Habari za Punde

Rais Magufuli Amewaagiza Wakuu Mikoa,Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri Zote Nchini Kutenga Maeno kwa Ajili ya Wafanyabiashara Ndogondogo Machinga.

Na Frank Mvungi, Maelezo. Dar es Salaam
6.12.2016
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wafanya biashara ndogondogo maarufu kama wamachinga.

Akizungumzia maagizo hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene alisema Rais Magufuli pamoja na kutenga maeneo hayo,  Viongozi na watendaji hao pia wanapaswa kuangalia utaratibu wa kutenga maeneo ya katikati ya miji yenye wateja wa bidhaa zinazouzwa kwa kuangalia uwezekano wa kufunga mtaa japo mmoja ili utumike kwa kazi za kimachinga.

Akifafanua zaidi Simbachawene alisema utaratibu huo haumaanishi kuwa wafanyabiashara hao wapange bidhaa barabarani bali wazingatie utaratibu utakaowekwa wa kufungwa kwa mtaa mmoja au miwili itakayobainishwa kwa mpango shirikishi ili kukuza kipato cha wananchi.

“Wajasiriamali hawapaswi kujenga  vibanda ambavyo vinageuza mandhari ya maeneo hayo kuonekana machafu “alisisitiza Simbachawene.

Aliongeza kuwa  Rais Magufuli licha ya kuwapongeza watendaji wote wa Ngazi mbalimbali kwa kazi nzuri wanayoifanya,  amewaagiza pia kuweka utaratibu shirikishi katika kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ndogondogo hasa swala la maeneo ya kufanyia biashara.

Aliongeza kuwa mamlaka zote nchini zinatakiwa kuandae maeneo rafiki yenye mahitaji muhimu ili yaweze kufikika kwa urahisi na kuruhusu biashara kufanyika bila shida yeyote kabla ya kuwahamisha wafanyabiashara hao  kwa njia shirikishi.

Katika kipindi cha hivi Karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ya kuwahamisha wananchi katika maeneo yao wanayofanyia shughuli zao za kiuchumi wakiwemo wamachinga hali iliyopelekea baadhi yao kupoteza mitaji yao ambayo wamekopa katika vikundi vya kuweka na kukopa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.