Habari za Punde

Dk Shein: Misikiti iwe ni sehemu ya kuwaunganisha waislamu


 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                    30.12.2016
---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa si vyema misikiti kuwa chanzo cha mizozo, mivutano na migongano na badala yake iwe sehemu ya kuwaunganisha Waislamu kwani hayo ndio mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W).

Alhajj Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya ufunguzi wa masjid Muhammad (S.A.W) uliopo Fujoni Mzambarauni, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akitoa nasaha zake kwa waumini wa Kiislamu wa Fujoni na vijiji vya karibu, Alhajj Dk. Shein aliwasisitiza waumini hao kwamba kamwe haitakuwa jambo jema msikiti kuwa chanzo cha mizozo na migongano kwani msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu.

Alhajj Dk. Shein aliwataka waumini hao kuufanya msikiti huo kuwa sababu ya watu kuzidi kuwa wamoja na kushikamana pamoja na kuendeleza masuala ya dini huku akiwataka kutafuta uongozi madhubuti wa msikiti huo.

Katika nasaha zake hizo, Alhajj Dk. Shein alieleza kusikitishwa kwake na tukio lililofanywa na  baadhi ya waumini wa Kiislamu hivi karibuni huko kisiwani Pemba la kuchoma moto msikiti, kuiba mashine ya kupandishia maji sambamba na baadhi ya waumini kubaguana katika baadhi ya misikiti.

Aidha,, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa katika historia ya Uislamu, misikiti imetoa mchango mkubwa katika kuuendeleza Uislamu kama chemu chemu muhimu ya elimu katika fani mbali mbali za dini.

Vile vile, Alhajj Dk. Shein alisema kuwa misikiti ina mchango muhimu katika kuwaunganisha wanajamii wanaosali pamoja na huwapelekea kujuana na kushirikiana katika masuala mbali mbali na kusisitiza umuhimu wa kuitunza misikiti ukiwemo msikiti huo mpya ambao una sifa zote.

Aliwaeleza Waumini hao kuwa ni jukumu lao wakiwa wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema na mafundisho ya dini na kusisitiza kuwa ulinzi wa watoto ni pamoja na kuwapa elimu, ili wajue mazuri na mabaya sambamba na kuwapatia hifadhi ya maisha yao kwa kuwaepusha na vitendo vya udhalilishaji na unjanjasaji.

Akiendeleza nasaha zake, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa  kuwapatia watoto elimu ni jukumu la kila mzazi, hivyo wazazi pia wanapaswa kuwa ushirikiano walimu kwa kila hali ili wapate moyo wa kuitekeleza kazi yao ambayo inajulikana kuwa ni ngumu.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuyatumia mafunzo ya Bwana Mtume (S.A.W) ili kuiepusha jamii na mifarakano kwa kuimarisha umoja, kwani umoja ni nguvu.

Alhaj Dk. Shein alisema kwua kila mmoja kwa nafasi yake ajue ana wajibu wa kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto na kinamama pamoja na vitendo vyote vya uhalifu ili jamii iendelee kuishi kwa mani.

“ Tushirikiane katika kuvikabili vitendo vinavyosababishwa na kumongonyoka kwa maadili, malezi na utamaduni wetu tulioachiwa na wazee wetu”,alisema Alhajj Dk. Shein.

Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwataka Waumini wa Dini ya Kiislamu, kila wanapopata wasaa waendelee kukumbushana umihumu wa kujiepusha na makatazo ya Mwenyezi Mungu ili kujikinga na adhabu zake na kuyafanya mambo yatakayowapa faida hapa duniani na huko akhera waendako.

Katika hotuba yake kwa Waumini hao, Alhajj Dk. Shein aliwaahdi kwamba maombi yao yamepokewa na yatafanyiwa kazi na kuwataka kuendelea kuwa na subira kwa yale mambo ambayo yanaweza kuchelewa katika utekelezaji kwa mashirikiano ya Mwakilishi wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Idd..

Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wale wote walioshiriki katika ujenzi wa msikiti huo azidi kuwafunguliwa milango ya riziki bna watilie baraka katika kufanya shughuli zao.

Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda  Alhajj Balozi Seif Ali Idd, alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kuhakikisha msfadhili wa ujenzi wa msikiti huo anapatikana ikiwa ni pamoja na kutumiza ahadi yake ya kutafuta mfadhili wa msikiti huo.

Alhajj Seif Idd aliwaeleza wananchi wa Fujoni kuwa kila muumini wa dini ya Kiislamu ana haki ya kusali msikiti huo tena bila ya kuingiza ubaguzi wa aina yeyote zikiwemo itikadi za kisiasa kwani hiyo ni nyumba ya Mwenyezi Mungu kila mmoja ana haki kuitumia.

Nao wananchi wa Shehia ya Fujoni katika risala yao walieleza  furaha yao kwa kujengewa msikiti huo mpya ambapo walieleza kuwa hapo kabla msikiti uliokuwepo ulikuwa haukidhi haja kutokana na udogo wake, uchakavu sambamba na kwenda masafa marefu kufuata misikiti kwa ajili ya sala za Idd na Ijumaa.

Katika risala hiyo iliyosomwa na Ustadhi Salmin Mbarouk, wananchi hao walitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Balozi Seif kwa kuchukua juhudi katika kutekeleza ahadi yake ya kutafuta mfadhili wa ujenzi wa msikiti huo na kumpongeza mfadhili huyo ambapo pia walitumia fursa hiyo kutoa maombi yao kwa Rais.

Mapema Sheikh Othman Maalim akitoa mawaidha katika ufunguzi huo alieleza umuhimu kwa waislamu kujenga misikiti sambamba na kuendeleza utamaduni wa kutoa sadaka kwa lengo la kupata fadhjila za Mwenyezi Mungu na kufuata mienendo ya Mtume Muhammad (S.A.W).

Sheikh Othman Maalim alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Mfadhili wa msikiti huo Ali Buwardy pamoja na msimamizi wa ujenzi wa msikiti huo Bwana Yakoub Othman huku akieleza jinsi Allah (SW) anavyochukia wale wanaotumia kinyume fedha za ujenzi wa misikiti.

Nae Sheikh Fadhil Soraga alisisitiza umuhimu wa waislamu kujenga misikiti pamoja na kuepuka mifarakano na migogoro katika kuiendesha msikiti hatua ambayo haileti tija kwa waislamu na uislamu wenyewe huku akieleza haja kwa waumini kuwa na  tabia njema itakayompwekesha Allah (S.W)

Viongozi mbali mbali wa Serikali, viongozi wa dini ya kiislamu, wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya Zanzibar walihudhuria katika ufunguzi huo wa masjid Muhammad (S.A.W).

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.