Habari za Punde

Balozi Seif akagua Bandari ya Kigomasha

 MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe;Balozi Seif Ali Iddi, akiangalia ramani ya eneo la Mnarani Kigomasha linalomilikiwa na shirika la bandari Zanzibar, kushoto ni Mkurugenzi wa shirika hilo Abdalla Juma.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA).

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma kati kati akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  wa kwanza Kulia tatizo la eneo la bandari la Kigomasha ambalo kitaalamu haliwezi kujengwa Gati kutokana na kina kidogo cha maji yake ya Bahari.

 MKURUGENZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Badru Amani Juma, akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe;Balozi Seif Ali Iddi, eneo ambalo wanataka kutengeneza ili helkopta iweze kutua katika sehemu ya Manarani Kigomasha Wilaya ya Micheweni, wakati balozi alipokwenda kukagua eneo litakalojengwa bandari na kituo cha Uhamiaji.(Picha na Abdi Suleiman, PEMBA).
Balozi Seif akikagua Kitalu cha miche mbali mbali ya matunda, Viungo na Mbao kinachoendeshwa na Wananchi wa Kijiji cha Junguni ndani ya Mkoa Kaskazini Pemba chini ya Mradi wa Tasaf.

Na Othman Khamis OIMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kuandaa mchakato wa kuwakutanisha Wataalamu wa Sekta hiyo ili wajadili na hatimae kupata kauli moja itakaobaini eneo muwafaka linalostahiki kujengwa Gati Rasmi ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.


Alisema hatua hiyo inastahiki kutekelezwa vyema kama ilivyoagizwa na Serikali Kuu la kutaka kujengwa kwa Gati katika Bandari ya Kigomasha ili kujaribu kudhibiti mapato ya Taifa yanayotokana na uingiaji na utokaji holela wa vyombo vya Baharini pamoja na usalama wa eneo hilo.



Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipokagua Bandari ya Kigomasha ambayo baadhi ya Wavuvi huitumia kusafirishia magendo akiwa katika ziara ya Siku Tatu Kisiwani Pemba kuangalia miradi ya Maendeleo na ile
ya Ustawi wa Jamii.



Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshaamua na kutoa mapendekezo ya kujengwa kwa Bandari Rasmi ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.



Alisema Uongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Mashariki tayari umeshalipigia kelele eneo hilo la Bandari ya Kigomasha linaloonekana kutumiwa na watu  wasiofahamika mazingira yao wakitokea nje ya Visiwa vya Zanzibar jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Taifa.



Balozi Seif alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutumia vyombo vyake vya ulinzi lazima itengeneze mazingira kuvihami Visiwa vyake kutokana na dalili zilizo wazi zinazobainisha baadhi ya wahalifu wanaingia Nchini kinyume na taratibu zilizowekwa za Uhamiaji.



Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma alisema eneo la Kigomasha limekuwa na kina kidogo cha maji kiasi kwamba Kitaalamu inakuwa vugumu kulitumia kwa shughuli za Bandari licha ya kupendekezwa na Idara ya Uhamiaji kutokana na uingiaji holela wa wageni.



Nd. Abdulla alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba lipo eneo Shumba Mjini ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ambalo linaweza kutumiwa kwa shughuli za Gati endapo litawekewa mazingira mazuri ya Miundombinu kutokana na kina kikubwa cha maji.



Naye kwa upande wake Kamanda wa Idara ya Uhamiaji Kisiwani Pemba Abdi Bulushi Juma alisema Kigomasha ni eneo sugu linaloleta usumbufu kwa askari wake wakati wanapofanya doria.



Alisema bandari Bubu ya Kigomasha imekuwa kero na ikiripotiwa matukio mengi ya uingiaji na usafiri wa watu wasiozingatia taratibu zilizowekwa za uhamiaji sambamba na shughuli za magendo ya Karafuu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.