanzibar Muhitimu wa fani ya Udaktari Said Mzee alisema mafunzo waliyoyapata yameweza kuokoa Watoto wa Kinyonge kupata Elimu ya Juu hapa Nchini.
Muhitimu Said kwa niaba ya wanataaluma wenzao wa sekta ya afya wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha mpango wa mafunzo ya Udaktari Nchini kitendo ambacho kitasaidia kupunguza uhaba wa wataaklamu wa sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Madaktari cha Matanzas cha Nchini Jamuhuri ya Watu wa Cuba imefanikisha mango maalum wa kusomesha Madaktari wazalendo hapa Nchini.
Dr. Malik alisema mpango huo uliosimamiwa na wataalamu wa sekta ya afya kutoka Cuba tayari umeshazalisha madaktari wazalendo 50 watakaoweza kutoa huduma katika hositali mbali mbali za Unguja na Pemba.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na hadha hiyo ya Mahafali ya Pili ya Chuo cha Madaktari Zanzibar na yale ya 23 ya chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya Zanzibar Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo aliwanasihi wahitimu wote kukubali kuwa sehemu ya mabadiliko ya tabia njema katika maeneo yao ya kutoa huduma za afya.
Mh. Mahmoud alisema yapo malalamiko kutoka kwa wananchi yanayoshutumu baadhi ya watendaji wa afya kukosa lugha nzuri wakati wanapohitaji huduma. Hivyo wahitimu hao wanapaswa kufahamu kwamba lugha njema ni tabia ambayo watalazimika kuivaa na kuiendeleza katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wote wa maisha yao ya utumishi.
Mahfali ya Pili ya Fani ya Udaktari yametoa wahitimu 12 wa Shahada ya Udaktari wakati wahitimu wapatao 515 wa fani za wasaidizi Madaktari, Wauguzi, Maafisa wa Afya, Mafundi sanifu wa Maabara wametoka Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya Zanzibar kiliopo Mbweni.
No comments:
Post a Comment