Habari za Punde

Rais Dk Shein afanya uteuzi wa naibu Mawaziri, Wakurugenzi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amefanya uteuzi wa Naibu Mawaziri katika Wizara tatu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Walioteuliwa ni Mihayo Juma Nhunga, ambae anakuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Shadia Mohamed Suleiman anakuwa Naibu Waziri Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto na Shamata Shaame Khamis, anaekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ.

Viongozi hao wameteuliwa kutokana na uwezo aliopewa Rais chini ya kifungu cha 47 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha Dk. Shein amemteua Dk. Sira Ubwa Mamboya kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi chini ya uwezo aliopewa na kifungu cha 66 cha Katiba ya Zanzibar.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 53 cha katiba hiyo, amefanya uteuzi wa Wakurugenzi wa Idara tatu katika Wizara mbili za Serikali.

Walioteuliwa ni Ramadhan Khamis Juma kuwa Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi katika Wizara ya Afya, Attiye Juma Shaame kuwa Mkurugenzi Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Afya na Mohamed El-Kharousy kuwa Naibu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza Novemba 4, 2016.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.