Habari za Punde

Makhatib Misikiti ya Ijumaa walaani vikali kitendo cha kukashifiwa Mtume Muhammad swalla Allaahu 'alayhi wasallam

Na mwandishi wetu

Ikiwa leo ndio Ijumaa ya kwanza tokea  kutokea kwa tukio kubwa linaloendelea kutikisa visiwani Zanzibar na dunia kwa ujumla la kijana Abdallah Saleh Aballah kudaiwa kumkashif na kumtusi kiongozi wa umma wa waisilamu Mtume Muhammad SAW waumini wa dini hiyo kupitia makhatib wa khutba za ijumaa kisiwani Pemba wamelaani na kupinga kwa nguvu zote kitendo hicho kilichotokea hivi majuzi na kusambaa picha zake katika mitandao ya kijamii.

Akiwahutubia waumini wa dini hiyo katika Masjid Lkhalil Mtoni chakechake Pemba Ust Abdulqadir Bakar Haji amesema kua tukio lililotokea nchini  la kumkashif Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam kwa maneno machafu na ya kufuru ni tukio baya na ubaya wake mpaka wanyama na mimea inachukia.

Amesema tukio hilo limegusa waisilamu wote  kwani mtume ana nafasi adhimu  kwa Allah S.W huku akinukuu maneno matukufu ya kitabu cha qur'an ambapo Allah S.W anasema “wewe uwe  mtukufu wa kutajwa na sio wa kukashifiwa”

Amesema Allah SW amemtukuza Mtume wake swalla Allaahu alayhi wasallam halafu anatokea mtu jahili asiyefahamu uisilamu wala nafasi ya Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam anamkashifu  kwa maneno machafu kisha kudai  eti ni   muislamu amesema huo si ukweli halisi.

Ust  Abdulqadir amefahamisha kuwa, vipi mtu muisilamu ametoka katika mishipa ya kiisilamu na amekulia katika uisilamu athubutu kumtusi na kumkashif mtume Muhammad swalla Allaahu alayhi wasallam  kama ilivyoonekana.

Amesema kutokana na ukubwa wa tukio kama watu watalinyamazia na hawataonyesha hisia zao za kuchukia,  hatari yake  katika umma itabakia hapa duniani na itachukua muda mrefu huku  adhabu za Allah zitatokea.

Nae Khatibu wa masijid L-jumaa wa Miembeni chakecheke  Shekh Said Abdalla  Nassor  katika khutba yake kwa waumini wa dini hiyo amelaani na kupinga  kwa nguvu kitendo hicho cha kumkashif Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam  ambapo amesema, Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam ni rehma kwa waisilamu wote duniani.

Amesema Zanzibar ni eneo moja muhimu sana kwa elimu ya dini ya kiisilamu, watu mbalimbali walikuja  kuchukua elimu hiyo ili kujua  vipi watamnusuru Mtume wa Allah S.W akitaja watu kutoka Comoro walikuja na wengineo lakini leo kunatokea tukio la kumkashifu Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam amesema jambo hilo ni kubwa na ikisikika katika mataifa mengine ni aibu kubwa kwa Zanzibar.

Katika hatua nyengine Sheikh Said ametoa wito kwa vyombo vya sheria kumchukulia hatua kali tena za kisheria wala sio za kisiasa kijana huyo anayedaiwa kumkashifu Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam.

Akitilia mkazo katika hukumu amesema kua, hakuna budi kumchukulia hatua kali  ili kunusuru kutokea kwa matukio mengine makubwa mbeleni  yatakayopelekea umma kuingia katika machafuko huku akitolea mfano wa nchi za Afrika ya kati na Baghdad nchini Iraq juu ya fikra za kimakundi zinazotikisa dunia.

Katika msikiti huo uliyoonekana kufurika waumini kutoka maeneo tofauti Khatib huyo amesema kua kitendo alichokifanya kijana huyo kinapaswa kulaaniwa kwa hali ya juu kwani hata ikitokea kupimwa inaweza kuonekana kua hakua amelewa na kama alilewa kweli kwanini asiwatukane viumbe wengine kama kuku, Ng’ombe na wengineo.

Muumini wa dini ya kiisilamu aliyesali katika masjid lkhali Zahor Saleh Ali amepinga na kulaani kitendo kilichojitokeza cha kumkashif Mtume swalla Allaahu alayhi wasallam na kusema kua mtuhumiwa achukuliwe hatua za kisheria zinazostahiki huku akiwataka wananchi popote pale duniani waisilamu na wasio waisilamu kila mmoja aheshimu dini ya mwenzake kwani kukashifu dini ya mwenzio  ni kosa na hata serikalini pia unaweza kuingia hatiani.

Mwisho kabisa amewataka waisilamu wasome kwa bidii ili kutambua ukubwa wa Allah SW na utukufu wa Mtume Muhammad swalla Allaahu alayhi wasallam   ili isitokee  mtu kufanya maasi eti kwa kisingizio cha ulevi amesema  itakua hajafanya kitu na wala sio sababu ya msingi.

Waumini wa dini ya kiisilamu kisiwani Pemba katika misikiti  mbalimbali ya Ijumaa kwa kiwango kikubwa wameonekana kuitikia wito wa Naibu katibu Mufti wa Zanzibar Shekh Salum Fadhil Soraga wa kuwataka makhatib wa khutba za ijumaa kulaani tukio hilo,  wito aliyoutoa juzi katika kikao maalum kilichoongozwa na Mufti mkuu wa Zanzibr Fadhilat Sheikh Saleh Omar Kaabi na waandishi wa habari kwa kulaani tukio hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.