MKE wa Rais wa Zanzibar
Mama Mwanamwema Shein amewataka viongozi na wananchi wa Mkoa wa Kusini
Unguja kuitumia vyema ardhi ndogo
iliyopo kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji na Vijiji, sambamba na kujiepusha
na migogoro ya ardhi ambayo husababisha uhasama na kuhatarisha amani.
Mama Shein aliyasema hayo
leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na akinamama, viongozi na wanachama
wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa Wilaya ya Kusini na Wilaya ya Kati
Unguja katika ziara yake yenye lengo la kuwasalimia na kuwashukuru kwa
kuendelea kuiunga mkono CCM, na kupelekea kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi
uliopita.
Akiwa katika ukumbi wa
Hoteli ya Karafuu, Michamvi Mkoa wa Kusini Unguja, Mama Shein alitoa nasaha
zake kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na wananchi wa Mkoa huo kushirikiana
katika kuihami misitu na miti ya asili ambayo ni muhimu katika kuyahifazi mazingira
ambayo ni hazina kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Mama Shein, ambaye katika
ziara yake hiyo amefuatana na viongozi mbali mbali wakiwemo Wabunge na
Wawakilishi wa Viti Maalum pamoja na wake wa viongozi wakiwemo Wabunge na
Wawakilishi, alitumia fursa hiyo kusisitiza suala zima la amani na kueleza kuwa
bila ya amani hakuna watakaokwenda kondeni, watakaojishughulisha na kilimo cha
mwani, uvuvi wala utalii na kueleza kuwa watakaoathirika zaidi ni akinamama na
watoto.
Hivyo, aliwataka
viongozi na wananchi wa Mkoa huo wasichoke kuwakumbusha vijana wao umuhimu wa
kuitunza amani na kujiepusha na vitendo vyote vya uvunjaji wa sheria na
kuhatarisha amani kwani kuvunja amani ni mara moja lakini kuirudisha huchukua
muda.
Mapema Mama Asha
Balozi, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza akinamama hao wa
Jumuiya hiyo kuwachagua viongozi wenye uchungu na chama, nchi na wanachama wenzao
katika uchaguzi wa Chama na Jumuiya zake hapo mwakani.
Mama Asha alitumia
fursa hiyo kuwataka akinamama wenzake kuwa karibu na watoto wao ili kuepuka
vitendo viovu wanavyoweza kufanyiwa hasa vitendo vya ubakaji.
Nae Mama Fatma Karume
aliwahamisisha wanawake kuchukua fomu za kugombania nafasi mbali mbali za
uongozi ndani ya chama cha CCM bila ya kuogopa pingamizi za kutowapa nafasi
waliokuwa hawakusoma na kueleza kuwa wengi wao waliofanya Mapinduzi na kuipa
uhuru Zanzibar walikuwa hawana elimu hivyo hicho sio kisingizio.
Alieleza kusikitishwa
na vijana ambao hupewa madaraka makubwa ndani ya serikali na kusahau wajibu na
majukumu yao na badala yake kufanya hilba kwa lengo la kujineemesha wao wenyewe
na pale wanapoondoka madarakani hukimbilia katika vyama vya upinzani.
Aliwaomba wale wote
walioteuliwa na Dk. Shein kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi kutomuangusha
hasa wanawake ambao katika uongozi wake amewapa nafasi nyingi serikalini.
Katika risala yao
wanachama wa Jumuiya ya UWT Wilaya ya Kusini Unguja , walitoa shukurani kwa Serikali
kwa kuwapelekea mradi wa JOCDO kwa madhumuni ya kusaidia vikundi mbali mbali
ili wajikwamue na hali ngumu ya maisha ambapo pia, UWT Wilaya imeanzisha
vikundi vya Jumuiya katika Matawi kwa lengo hilo la kujikwamua kimaisha.
Aidha, walieleza kutokuwa
nyuma katika kukiimarisha chama na kuleta maendeleo endelevu na kueleza juhudi walizozichukua
katika kuhakikisha CCM inapata ushindi na kumuahidi Mama Shein kuwa katika Wilaya
yao upinzani hautokuwa na nafasi milele.
Walieleza kusikitishwa
na suala zima la unyanyasaji wanawake na watoto huku wakitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kutekeleza
Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Wakati huo huo, akiwa katika ukumbi
wa Kituo cha Elimu kiliopo Dunga, Wilaya
ya Kati Unguja, Mama Shein aliwahimiza akinamama na vijana umuhimu wa kuanzisha
na kuviendeleza vikundi vya maendeleo ili kujiimarisha kiuchumi.
Mama Shein aliwaahidi
akinamama hao kuwa wake wa viongozi pamoja na waheshimiwa wabunge na
wawakilisgi wataendelea kushirikiana na vikundi vya akinamama na vijana katika
jitihada zao za kujiletea maendeleo.
Aidha, Mama Shein
aliwataka wanajumuiya ya UWT kujitahidi kuzitumia vyema fursa ambazo Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba inazitoa kwao kwa lengo la kuwawezesha
kiuchumi.
Nao wanajumuiya ya UWT
Wilaya ya Kati waliahidi kuendelea kumuunga mkono Mama Shein katika juhudi zake
hizo sambamba na kuendelea kukiunga mkono chama cha Mapinduzi ili kiendelee
kushika hatamu.
No comments:
Post a Comment