Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kutoa Taarifa Kuhusu Mabango ya Ajira Yenye Kutiliwa Shaka.

Jovina Bujulu- MAELEZO.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na watu wenye Ulemavu Mh. Jenista Mhagama amewatahadharisha wananchi kuwa makini na mabango ya ajaira yanayoyozagaa barabarani.

Waziri Mhagama ametoa tahadhari hiyo alipokuwa akizungumzia mada kuhusu kuwepo kwa utitiri wa mabango ya ajira yanayoambatana na ahadi za uongo kwenye mishahara

Aliongeza kuwa ni vyema wananchi wakitilia shaka uhalali wa mabango hayo wakatoa taarifa kwenye mamlaka husiko ili hatua ziweze kuchukuliwa ikiwemo kutasaka waliobandika ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

 “Mamlaka husika zina wajibu wa kujiridhisha na kuhakikisha kuwa mabango yanayopewa ruhusa kubandikwa barabarani ni sahihi yanatangaza ukweli na yanafuata maadili,” alisema Waziri Mhagama.

Ikibainika kuwa mabango hayo yanakwenda kinyume na utaratibu waliokubaliana mamlaka husika wana wajibu wa kufuatilia na kuyaondoa mabango hayo ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Akizungumzia suala la mabango yanayotangaza ajira yanayoambatana na ahadi za uongo, Mhagama amesema kwa kuwa Wizara yake ndiyo yenye dhamana ya ajira, inabidi wawasiliane na mamlaka husika ambazo zimeruhusu mabango hayo ili wafuatilie na kuchukua hatua stahiki.

Aidha alizungumzia ukaguzi unaofanywa na wizara yake mahali pa kazi alisema kuwa wao hawafuatilii mabango bali huenda kufuatilia kama mwajiri anafuata sheria za kazi ikiwemo mikataba, mishahara, afya na kupeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya jamii.

“Tunapokuta malalamiko ya wafanyakazi, au kukuta mwajiri hapeleki michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii, kuna adhabu za hapo kwa hapo kama vile kumtoza mwajiri pesa” alisema Mh. Janista Mhagama.

Katika kuhakikisha utendaji kazi unaridhisha na maridhiano sehemu za kazi Mhagama alisema kuwa wao kama wasimamizi wakuu wa ajira nchini wanafanya kazi kwa karibu na shirikisho la vyama vya wafanyakazi na waajiri, ili kutatua kero sehemu za kazi.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar-es-Salaam Isaya Mwita amesema kuwa utaratibu wa kuweka mabango upo kisheria katika Halmashauri ila usumbufu mkubwa ni kuwa matangazo madogo madogo ambayo mengi yanawekwa kwenye karatasi za A4 ambayo yanabandikwa kwenye kuta za nyumba, nguzo za umeme na miti.

Meya huyo amebainisha kuwa wapo katika mchakato wa kukutana na viongozi wa Jiji wakiwemo Madiwani, Wenyekiti wa Halmashauri na wengine ili kuweka utaratibu wa kudhibiti matangazo hayo, ikiwemo kuweka sheria ndogo ndogo lengo likiwa ni kuwapunguzia kero wananchi ambao wanaumizwa na matangazo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.