Habari za Punde

Ali Khamis Mtumweni: Mchezaji alievuma miaka ya 80

 Mchezaji wa zamani wa timu ya Tamasha, Timu ya Taifa ya Zanzibar na Taifa Stars kutoka Pemba , Ali Khamis Mtumweni
WA mwanzo kulia waliosimama Ali Khamis Mtumweni  akiwa na kikosi chake cha timu ya Tamasha mnamo mwaka 1976 kwenye uwanja wa Mjimbini Mkoani, kwenuye mchezo wa kirafiki na timu ya Chipukizi ya Chake chake (picha na hisani ya Fuom Haji machezaji wa Tamasha )


Na Hamad Hassan, OUT

‘’UTITIRI wa vilabu haukuzi soka bali washusha soka la Zanzibar’’ ni kauli ya ya aliekuwa kinara wa soka miaka iliopita.

Kauli hiyo iliotolewa na mchezaji alievuma miaka ya 80, na jina lake ambalo litachelewa kuvunja rekodi la ‘Ali Khamis Mtumweni.

Mtumweni alinishitumia hata mimi mwandishi wa makala haya, juu ya kauli yake kwamba utitiri wa vilabu unachangia kuangusha soka la Zanzibar.

Hapo sasa nililazimika kweka sawa kalamu yangu, na niliganda nae kutaka kujua ni kwa nini uwepo wa vilabu vingi hakuinui soka?

Hakuwa na kigugumizi kuelezea kwa upana juu ya kuwepo kwa vilabu vingi hasa katika kijiji kimoja na walioanzisha wakidhani kuwa wanataka kunyanyua soka.

Mtumweni aliezaliwa mwaka wa Mapinduzi ya Zanzibar, yaani mwaka 1964, hakusita kusema kuwa vilabu vinapokuwa vingi kinachojitokeza ni ushindani usio na faida kwa taifa.

Kwa mfano katika ukanda wa Wilaya ya Mkoani ambapo yeye anaishi, kuna vilabu zaidi ya sita vinavyoshiriki lidi daraja la kwanza taifa Pemba.

Hakusita kutilia nyama kauli yake kuwa, huku kukiwa hakuna hata klabu moja iliowahii kusonga mbele na aalu kuwa mshidi wa soka la Zanzibar.

Kauli hiyo ya Ali Khamis Mtumweni, ilikuwa ikiashiria kwamba hakuna umuhimu wa kuwa na vilabu vingi hapa Zanzibara, kama kweli kuna nia ya kukuza soka.

‘’Mimi wakati nakipiga na timu kali ya Tamasha ya Mkoani, ambayo iliwahi kutikisha sana kulikuwa na timu mbili tu Mkoani mzima, ikiwa ni pamoja na Pindua lakini leo du…..’’,alisema na kucheka.

Mtumweni ambae soka lilimuzesha kumpa umaarufa na kisha kujenga nyumba ambayo anaishi huko Mbuguwani Mkoani, hakusita kunieleza kwa upana historia yake ya soka.

Mtumweni alianza kulipenda soka akiwa Skuli ya msingi ya Uweleni wakati huo mnamo mwaka 1972, kabla ya kuingia Sekondari hapo hapo Uwelini miaka 10 baadae.

Alidokiza kuwa, wakati akiwa Skuli hasa ya Sekondari waliweza kutamba sana akiwa anachezea namba tisa ‘streak’ na kufanikiwa hata kutwaa uchampioni wa skuli za sekondari.

‘’Nyota yangua hasa ilianzia nilipoingia Sekondari na ndipo hapo hasa mwalimu wa timu ya Tamasha, aliponiona na kuanza kunifuatilia na nikafanikiwa kuanza kucheze nayo hata kabla ya kumaliza skuli’’,alisema huku akiwa juu ya bao analozungumzia.

Mtumweni alianza kutikisha wavu kwa kujipatia goli lake la kwanza kwenye mashindano maalum ya Skuli katika miaka ya 80, pale alipoifunga goli pekee kwa timu yake ya Skuli ya Uweleni.

Mchezo huo ambao alisema ulianza kumpa umaarufu na kuwa gumzo hata skuli ni pale wakati skuli yake ilipocheza na skuli jirani ya Ng’ombeni.

Hamu ya kupenda soka iliendelea kumuingia kichwani na kuwa na hamu ya kuwa mchezaji wa timu ya taifa, ambapo hilo alifanikiwa kama kula Papai kwa jiko.

Mwaka mmoja tu baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari, Mtumweni ndipo alipoanza rasmi kusakata kabumbu, akikipiga na Tamasha iliokuwa na mastakimu yake Mkoani Pemba.

