Habari za Punde

Katibu Mkuu Utumishi: Tunzeni kumbu kumbu za watumishi

NA HAJI NASSOR, PEMBA

KATIBU Mkuu wizara ya Nchi Afis ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa na Utawala Bora Zanzibar Yakout Hassan Yakout amewaagiza watendaji wa idara ya utumishi wa umma, kuhakikisha wanakuwa na kumbu kumbu sahihi za wafanyakazi, ili kuepusha usumbufu pale wanapofikia hatua ya kustaafu.

Alisema haipendezi na wala haingii akili, kuona mtumishi analitumikia taifa kwa miaka kadhaa, kishaa anapostaafu iwe ni kazi kupatikana kumbu kumbu zake.

Katibu huyo alieleza kuwa, lazima kila mmoja ndani ya wizara hiyo, awajibike ipasavyo na hasa kwa wale wanaohifadhi kumbu kumbu za watumishi wa umma, ili anapomaliza muda wake wa utumishi, isiwe kuhangaika huku na kule, kutafutiwa vielelezo vyake.

Katibu Mkuu huyo alieleza hayo, ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo kisiwani Pemba, wakati alipokutana na watendaji wa wizara hiyo na wafanyakazi wengine, ili kusalimiana nao, na kuwataka kuwajibika ipasavyo.

Alisema jina la wizara hiyo limebeba bango la utumishi wa umma na utawala bora, hivyo ni vyema wakaendena na kasi ya jina hilo, ili watumishi wanapomaliza kulitumikia taifa lao, wapate haki yao kwa haraka.

“Mtu anaefanyakazi kwa muda mrefu, na ikafika siku ya kustaafu anataka kupewa haki zake, kisha afike wizarani aambiwe ngoja kwanza tutafute vielelezo vyako, kwa kweli hatutomtendea haki’’,alifafanua.

Katika kuhakikisha hilo linakuwa imara, Katibu Mkuu huyo Yakout Hassan Yakout alisema wizara inaendelea na mpango wa kuweka kumbu kumbu za wafanyakazi ‘data base’ ili iwe rahisi kupatikana.

Akizungumzia suala la nidhamu, aliwataka wafanyakazi hao kuhakikia wanaheshimiana, ili wafanyekazi zao kwa utulivu, sambamba na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mpaema Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Pemba Massoud Ali Mohamed, amemuhakikishia Katibu Mkuu huyo, kuendelea kufanyakazi kwa moyo mmoja, licha ya changamoto zinazowakabili.

Hata hivyo amewataka wafanyakazi hao, kuendelea kusaidiana na kufanya kazi kwa kushirikiana, ili kufanikisha malengo ya wizara hiyo.

Baadhi ya wafanyakazi waliochangia kwenye mkutano, huo walisema wanayohamu na shauku ya kufanyakazi kama wakipatiwa vifaa.

Nassor Bakar, alisema suala la kuhifadhi kumbu kumbu za watumishi ni jambo jema, ingawa linahitaji kupwatia vifaa vya kisasa.


Hata hivyo wafanyakazi hao, wamempongeza Katibu Mkuu huyo kwa kufika kisiwani Pemba kujitambulisha kwake, na kuahidi kushirikiana naye.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.