Habari za Punde

Kuelekea Novemba 14 Wizara ya Afya Zanzibar Yaandaa Michuano ya Mpira wa Miguu Kuadhimisha Siku ya Kisukari Duniani

Na Ramadhani Ali/Maelezo.
Waandaaji wa michuano ya maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani kwa Zanzibar Timu ya Wizara ya Afya imeyaaga mashindano hayo katika mchezo  wa ufunguzi baada ya kufungwa na timu ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na watoto kwa mikwajuni ya penelti katika kiwanja cha Amani nje.

Michezo hiyo inayoshirikisha Timu  nane za Wizara za Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar  inachezwa kwa mtindo wa mtoano na fainali itachezwa tarehe 13 mwezi huu, siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo yanayofanyika kili ifikapo 14 Novemba, ya kila mwaka.

Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa zimefungana bao 1-1 mabao yote yakipatikana kipindi cha kwanza . Wizara ya Kazi ilipata bao lake dakika ya 26 kupitia kwa mchezaji wao Ali Seif na  Wizara ya Afya ilisawazisha kwa njia ya penelti iliychongwa na Ahmed Rashid dakika ya 35.

Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi ya kila upande lakini hakuna timu iliyoweza kuona nyavu za mwenzake huku wachazaji wa timu zote mbili wakikabiliwa na wakati mgumu wa kuanguka mara kwa mara kutokana na utelezi ulisababshwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa muda mrefu kabla ya  pambano hilo.

Muda wa penelti tano ulipowadia kila timu ilipoteza mbili na hatua ya kupigiana penelti moja moja ikaendelea na ndipo wenyeji wakajikuta wanapoteza penelti yao muhimu na kuipa michuano hiyo mkono wa kwaheri kwa masikitiko.

Akizindua michuano hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili alisema lengo la maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ni kuunga mkono jitihada za Kimataifa katika kupambana na maradhi hayo yanayoongezeka  kwa kasi duniani kote.

Alisema asilimia 3.7 ya Wazanzibari wanaugua maradhi ya kisukari na wengine wengi wako katika hatari ya kupata maradhi hayo iwapo hawatafanya juhudi za kujikinga.

Hata hivyo alisema tiba kubwa ya maradhi ya kisukari ni  watu kuweka utaratibu wa  kufanya mazoezi na kuweka utaratibu mzuri wa vyakula kwani ndiyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maradhi hayo.

Katibu Mkuu aliwashauri wafanyakazi wa Mawizara maidara taasisi za Serikali na binafsi na jamii kwa jumla kuhamasisha katika kufanya mzaoezi na kutenga wakati wa mapumziko ili kuweka mzunguruko mzuri wa damu na kupunguza uzito.

Timu zinazoshiriki michuano hiyo ni Wizara ya Afya, Wizara ya Kazi, Wizara ya Habari, Utalii Utamaduni na Michezo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko, Wizara ya Kilimo Maliasili Uvuvi na Mifugo na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. 

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.