Habari za Punde

Wafanyakazi Shamba la mipira Kichwele waomba kukabidhiwa shamba



 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma{ ZAPSWU } Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha ZAPSWU Nd. Nd.Ameir  Mwadini na kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu wa Chama hicho Bibi Mwatum Othman.

 Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi  wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar { ZAPSWU } Bibi Mwatum Othman aliyesimama akitoa ufafanuzi katika Kikao cha mrejesho wa agizo la Balozi Seif aliloupa Uongozi huo mnamo Tarehe 9 Juni mwaka 2016 wa kukutana na Wizara ya Fedha kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi wa shamba la mipira Kichwele.

Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi  wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar Nd. Ameir Mwadini.
Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi  wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar { ZAPSWU } wakifuatilia mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Wafanyakazi wa shamba ya mipira Kichwele liliopo Wilaya ya Kaskazini “B” wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa utaratibu utakaowapa idhini ya kulihudumia shamba hilo kiuzalishaji  baada ya Kampuni iliyopewa  jukumu la kuliendesha shamba hilo ya Agro Tec kushindwa kuliendeleza.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma{ ZAPSWU } Tawi la Shamba hilo Bibi Kazija Sheha Mohammed alitoa ombi hilo wakati Uongozi wa Chama hicho Taifa ulipofika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  kufanya mrejesho wa agizo aliloupa mnamo Tarehe 9 Juni mwaka 2016 wa kukutana na Wizara ya Fedha kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi wa shamba hilo.

Bibi Kazija alisema wafanyakazi wa shamba la mipira Kichwele kwa sasa wanaendelea kukabiliwa na ukali maisha kufuatia Uongozi wa Kampuni ya Agro Tek kusitisha uzalishaji wa mipira uliokwenda sambamba na kulimbikiza madeni ya mishahara ya muda mrefu ya wafanyakazi hao.

Alisema endapo Serikali Kuu itaridhia ombi lao upo uwezekano mkubwa kwa ari waliokuwa nayo wafanyakazi hao kuliendeleza shamba hilo kwa nia ya kutafuta faraja ya kupunguza changamoto za muda mrefu zinazowakabili katika mradi huo wa uwekezaji.

Alieleza kwamba changamoto kama hiyo kwa wafanyakazi wenzao wa Kisiwa cha Pemba imeshapatiwa ufumbuzi baada ya Uongozi wa Mkoa kuwapa ruhusa ya kuendeleza mradi huo ili kukidhi mahitaji yao.

Bibi Kazija alieleza kwamba wafanyakazi wa shamba la Mipira Pemba wamerejea tena katika uzalishaji wa zao la mipira na kuwaingizia mapato yanayosaidia kurejesha madeni, kulipa wafanyakazi pamoja na walinzi wa shamba hilo.

Alifahamisha wazi kwamba katika kuhakikisha mradi huo wa mipira kwenye shamba la Kichwele unarejea katika uhalisia wake Wafanyakazi hao karibu 350 waioachwa kabla ya kufungwa mradi huo tayari wameshajipanga hata Kiuongozi katika kuona kazi za uendelezaji na ugemaji wa utomvu zinafanyika kama awali.

Mapema akitoa mrejesho wa agizo la Balozi Seif  la kukitaka Chama cha Zapswu  kukutana na Wizara ya Fedha kutafuta ufumbuzi wa tatizo la shamba hilo Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Nd.  Suleiman Juma alisema Wizara ya Fedha haikuwa na kipengele cha moja kwa moja kinachoruhusu njia ya ulipaji wa madeni ya Wafanyakazi wa Shamba hilo.

Nd. Suleiman alisema Uongozi wa Wizara ya Fedha ulifafanua wazi kwamba inakuwa vigumu kwa wafanyakazi hao kupatiwa haki zao kupitia Wizara hiyo kwa vile Kampuni iliyowaajiri ilikuwa binafsi.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi  wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar { ZAPSWU } Bibi Mwatum Othman aliiomba Serikali Kuu kuwaagiza watendaji wake waandamizi na wale wa ngazi za Kati kutoa ushirikiano wa karibu na Vyama vya Wafanyakazi kwa nia ya kupunguza migogoro kati ya waajiri na Wafanyakazi.

Bibi Mwatum alisema yapo malalamiko mengi kwa baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi tofauti yanayokosa kushughulikiwa licha ya kuripotiwa kwenye vyama vya Wafanyakazi sababu ni dharau za watendaji waandamizi wenye tabia ya kuwakimbia kwa mazungumzo viongozi wa vyama vya wafanyakazi.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Taifa halina nia ya kulikataa ombi la wafanyakazi hao, lakini kinachopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni kulifikisha Serikalini ili kuangalia hatua zinazostahiki kuchukuliwa.

Balozi Seif alisema Ilani ya CCM Imekuwa ikitoa miongozo kwa wananchi kutafuta mbinu za kujiajiri ili kuendesha maisha yao ya kila siku na lazima yasimame katika njia na misingi ya halali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliupongeza Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma{ ZAPSWU } kwa jitihada unazochukuwa za kufuatilia changamoto zinazowakabili wanachama wao katika taasisi mbali mbali hapa nchini.
Kampuni ya Agro Tec ilikuwa ikikabiliwa na madeni ya zaidi ya shilingi Milioni 284,839,982/- ikiwa ni pamoja na Mishahara ya wafanyakazi  wa mashamba ya Mipira Unguja na Pemba, fedha za Likizo pamoja na deni la  ZSSF kwa wafanyakazi wake katika kipindi kati ya miezi Mitatu hadi Minane.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.