Habari za Punde

Tutatumia Interpol kumsaka muuwaji wa Mtambile: Jeshi la Polisi


Na Haji Nassor, Pemba
JESHI la Polisi mkoa wa kusini Pemba, limesema linangalia uwezekano wa kuwatumia askari wa kitengo cha ‘Interpol’,  ili kufanikisha kumkamata mtuhumiwa wa mauwaji wa kutumia kitu chenye ncha kali, Kassim Amour Seif nje ya kituo cha Polisi Mtambile wilaya ya Mkoani mwezi uliopita .
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema baada ya kuona wanafamilia wanashindwa kutoa ushirikiano, sasa Jeshi hilo linaangalia uwezekano wa kuwatumia askari hao, ili kumtia mikononi mtuhumiwa huyo aliemuua kaka yake Masoud Amour Seif.
Alisema Jeshi la Polisi, linazombinu kadhaa za kumsaka mtuhumiwa na kama wanafamilia wanashindwa kutoa ushirikiano, wao wataendelea kumtafuta kwa mbinu za kitaalamu na wanazozijua wao.
Kamanda huyo alisema kwa kuanzia tayari, wameshasambaza picha ya mtuhumiwa huyo kwenye mitandao ya kijamii, ili kuonyesha kwamba bado anatafutwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Ijapokuwa tulitarajia kuwa wanafamilia hao waliouliwa ndugu yao washirikiane na sisi kumtafuta, lakini hawatowi ushirikiano sasa sisi Polisi, tunazombinu za kumpata’’,alifafanua.
Hata hivyo Kamanda huyo aliwataka wananchi wengine na ambao wanamfahamu mtuhumiwa huyo, wasisite kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, pale watakaposikia tetesi za uwepo wake.
Aidha amewaahidi wananchi kuwa mtuhumiwa huyo hata kama amekimbilia nchi za Kenya, Uganda au pengine popote, wasiwe na wasiwasi, jeshi hilo litamshika na kisha kufunguliwa mashitaka.
Katika hatua nyengine, amesema tayari jalada la kesi yake lipo na linamsubiri mtuhumiwa huyo, na atakapopatikana ili afunguliwe mashitaka, katika vyombo vya kisheria kwa tuhumza zinazomkabili.

Disemba 1, mwaka huu Kassim Amour Seif bdalla wa mkaazi wa Mtambile wilaya ya Mkoani, alivikimbia vyombo vya ulinzi na usalama, baada ya kudaiwa kumuua kaka yake wa damu, nje ya kituo cha Polisi Mtambile, kwa ugomvi ulioanzia kwa wake zao, ambapo hadi sasa hajapatikana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.