Balozi Mdogo Mpya wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi Kushoto akibadilishana mawazo na Balozi Seif nje ya Jengo baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Balozi Mdogo Mpya wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi aliyefika ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiagana na Balozi Mdogo Mpya wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Vuga Mjini Zanzibar.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa anzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa Oman kutokana na historia ya miaka mingi iliyopo ya udugu wa kidamu baina ya Wananchi wake.
Alisema Oman imejitolea kwa nguvu zake kuunga mkono harakati za maendeleo na uchumi za Zanzibar kupitia udumishwaji wa ushirikiano huo ulioasisiwa na Viongozi wakuu wa pande hizo mbili.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akibadilishana mawazo na Balozi Mdogo Mpya wa Omar aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi aliyefika kujitambulisha rasmi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alishauri ziara za kukuza ushirikiano wa pande hizo mbili kwa kujumuisha Maafisa wa Taasisi, mashirika na hata jumuiya za kiraia uendelee kuimarishwa zaidi badala ya kuziachia ziara za sehemu hizo kufanywa na Viongozi wakuu pekee.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman chini ya Utawala wa Mfalme Qabous Bin Said kwa misaada mbali mbali ya maendeleo inayotowa kwa Zanzibar.
Balozi Seif aliutolea mfano msaada mkubwa wa Kiwanda cha Uchapaji Maruhubi kilichopata msukumo wa vifaa vya kisasa vilivyogharamiwa na Serikali ya Oman ambao ni hazina kubwa kwa Zanzibar.
Alisema miundombinu ya kisasa ya vifaa vilivyofungwa kwenye Kiwanda hicho cha Uchapaji itawezesha kazi zote za Serikali, Taasisi na Mashirika yake hivi sasa kuchapishwa katika kiwanda hicho.
Akigusia suala la Mafuta na Gesi Asilia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi huyo Mdogowa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed kuyashawishi Makampuni ya Nchi yake kufikiria wazo la Zanzibar katika kutaka kuwekeza kwenye Sekta hiyo Mpya.
Alisema Zanzibar hivi sasa iko mbioni kujiandaa na uanzishaji wa miradi ya Kiuchumi kupitia sekta ya Mafuta na Gesi ambayo Oman inaweza kusaidia Taaluma kwa vile Nchi hiyo tayari imekuwa mzalishaji mkubwa wa Nishati hizo kwa muda mrefu.
Naye Balozi Mdogo Mpya wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuona uhusiano wa kidugu uliopo baina nchi mbili unazidi kuimarika.
Alisema ahadi iliyotoa Oman kwa Zanzibar katika kugharamia matengenezo makubwa ya Ujenzi wa Jengo la Jumba la Ajabu Forodhani Mjini Zanzibar itatekelezwa kama ilivyopangwa.
Alimfahamisha Balozi Seif kwamba matayarisho ya utengenezaji wa Jengo hilo hivi sasa yako tayari na ameahidi kufuatilia mitakaba iliyofikiwa ili kuona kazi rasmi ya ujenzi huo inaanza bila ya kupoteza wakati.
Dr. Ahmed Humoud Al – Habsi anaiongoza Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Oman Zanzibar kufuatia aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Balozi Ali Abdalla Al – Rashid aliyefariki Dunia ghafla mwezi Mei mwaka 2016 baada ya kusumbuliwa na tatizo la sindikizo la Damu { Blood Presure }.
No comments:
Post a Comment