Habari za Punde

Wastaafu Sasa Kuhakikiwa Majumbani na Hospitalini

Mkaguzi wa ndani kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bi.Mary Mauki akimpa maelekezo mstaafu wa Jeshi Bw.Rashid Hussein wakati wa uhakiki wa wastaafu wanaolipwa Pensheni na Wizara ya fedha na Mipango unaondelea katika Viwanja vya karimjee Jijini Dar es Salaam.

Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Bw.Mohamed Mtonga ametoa wito kwa wastaafu wanaolipwa Pensheni na Wizara ya Fedha na Mipango ambao ni wagonjwa na hawawezi kufika katika viwanja vya Karimjee na Mwalimu Nyerere(Sabasaba) kwa ajili ya uhakiki wa nyaraka zao kutoa namba za simu na majina yao ili waweze kuhakikiwa pale walipo kama ni Hospitali au nyumbani.

Bw.Mohamed Mtonga ametoa wito huo leo Jijini Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya zoezi la uhakiki wa taarifa za wastaafu wanaolipwa pensheni na Wizara ya Fedha na Mipango linalofanyika katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia leo tarehe 6-10 Machi.

“Kwa sasa ninavyozungumza zoezi hili liko kwenye hatua ya mwisho katika Mkoa wa Dar es Salaam,Zoezi hili lilianza Mkoa wa Pwani na tumelifanya nchi nzima na limefanyika kwa ufanisi mkubwa sana na wastaafu wengi wamejitokeza na kama mnavyoona zoezi limekuwa likiendelea kwa utaratibu mzuri sana”,Aliongeza Bw.Mtonga.

Mtonga amesema wastaafu hao wengi ni watumishi wa Serikali ambao walifanya kazi kabla ya mwaka 1999 ambapo walikuwa hawapo katika mifuko ya pensheni ndio ambao wanalipwa pensheni na Serikali wakiwemo watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Aidha amesema lengo kubwa la kuhakiki wastaafu hao ni kuboresha daftari la wastaafu ili kusaidia kujua ni kiasi gani cha wastaafu wapo katika kumbukumbu ya daftari la pensheni na kusisitiza wastafu ambao hawatajitokeza watafutwa katika daftari hilo.

Ukaguzi huu kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2014 na ukaanza tena mwezi Octoba mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.