Kocha Yussuf Ramadhan, ndio iliokuwa taa ya mwanadinga huyu, ambae alishalitumikia taifa kwa muda wa takriba miaka kumi, hadi kufikia kustaafu soka.

‘’Nilipofika ndani ya klabu hiyo, nilidhani sitoweza kucheza maana nilikutana na vijeba tena vya wakati huo vikubwa na vinene’’,alieleza kwa bashasha.

Mtumweni mwenye umbo la wastan na mrefu aliepanda juu , alisema kutokana na umbo lake sikudhani kuwa ningeweza kuchuuana na vijeba ambavyo vyengine ni kaka zangu mara mbili i’’,alisema .

Wakale walisema kuwa ukubwa sio hoja, wala usione samaki mkubwa ukaogopa kuuliza bei ndivyo ilivyokuwa kwa Mtumweni wakati alipobisha hodi kwenue klabu ya Tamasha.

Alivitaja  vijeba alioanza nao kwenye timu hiyo kuwa ni pamoja na Salim Kiburungu aliewahi kuwa muwamuzi wa soka, Hamza Ussi aliewahi kuwa karani wa Mahakama, Foumu Haji nae pia aliwakuwa karani Mahakamani.

Wengine aliocheza nao Mtumweni akiwa kwenye klabu kongwe ya Tamasha ni Salim Khamis, na Affan Othuman aliewahi kuwa Katibu Mkuu  Msaidizi wa ZFA Pemba na wengine aliowasahau.

Mtumweni alijingamba kwamba wakati huo soka la Zanzibar lilikuwa juu na hata baadhi ya timu za nchi za Afrika Mashariki na Kati kuiogopa Zanzibar kutokana na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja uchache wa vilabu.

Alivitaja vilabu ambavyo wakati huo vilikuwepo kuwa ni pamoja na Wete Star, Tamasha ya Mkoani, Pindua, Chipukizi, na kwa Unguja zikikuwepo kama vile Small Simba, KMKM, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kimtazamo hapo utaanona kuwa kauli ya Mtumweni, inaingia akilini kwamba uwepo wa vilabu vingi, kamwe havisaidii kunyanyua soka hapa Zanzibar.

Mtumweni alidumu  na timu ya Tamasha ya kwa muda wa miaka saba, kuanzia mwaka 1986 ,kabla ya kujiunga na Mkoani Shootin katika miaka ya 1987 mara baada ya kusambaratika kwa timu ya Tamasha.

Timu ya Tamasha katika uhai wake iliwahi kunyakua nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya Zanzibar, katika mwaka 1983, huku Small simba ikiibuka na machampion na KMKM kushika anafasi ya pili.

‘’Mwaka huo nilijisikia mmbora na safi kwenye soka maana nilicheza mpira bila ya kuchoka na kama si hujuma zilizofanywa, tulipaswa tuwe washindi wa pili’’,alieleza Mtumweni.  

Hata hivyo Mtumweni alilalamikia kwa wakati huo kwa kosa udhamini hata kwenye ligi, jambo ambalo kwa upande mmoja liliamsha ari kwa wachezaji.

‘’Suala la ufadhili kwa enzi zetu, halikuwa likizungumzwa, na badala yake wachezaji walikuwa wakijihudumia wenyewe na hata watu wenye uwezo ndio wafadhili’’,alifafanua.

Kwa kanre hii mwanandinga huyu anashangaa kuona kwamba timu hasa ligi kuu ya Zanzibar, imekuwa ikipata ufadhili japo mdogo, lakini hakuna kiwango cha soka kinachoonekana.

Hakuacha kurejea kauli yake kuwa suala la utitiri wa vilabu, sio suluhisho la kukuza soka Zanzibar, bali uwajibikaji na uzalendo ndio kinachozingatiwa kwa wachezaji.

‘‘Sisi enzi zetu hatukuwa na njaa ya kuhama hama vilabu, maana tukiona ni usaliti kuacha kbalu ya nyumbani na kuhamia klabu ya ugenini’’,alisema akiashiria kua suala la kuhama vilabu  sio zuri.

Mtumweni alizidi kubainisha kuwa kwa sasa wachezaji kadhaa hawana uzalendo, mapenzi, nidhamu, uwajibikaji kwenye vilabu kutokana na kuweka mbele suala la fedha.

Yeye  anadhani suala la kwanza unapoingia kwenye soka, mchezaji aelewe hakuna malipo yanayofanana na kazi hiyo, ni vyema tu wachezaji wawajibike ili kuliletea heshima taifa lako.

Pamoja na kwamba hakupata matatizo mengi alipokuwa kwenye ngarambe za soka, lakini anasema alipata faida nyingi moja wapo ikiwa ni pamoja na kutembelea nchi kadhaa za bara la Afrika.

