Habari za Punde

ZIFA Yaandaa Ziara ya Mafunzo kwa Wakulima Mwani wa Chwaka

Chuo cha Uongozi wa fedha Zanzibar (ZIFA) kiliandaa ziara ya siku moja ya mafunzo kwa wakulima wa mwani wa Chwaka kutembelea kikikundi cha Ushirika cha Tusife Moyo cha Kijiji cha Kidoti ambacho kimepiga hatua kubwa katika kusanifu zao hilo kwa ajili ya matumizi mbali mbali.
Ziara hiyo  ni moja ya juhudi zinazochukuliwa na chuo katika azma  yake ya  kusaidia jamii kufikia maendeleo  endelevu ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Mhadhiri wa ZIFA Maalim Said  Mohd Khamis alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar mwaka jana, ulionyesha kuwa zao la mwani ambalo linawashirikisha asilimia 80 wananchi wanaoishi pembezoni mwa bahari, wengi wao wakiwa wananwake bado halijamsaidia  mkulima ipasavyo.
Alisema kutokana na kasoro hiyo  chuo kimeamua kutoa msukumo maalumu wa kutoa mafunzo ya vitendo  kwa wakulima wa mwani ili wawe na uwelewa wa kulisarifu zao hilo kwa matumizi mengine  badala ya kuwauzia wafanyabiashara  kwa  bei wanayopenda wao.
Maalim Said alisema wakulima wa mwani wanatumia muda na rasilimali nyingi katika  kushughulikia kilimo hicho huku tija wanayopata ni ndogo  na haikidhi nguvu wanazotumia.
Aliswashauri wakulima wa  mwani wa Chwaka kujikusanya  na kuanzisha vikundi vya ushirikia ili waweze kupatiwa mikopo na misaada ya kununulia mashine za kusarifu mwani kwa matumizi mengine kama wanavyofanya wakulima wenzao wa kijiji cha Kidoti badala ya kuuza bidhaa hiyo kwa bei ndogo.
Kikundi cha Tusife moyo cha Kidoti kinamiliki mashine ya kutengenezea sabuni na mashine ya kusagia mwani mkavu kwa matumizi mbali mbali ambapo kilo moja ya mwani uliosagwa inauzwa shilingi 10,000 na kabla ya kusaga wanauza  shilingi 300
Katibu wa kikundi cha Tusife moyo cha Kidoti Hawa Simai Khamis aliwaeleza wakulima wa mwani wa kijiji cha Chwaka kwamba mafanikio waliopata yanatokana na kujikusanya pamoja na kutafuta wafadhili wa ndani na nje ya nchi
Amesema wanauweza wa kuzalisha aina tofauti za sabuni na wamepata soko katika baadhi ya mahoteli  ya kitalii yaliopo ukanda wa  Nungwi, Matemwe na Pwani Mchangani.
Katibu huyo aliongeza kuwa mwani kwa sasa ni chakula na unatumika katika vyakula vingi ikiwemo mchuzi, keki , juisi, kachumbari  na pia unatumika kutibu maradhi mengi ikiwemo maradhi ya ngozi.
Wakulima wa mwani kutoka Chwaka walifundishwa kutengeneza sabuni na kupika mchuzi  wa kukaanga kwa kutumia zao hilo  na kujifunza matumizi mengine .
Wakulima wa Chwaka walikishukuru Chuo cha uongozi wa Fedha Zanzibar kwa kuwaandalia ziara hiyo na wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyopata ili kuwa mkombozi wao kupitia zao la mwani.
Aidha walikishauri Chuo hicho kuendelea kuwapatia mafunzo zaidi  na kuwasimamia na kuwaongoza katika kuanzisha ushirika wa mwani wa Chwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.