Habari za Punde

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Balozi Mstaafu Msuya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akisalimiana na Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi aliyefika Ofisini kwake Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi Kushoto akimkabidhi Balozi Seif Ali Iddi Nakala ya Kitabu alichokitunga kinachoelezea uzoefu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya zamani kwenye mazungumzo yao.
Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiwa makini kufuatilia ufafanuzi uliotolewa na Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi wakati akielezea yaliyomo ndani ya Kitabu alichotunga kinachoelezea uzoefu wa Jumuiya ya Afrika Mahshariki ya zamani.
Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi Kushoto akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wa kwanza kutoka kulia ni Msaidizi wa Balozi Mstaafu Msuya, Bwana Msangi Mangachi na aliyepo kati kati ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.(Picha na OMPR) 

Na Othman Khamis OMPR.
Mgawanyo wa fursa za uwekezaji unaofanywa na Makampuni na Taasisi za Kimataifa ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ukizingatiwa vyema kulingana na ushiriki wa Nchi Wanachama utaiongezea dira na umadhubuti Jumuiya hiyo katika malengo yake ya muda mrefu.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mstaafu wa Tanzania ambae kwa sasa amekuwa mhadhiri wa Elimu ya Chuo Kikuu  Nchini Balozi Msuya Waldi Mangachi wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Ofisi za Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Msuya Waldi Mangachi ambae katika mazungumzo hayo alimkabidhi nakala ya Kitabu alichokitunga kinachoelezea uzoefu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya zamani alisema mgawanyo wa fursa hizo utakaokuwa na muelekeo wa kutumia maeneo yote utasaidia kuondoa au kupunguza  malalamiko yanayoweza kuonyesha sura ya upendeleo wa upande mmoja.

Balozi Msuya alisema  sababu za msingi zilizopelekea kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mnamo mwaka 1977 ilitokana na mitizamo tofauti ya kisiasa na hasa falsafa ya kujenga uchumi baina ya Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

Mtaalamu huyo wa Fani ya Udaktari wa  Historia alieleza kwamba Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya zamani isingeweza kufanikiwa bila ya kubadilika kwa mfumo wa uchumi Kimataifa.

Alisema mfumo uliotumika ulizikuta Nchini wanachama  zikizalisha malighafi na kuziuza kwa nchi za Kaskazini na matokeo yake wanunuzi hao walichakachua malighafi hiyo na kuzirejesha kwa wazalishaji hao kama bidhaa  za Viwandani.

Balozi Msuya alifafanua kwamba mantiki ya ushirikiano uliopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bado haijakaa vizuri licha ya kwamba biashara huru ndio njia pekee ya kuimarisha ushirikiano wa Jumuiya yoyote ile iwe ya Nchi au ya kanda.

Hata hivyo Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi aliipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa utendaji wake uliopiga hatua ya ufanisi ikiwa bado mfano mzuri kulinganishwa na Jumuiya nyengine zilizowahi kuundwa ndani ya Bara la Afrika.

Alipendekeza Nchi Mwanachama  kupewa haki na fursa ya mapato yake inayokusanya kwa mujibu wa uuzaji wa ulinganifu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Balozi huyo Mstaafu ambae pia Mhadhiri wa Elimu ya Chuo Kikuu Nchni Balozi Msuya Waldi Mangachi kwa uamuzi wake wa kuandika Historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Balozi Seif alisema Historia ya Kitabu hicho itatoa fursa  zaidi kwa Kizazi kipya kuelewa malengo ya Waasisi wa chimbuko la Jumuiya hiyo waliokuwa na muono mpana zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.