Habari za Punde

Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 -Yatandaza barabara za lami hadi vijijini


 -Ngomeni, Mgelema nako dk Shein atoa maagizo zijengewe 

Na Haji Nassor, Pemba

LEO wanzibari wote, tuko katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 53, ya Mapinduzi Zanzibar, ambayo yalitukomboa.

Kila mmoja ni shahidi aidha kwa kuona au kuosma kwenye vitabu, kuwa hatukuwa na thamani kabla ya mwaka 1964.

Unyonge, unyonyaji, adhabu ndio iliokuwa imetawala kwa wazalendo kupitia watawala wa enzi hizo, kabla ya jemedari wetu wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume kutukomboa.

“Leo wana wa nchi tuko katika uhuru, na tumeshajitawala sasa kila mmoja, ataishi kw afuraha na faraja, maana wale wadhalimu tumeshawaondoa’’,alisema moja kati ya hutuba zake.
Kabla ya ujio huu wa uhuru miaka 53 iliopita, hakuna alieamini kwa wananchi wanaoishi vijijini, kwamba iko siku hata gari ndogo itafika wanakoishi.

Kauli hii kama ya mzaha hivi, lakini ni ukweli usiofichika baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupokea ahadi ya ujenzi wa barabara zao hawakuamini.

Mimi, wewe na yule sasa unapotembelea barabara hizi sita za mkoa wa kusini Pemba, mbona ni bora hata hapo katikati ya mji wa Pemba Chake Chake

Hujafika wewe….. pamejaa mashimo, misingi inayotishia ajali, lakini tutafanyaje ndio mji wetu.

Sasa leo hii tukiwa tunaelekea kushereheke kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa wananchi wanaoishi vijiji hivyo ikiwa ni pamoja na Kangani, Kengeja, Pujini na Wambaa, Tundauwa wako burudani.

Huwezi amini kwamba tokea tulipojinasua na makucha ya wakoloni mwaka 1964, barabara hizi takriban sita zilikuwa katika mashaka na tabu kubwa ya usafiri, lakini miaka hii 53 sasa tunasema hongera Mapinduzi.

Ni ukweli usiofichika kwamba, vijiji kadhaa vya Kisiwani Pemba vilikua vimeasahauliwa juu ya kufikishiwa huduma ya mawasiliano ya barabara .

Hakuna asieju kuwa lengo hasa la baba wa taifa hili la Zanzibar jemedari Abeid Aman Karume, ni kuhakikisha kila mmoja anafaidi matunda ya Mapinduzi.

‘’Leo wananchi wa Zanzibar, muko huru na sasa ni wakati wetu kujitawala, na udhalimu na udhalilishaji sasa basi, mmesikiaaa…. ndiooooo……..’’, ni miongoni mwa kauli zake.

 Wakati huu tukiwa kwenye wiki ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, sasa wananchi hawa, wametulia tuli na wanaendelea kuimarisha uchumi wao kama ilivyokua azma na lengo Mapinduzi.

Miaka hii 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, iko tofauti na miaka 48 iliopita, maana hatua hii ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizi sita, tena kwa kiwnago cha lami, kumeondoa utabaka baina ya mjini na vijijini.

‘’Barabara ndio hazina…….. barabara ndio uti wa mgongo wa taifa lolote lile…………barabara ndio kiunganishi’’, ni kauli ya rais wa awamu hii ya saba dk Ali Mohamed Shein, alioitoa wakati wa ufunguzi wa barabara hizo.

Wakati huu tukiadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanziabr, ni kweli jemedari wetu mzee Abeid Amani Karume, hatunae tena, lakini fikra, mawazo na busara zake ndio hayo yanayotumiwa na viongozi waliopo madarakani kipindi hiki.

Ili kuthibitisha haya….. tembelea vijiji hivyo uone barabara za kiwnago cha lami, zilivyotandazwa na wananchi kupata faraja ya kuendeleza kazi zao za kujiletea maendeleo.

Kwa vile ahadi ni deni, ndio maana Serikali yetu iliopo madarakani kwa kuunganisha na nguvu za wananchi, ikaanza kuzinduka kwa mwendo wa haraka, ujenzi wa barabara za vijijini Mkoa wa Kusini Pemba.