Miongoni mwa nchi alizozikanyaga mwanandinga huyo wakati akiwa na timu ya taifa ya Zanzibar ni pamoja na Ethiopia, Oman, Kenya, Malawi ambapo pia aliwahi kucheza michezo kadhaa ya kimataifa ikiwa ni pamoja na ya kirafiki.

Mchezaji huyo aliekuwa kama kiraka, pia aliwahi kukipiga na timu ya taifa ya Tanzania mnamo mwaka 1987, na akiwa na klabu hiyo anasema hatousahu mchezo baina ya Tanzania na Algeria kwenye uwanja wa Arusha.

Mchezo huo kwa Ali Khamis Mtumweni ambao walishindwa kutambiana na wageni wao hao, alijiona kucheza kwa nguvu na maarifa makubwa tena bila ya kuchoka.

‘’Wakati huo nilikuwa najisikia sana ninapokua na mashujaa wenzangu akina Abubakar Salim, Khalfan Ngasa, Rajab Risasi, Othuman Jum, na kutoka Zanzibar walikuwepo wengi’’,aliwataja haraka haraka.

Wakati huo hata Zahoro Salim, Othuman Abdallah Foreman, Nassor Mwinyi Bwangwa nao walikutana na Mtumweni kwenye kikosi kizito cha timu ya taifa ya Tanzania.

Ambapo hapo ndio hasa timu hiyo ilipokuwa ikivuma ambapo kwa wakati huo alikuwa mchezaji pekee kutoka Kisiwani Pemba.

Kinara huyo wa soka alidai kuwa siku hipo waliowaliza wageni wao kutoka Msumbuji kwenye uwanja wa Dodoma, kwani hadi dakika 88 walikuwa hatujafungana na dakika moja kabla ya mchezo kumaliza kulipigwa shuti na mchezaji mmoja hadi wavuni.
  
Miaka michache baadae Mtumweni alijunga na timu ya Jamhuri akiwa anachezea namba tisa, ingawa hakuduma kwa muda mrefu na baadae kuamua kustaafu soka.

Kwa muda huu mwanasoka huyo anasema hana hata klabu moja ya ndani ya nchi anayoishabikia kutokana na soka bovu linaloonyeshwa na wachazaji ingawa wanaufadhili wa hata vifaa.

Kuhusu watoto wake, ikiwa kuna mmoja alau anaefuata nyayo zake alisema kati ya watoto wake 10, hakuna hata mmoja ambae ameanza kujituma kwenye soka.

‘’Mimi hata mwanangu mmoja hakuna anaenifuatia na wala sina klabu hata moja ninayoifundisha na nipo tu na pirikapirika zangu za kuvua tu na kilimo’’,alisema huko nyumbani kwake Mbuguwani Mkoani Pemba.

Hata hivyo alisema aliwahi kutimuliwa kazini kutokana na soka, ingawa alipewa mafao yake wakati alipokuwa akifanya kazi bandari ya Mkoani alipochukuliwa na kocha wake Ramadhan Yussuf.

Hakuacha kuishauri Serikali kupitia Wizara yake inayoshughulikia michezo kuwatambua wanamichezo wa zamani na hasa walioliletea taifa hili heshima kwenye michezo mbali mbali.

‘’Kwa mfano kama mimi hapa leo hii nikienda kwenye viwanja vya michezo lazima nilipe, lakini mchezaji wa juzi anapita bure sasa ule mchango wa Serikali kwetu sisi uko wapi’’,alihoji.

Mtumweni pia aliwataka vijana wa leo kuacha kuchanganya mpira na uvutaji wa hata sigara, iwapo wana nia ya kweli katika michezo na kuacha anasa ambazo zitawadhoofisha afya zao.

Alimtaja mchezaji Stevin Gerard wa klabu ya Liverpool kwamba ndio klabu na mchezaji pekee ulimwenguni anaemmaliza moyoni mwake na kukosa usingizi wakati inapocheza.

Ali Khamis Mtumweni (58) aliezaliwa Mbuguwani Mkoani Pemba, kwa sasa anaishi hapo hapo kwenye nyumba yake ya kujenga kutokana na soka iliopo mkabala na bekari ya Mbuguani.

Alipata elimu yake ya Quran katika chuo cha baba yake mzazi mzee Khamis Mtumweni na kuanza masomo yake ya darasa la kwanza skuli ya Uweleni mwaka 1972 hadi mwaka 1982 na kumalizia elimu ya sekondari.

Kwa sasa Mtumweni ni mvuvi mkuu wa bahari ya hindi na anaendesha maisha yake kupitia rasilimali ya bahari, huku alilalamikia kutoenziwa kama mtu alieliletea heshima taifa la Tanzania na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.