Habari za Punde

Ndoa za utotoni chanzo cha kifafa cha mimba: wataalamu wasemaNa Haji Nassor, Pemba

‘’KUANZIA umri wa miaka 10 hadi 19, yote ni hatari kwa mtoto wa kike kupata ujauzito kitaalamu.

Wataalamu wa afya ya uzazi, wanasema kwa ujumla kuanzia siku ya mwanzo mimba inapotunga hadi kufika siku ya kuzaliwa, huzungurukwa na matatizo, lakini kwa wale wenye umri ni mdogo tatizo huwa kubwa zaidi.

Elimu ya afya ya uzazi, imekuwa ikitolewa hata kwenye vituo vya afya na kliniki, ili kuisadia jamii kujua athari za mimba za umri mdogo, lakini bado tatizo linaendelea kuwepo.

Makala haya ilikutana na daktari wa hospitali ya wilaya ya Chake Chake, Zeana Abdull-aziz Ibrahim, ambae anasema mimba katika umri mdogo sasa ni tatizo kubwa.

Anasema kwa kawaida, huzigawa mimba katika misimu mitatu; miezi mitatu ya mwanzo, kati na mwisho ambapo kila hatua huzunguruka tofauti na hatua nyengine.

Anasema kwa  mtu aliebeba ujauzito akiwa na umri baina ya miaka 10 hadi 19, anaweza kushambuliwa na matatizo mbali mbali ambapo kwa miezi mitatu ya mwanzo (first trimester) kuna mlolongo wa magonjwa yanayoweza kumpata mama mjamzito.

Kwa walio chini ya umri wa kitaalamu wa kuweza kubebea ujauzito na kuzaa, yaani kuanzia miaka 20 na kuendelea, wanaweza kupata magonjwa ya kuambukiza.

Kwa mfano kwa mtoto aliebeba mimba chini ya umri, anaweza kushambuliwa na wadudu kama bacteria, fangasi na virusi ambao  wanashambuliwa njia za mkojo.

Mtaalamu huyu anasema hata kinga ya mwili kwa mtu aliebeba ujauzito akiwa na umri mdogo hupotea, ambapo hapo magonjwa kama malaria na hata Ukimwi huwa ni rahisi kwake, tofauti na mwanamke aliepata ujauzito kwa umri unaoshauriwa kitaalamu.

Lakini hata magonjwa ya zinaa, kama vile Ukimwi, kaswende hujitokeza kwa mjamzito aliebeba mimba akiwa hajafikia umri, sambamba na mtoto kuwa na ukuaji usioridhisha.

Upungufu wa damu kwa watoto wanaobeba mimba wakiwa na umri mdogo huwa la kawaida na hapo mama mjamzito anaweza kupoteza maisha ndani ya wiki 12 za kwanza.

Kwenye hatua ya pili ambazo ni kuelekea wiki 24, mama mjamzito ambae ameshabeba mimba kabla ya mwili kuruhusu, damu kwa kipindi hiki huwa baina ya asilimia 9 hadi 7, na sehumu ya pili huwa baina ya asailimia kati ya 7 hadi 6 na mwisho ‘sear via’ ambapo mjamzito huhitaji masaada wa damu.

Kwenye miezi mitatu ya mwishio, mama mjamzito ambae ameolewa na kupata ujauzito akiwa mdogo,  hukabiliwa na ugonjwa wa presha wa mara kwa mara.

Zile wiki za kuanzia za 28 hadi 39, ambapo nguvu ya msukumo wa damu kwa kawaida huwa baina ya mwendo wa 120 hadi 140, lakini kutokana na umri wake mdogo wa kubeba mimba, hushuka hadi kufikia 90.

Kwa walio chini ya umri wa kuweza kuzaa, mifupa ya uzazi hukumbana na adhabu kubwa wakati mtu anapojifungua, na ndio maana kwa hawa ambao umri wao ni mdogo wakati huo wa huweza hata kupoteza maisha.

Kwa hospitali ya Chake Chake, uchunguzi umeonesha kuwa, wastani wa wasichana walio chini ya umri wapatao 18, kila mwezi hulazimika kuongezewa njia ya uzazi ili waweze kujifungua kutokana na mifupa yao kutopevuka.

Hospitali hiyo ambayo huchukua  wajawazito kutoka wilaya ya Mkoani na Chake Chake, wastani wa mama wajawazito 300 kwa mwezi hupokelewa, ambapo kati yao saba ambao ni chini ya miaka 18 hufanyiwa upasuaji.

