Habari za Punde

Profesa Chris Maina Peter Aibuka Kidedea Tume ya Kimataifa ya Sheria

 Bi. Lilian  Mukasa ,Afisa wa  Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambaye pia  anahusika na  masuala ya   Uchaguzi  ( Election Officer)  akiwapigia kura wagombea ambao wameomba kuwa wajumbe wa  Tume ya Kimataifa ya Sheria. Nyuma anaonekana  Mgombea wa Tanzania, Profesa Chris Maina Peter ambaye alishindana na  wagombea wengine 13 kutoka Afrika ambapo  walitakiwa nane  kati ya hao  13.  Afisa  Lilian  kwa  nafasi yake kama Election Officer alikuwa na  jukumu kubwa  la kusaidia na  kufanikisha mgombea wa Tanzania anapata kura za kutosha.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania    Katika  Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi  akiwa na  Profesa Chris Maina Peter aliyesimama pamoja na  baadhi ya Maofisa wa Uwakilishi wa Kudumu  wa Tanzania mara baada ya  kutangazwa kwa majina ya  wagombea  34 ambao  walishinda  kwa  kupigiwa  kura ya  siri  na  Wajumbe wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa kuwa  wajumbe wa  Tume ya Kimataifa ya Sheria ( ILC) katika uchaguzi  uliofanyika  jana  ( alhamisi) hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
Na  Mwandishi Maalum,  New York

Profesa  Chris   Maina Peter ,  kutoka  Tanzania, ni kati ya     wagombea  nane miongoni  mwa wagombea   13 kutoka   Afrika, ambao jana  ( alhamisi )   Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa  liliwapiga kura  ya siri ya  kuwachagua kuwa  wajumbe wa   Tume ya Kimataifa  kuhusu masuala ya  Sheria ( International Law  Commission).

Ushindi wa Profesa  Maina ambaye ataitumikia   Tume   hiyo wa miaka mingine mitano  kuanzia Januari 2017, pamoja na juhudi   zake binafsi za kujinadi, kujitangaza, kwa wajumbe  193 wa Baraza Kuu la Umoja wa Matifa, na  akisheheni sifa na  weledi mkubwa katika sheria za kimataifa. Ushindi  wake umechangiwa zaidi na   kazi kubwa iliyofanywa na   Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  Balozi  Tuvako Manongi  kwa kushirikiana na Maafisa wake ambao walifanya kazi kubwa ya kumkampenia  na  kumwombea kura.

 Ingawa Profesa Maina  anaingia kama  mtu binafsi  katika  kazi za   ILC anabeba   jina na kuipeperusha  bendera ya  Tanzania katika   Tume hiyo. Na kwa sababu hiyo,  ushiriki wa Serikali  katika kupendekeza jina lake pamoja na  kumsaidia katika kampeni ilikuwa ni sehemu  kubwa  ya  kufanikisha hatua hiyo muhimu ya kuendelea tena kuitumikia  Tume  kwa pindi cha pili cha miaka mitano.

 Katika  uchaguzi huo  wa jana ambao ulikuwa na ushindani mkubwa huku ukishuhudia  nchi kubwa kama  Ufaransa ikishindwa  kufurukuta.  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  lilitakiwa kuwachagua  wajumbe  34  watakaohudumu  katika  Tume hiyo kwa mgawanyo wa wajumbe   nane kutoka Afrika,    wajumbe  Saba kutoka  Asia-Pacific ,  wajumbe  wanne kutoka Ulaya ya Mashariki,  wajumbe saba kutoka  Amerika  ya  Kusini  na Visiwa vya  Caribbean  na  wajumbe  nane kutoka  nchi za Ulaya Magharibi na  nchi nyingine.

 Baada ya  upigaji  huo wa kura ya  sira,  washindi waliotangazwa   kwa   upande wa Afrika, waliochaguliwa   ni  Chris Maina Peter(Tanzania) Ahmed Laraba (Algeria), Tacouba Cissé (Ivory Coast), Dire D. Tladi (South Africa), Hussein A. Hassouna (Misri), S. Amos Wako (Kenya), Charles C. Jalloh (Sierra Leone) na Hassan Ouazzani Chahdi (Morocco).

 Kutoka  Asia-Pacific  waliochaguliwa ni  Ali bin Fetais Al-Marri (Qatar), Mahmoud Daifallah Hmoud (Jordan), Huikang Huang (China), Shinya Murase (Japan), Hong Thao Nguyen (Vietnam), Ki Gab Park (Jamhuri ya Korea ) na Aniruddha Rajput (India).

Waliochaguliwa  kutoka  Amerika ya Kusini na Caribbean ni  Carlos Argüello Gómez (Nicaragua), Juan Manuel Gómez-Robledo (Mexico), Claudio Grossman Guiloff (Chile), Juan Jose Ruda Santolaria, (Peru), Gilberto Vergne Saboia (Brazil), Eduardo Valencia -Ospina (Colombia) na Marcelo Vázquez-Bermúdez (Ecuador).

Wajumbe kutoka Ulaya ya Mashariki waliochaguliwa ni   Bogdan Aurescu (Romania), Kirumi Anatolyevitch Kolodkin, (Shirikisho la Urusi), Ernest Petric (Slovenia) na Pavel Šturma (Jamhuri ya Czech).

Kwa upande wa  Ulaya Magharibi na  nchi nyingine  waliopita ni , Concepción Escobar Hernández (Hispania), Patrícia Galvão Teles (Portugal), Marja Lehto (Finland), Sean David Murphy (United States), Georg Nolte (Ujerumani), Nilufer Oral (Uturuki), Agosti Reinisch (Austria) na Michael Wood (United Kingdom)

Majukumu   ya  Tume ya  Kimataifa kuhusu  sheria   pamoja  na mambo mengine, ni  kukuza na kuendeleza sheria za kimataifa,  kutoa ushauri wa kitafiti kuhusu sheria mbalimbali, kupitia  masuala yahusuyo  sheria na  mikataba ya kimataifa.
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.