Hili kwa wale waliofika Pemba kwenye miaka hii miwili ya karibuni wanaweza kuwa mashahidi, maana kwa sasa ni takriban asilimia 90 ya vijiji vya Pemba, sasa vinabarababara za uhakika na za kudumu, zinazoteleza kama mgongo wa ngisi.

Hili kwa haraka sana, si rahisi kuliamini hasa kwa wenzetu walioko nje ya Kisiwa cha Pemba, hasa kutokana na kutolewa ahadi zisizotekelezwa na za muda mrefu juu ya ujenzi wa barabara za ndani.

Kama ukweli ni sumu, basi kila anaesoma makala haya unaweza kumdhuru, maana leo hii tukiadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, barabara kadhaa za vijijini kuna mtelezo wa hali juu kutokana na barabara kung’ara.

Serikali hii ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliovuliwa kutoka makuchani mwa wakoloni, kwa kushirikiana na washirika wake wa maendeleo, ambao ni Serikali ya Norway, imejenga barabara sita.

Hizi zilijengwa kwa pamoja na hata baadhi ya wanasiasa kushindwa kuamini, kama Serikali hii ingeweza, kama ilivyoahidi kwa wananchi.

Kwa hakika keki ya taifa hili la Zanzibar, sasa imeanza kuliwa, na kila miaka ikisonga, ndio kila mmoja anapata kwa mujibu wa tumbo lake, hapa nazungumzia maendeleo.

“Faida ya Mapinduzi ya mwaka 1964, sasa hakuna asieiona, maana leo hii tukizifungua barabara hizi kila mmoja atazitumia bila ya kujali chama, dini, rangi, wala mtu eneo analotoka’’, alisema dk Shein eneo la Kengeja kwenye ufunguzi wa barabara hizi.

Ujenzi wa barabara zote hizo, naamini ni zile ambazo wakaazi wake walikuwa wameshakata tamaa, kwamba hazitojengwa tena maana walikuwa wameshaahidiwa kwa muda mrefu bila ya mafanikio.

Miongoni mwa barabara zilizoingia kwenye mkumbo wa huo wa ujenzi ni pamoja na barabara ya Mtambile –Kangani yenye urefu wa kilomita 6.2 ambayo kwa sasa haina shaka tena juu ya usafiri wake.

Said Omar Juma (50), yeye ni mkaazi wa kijiji hicho, wakati akizungumza na ukurasa huu, alikua haamini hadi walipoona vitendea kazi vya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano vikiaza kukata milima na miti.

“Umri wangu sio mdogo hapa Kangani, na nikikumbuka ahadi zilizokua zikitolewa na viongozi hata wa majimbo, si kuamini sana wakati nilipoona magari ya Mawasiliano yakianza pilika pilika za ujenzi nilidhani tu kuondoa njiani’’,alieleza.

Kama hayo ni wananchi wa Kangani na barabara yao,  ndani ya miaka hii 53 ya mapinduzi, furaha nyengine iko kwa wananchi wa Mtambile – Kengeja - Mwambe yenye urefu wa kilomita 9, ambao nao hasa walikua ndio wa mwanzo kukata tamaa.

Maana wenyewe walitarajia kuwa barabara yao iwe imeshajengwa tokea utawala wa rais wa mwanzo wa Zanzibar, hayati Abeid Aman Karume, kutokana na mji wao kuwa makao makuu wa Wilaya ya Mkoani enzi hizo.

Ismaili Haji Mcha (49), alisema tokea akiwa mdogo, akisikia taarifa za kujengwa barabara yao kwa kiwango cha lami, lakini lililokuwa likijitokeza ni kutengenezwa kwa kiwango cha kifusi pekee.

“Naamini kwa watu wenye umri kama wangu, hakuna hata mmoja aliekua akiamini kwamba barabara yetu wakati tukiadhimisha miaka 53 hapa Zanzibar itakua imeshajengwa kwa kiwango cha lami’’,alieleza.

Usafiri wakati kabla ya kuadhimisha miaka 53, kwa vijiji vyote hivyo, kulikua na gari moja inayoondoka kijijini huko mjini mapema asubuhi na kurudi mchana.