Wakati ni wanne walio chini ya umri na kujifungua kwa njia za kawaida, ingawa wapo wengine 10 ambao njia zao kuchanwa ili kuongezewa nguvu.

Kubwa zaidi ambalo hujitokeza kwa waliobeba mimba kabla ya kufikia umri, ni kukaa na uchungu zaidi ya siku mbili jambo ambalo kwati huo huwezi kujitokeza hata michubuko mtoto akizaliwa.

Na wakati mwengine hukumbana na maradhi ya kukojoa mfululizo au haja ndogo na kubwa zote kutoka seheumu ya siri ya mbele bila ya kizuizi.

Aidha kwa watoto wanaoolewa na kisha kubeba ujauzito, pia wanaweza kukosa watoto wenye uzito unaotakiwa, (normal weight) ambao ni kuanzia kilo 2.5, 3.0 ingawa wengine wao huzaa watoto wenye uzito baina ya kilo 1.5, kilo 2.4 na kilo 2.0

Msichana Sanura (17) ambae sio lake rasmi, wa Uwanadani wilaya ya Chake Chake ambae alijifungua mwaka jana mtoto wake akiwa na uzito wa kilo 1.8 anasema, alipata mimba hiyo kabla ya kuolewa na alikaribia kufa wakati wa kujifungua.

Anasema tokea miezi mitatu ya mwanzo, baada ya kujificha sana ili wazazi wake wasifahamu, alishindwa na kuamua kumueleza dada yake.

Yeye anasema alikuwa anaona ‘kizungu zungu’ kila wakati na kuanzia miezi mitatu ya mwanzo hakumbuki siku aliokula chakula akashiba kutokana na mwili wake, kukosa hamu ya kula.

“Niliacha skuli na madrasa mwenyewe, na mimi nikawa mtu wa kulala saa 24, maana sikuwa natamani kufanya lolote kutokana na mwili kukosa nguvu,” alisema.

Anasema mwezi wa kujifungua ulipofika, matatizo mwilini mwake yaliongezeka, na kila siku moja hakuwa na hakika kwamba atakutana na siku ya pili.

Aliamua kukaa karibu na hospitali kuu ya Chake Chake, ili lolote litakalojitokeza awe karibu, ambapo siku mbili kabla ya kujifungua alipelekewa hospitali.

“Mimi niliumwa na uchungu nadhani siku tatu na kisha sikuwa na nguvu ndipo madaktari walipoamua kuniongezea damu  hadi nilipomzaa mwanangu,” anasema.

Ingawa mwanawe ameshafariki miezi mitatu iliopita, lakini anasema anakumbuka mimba hiyo jinsi ilivyomtesa na kisha mwanamme kuamua kuhakama Pemba hadi leo.

Mama wa msichana huyu, anasema mwanawe wakati wa ujauzito wake aliwahi kutiwa damu mara mbili, mara moja kabla ya wao kugundua na mara nyengine wakati akitaka kujifungua.

Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman,  anasema kama wazazi hawakuwa makini wanaweza kukosa watoto wao  wakati wanapojifungua, kutokana na tabia yao ya kuwaozesha waume mapema.

Mwananchi Amini Haji Makame, anasema kama jamii haikuweka  mikakati vifo vya watoto wa kike vitakuwa vinaendelea.

Sheikh Mohamed Adam wa Mkoani, anasema waislamu wamekatazwa kujitia katika maagamizi kwa mikono yao, likiwemo la ndoa za utotoni.

“Kama ikionekana ndoa ikifungwa hata mtu mwenye umri mkubwa, basi uislamu umekataza aina hiyo, maana ndani yake mnamatatizo ya kiafya’’,alifafanua. 

Uchunguuzi umebaini, wapo watoto wa kike 240 wameripotiwa kukatishwa haki yao ya elimu kwa kuolewa, ambapo idadi hiyo ni ile iliopatikana katika taasisi mbali mbali na kuanzia  2013-2015.

Azimio la Umoja wa Mataifa la kupunguza aina zote za udhalilishaji kwa wanawake (CEDAW) haliruhusu watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 kuolewa.

Kila mwaka, watoto wa kike milioni 7.3 dunaini kote walio  chini ya umri wa miaka 18, hushika mimba, hii ni kwa mujibu wa ripoti Shirika la Idadi ya watu Duniani  ya mwaka 2013.

                             

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.