Leo hii tukielekea miaka hii 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakati suala la miundombinu ya usafiri ukiwa umeimarika, ndio chachu ya maendeleo, ikiwa ndio azma ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

 Wananchi wa shehia za Wambaa na Chumbageni Wilaya ya Mkoani, nao wamepitiwa na mwangaza wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwa kujengewa barabara yao tena kwa kiwango cha lami.

‘Sisi ilikuwa mgonjwa atiwe kwenye gunia hadi barabara kuu kwa kupelekwa hospitali kutokana na barabara yetu kuwa mbovu na yenye mashimo makubwa’’,alisema Amin Haji Makame.

Alisema kua miaka ya 2000 akiwa kwenye kamati ya maendelo ya Shehia ya Wambaa alifika mahala wakavunja kamati kutokana na kushindwa kuamini waliokua wakiaambiwa juu ya ujenzi wa babarabara yao.

“Tulifika mahala siku moja kuivunja kwa muda mrefu kamati yetu, maana walikua wakija viongozi wanatueleza juu ya ujenzi wa barabara yetu nasi tunawapowaleza wananchi wanashindwa kutuamini’’,aliongeza Amini Haji.

Akizungumza bila wasiwasi alisema sasa tukiwa katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar hata gari ndogo aina ya ‘MarkII’’inafika Wambaa bila ya tabu.

Haya yote unapoyaangalia ndio sasa unaona kwamba Kisiwa cha Pemba hasa Mkoa wa Kusini, kuna utekelezaji mkubwa wa ahadi za ujenzi wabarabara za vijijini na ile azma ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa upande wa huduma ya barabara.

Barabara hii ya Mizingani –Wambaa ambayo ina urefu wa kilomita zaidi ya 9, na kwa sasa imekamilika kwa kiwango cha lami na kuruhusu kutumika wakati wowote.

Kama ilivyo barabara nyengine, nayo hii imewapunguzia joto na usumbufu wananchi na wanfanyabiashara wa vijiji hivyo, kutokana na kupata fursa ya kusafirisha mazo na wao wenyewe kwa utulivu.

Matunda ya Mapinduzi ya Zanzibara ya mwaka 1964 pia yakabisha hodi kwenye barabara ya Kenya- Chambani ikiwa ni miongoni mwa barabara zipazo sita Mkoa wa Kusini Pemba ambazo imeingia kwenye mkumbo wa ujenzi wa kiwango cha lami.

Eneo la Chambani hapo awali lilikua likitajwa sana kama ni sehemu mojawapo ambayo hata barabara yake kwa kipindi cha jua, ilikua na usumbufu mkubwa kupitika.

Idrisa Juma Khamis (49), alisema kwa mara ya kwanza aliposikia kuhusu ujenzi wa barabra hiyo alijua hiyo ni sehemu ya kampeni.

‘’Unajua tokea zamani nilikuwa nasikia kwamba barabara yetu inataka kujengwa lakini sikuamini, ili sasa mambo ‘bomba’ inapitika vizuri’’,alisema akiwa juu ya baiskeli yake.

‘’Sisi ilikua ikifika hekaheka za kampeni basi utasikia tu viongozi hata wa majimbo ‘mkitupa kura tutahakikisha barabara yenu hii inajwengwa kwa kiwango cha lami’, na baada ya muda inafukiwa mashimo tu’’, alifafanua.

Barabara ya Chanjamjawiri – Tundaua kwa sasa nako kuna mtelezo wa haja na mg’aro wa lami, na kuwafanya wananchi wa vijiji vya Misooni, Kungeeni, Tundaua, Kilindi kufaidika na barabara hiyo.

Juzi rais wa awamu hii ya saba ndani ya miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar, dk Ali Mohamed Shein, ameshatoa agizo kwa wizara husika ya ujenzi wa barabara, kwamba barabara za Ngomeni na Mgelema nazo zijengwe.

“Hadi ikifika mwakani tukiadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar, wananchi wanaotumia barabara hizi nao wafaidike na matunda kwa kujengewa haraka abarabara kwa kiwnago cha lami’’,alifafanua.

Dk Shein ametoa agizo hilo hivi karibuni, wakati alipozitembelea barabara hizo, kwenye ziara yake ya siku nne kisiwani, Pemba.

Haya ndio matunda ya Mapinduzi ya Zanzbar na nasema Mapinduziii….diamaaa hasa kwa vile maana yake ni maendeleo kwa wote.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.