Habari za Punde

Balozi Seif azindua rasmi Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya


  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiizindua rasmi Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi wa Tume hiyo Bibi  Kheiryangu Mgeni Khamis,Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Waoto Mh. Moudline Syrus Castico na Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud.
Balozi Seif akiwa pia Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya akikiongoza Kikao hicho cha kwanza mara baada ya kuizundua rasmi. 

Picha na – OMPR – ZNZ. 

Na Othman Khamis OMPR

Makamu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba hatma ya Zanzibar kuhusiana na janga la Dawa za Kulevya limo mikononi mwa Tume ya Kitaifa ya kuratibu na kudhibiti madawa ya kulevya iliyoundwa kwa lengo la kukabiliana na janga hilo.

Alisema wakati Wajumbe wa Tume hiyo wakijipanga kuingia kwenye vita hivyo  waelewe kwamba wanaingia katika vita vikali vya kupambana na wenye fedha nyingi na mtandao wa siku nyingi.

Akiizindua rasmi Tume hiyo ya Kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar akiwa yeye ndie Mwenyekiti wa Tume hiyo  Balozi Seif Ali Iddi alisema mafanikio ya Tume hiyo yatategemea zaidi jindi wajumbe wake watakavyojipanga vizuri kwa kushirikiana  kwa karibu zaidi na wadau wengine katika kukabiliana na uingizwaji wa dawa hizo Nchini.

Balozi Seif alisema hali ya utumiaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini kote sio mzuri hali iliyopelekea Serikali zote mbili kulivalia njuga tatizo hilo sugu la Dawa za kulevya lenye kuiangamiza jamii hasa Vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa.

Alisema kwa kuwa wanaojishughulisha na dawa za kulevya baadhi yao wanaeleweka na wanaishi pamoja na jamii Mitaani. Hivyo ni vyema jukumu la Wajumbe wa Tume hiyo likaelekeza zaidi nguvu zake katika uzuiaji wa uingizaji wa dawa hizo hapa nchini sambamba na kutoogopa kuwachukulia hatua za kisheria wahusika hao.

Balozi Seif alisisitiza kwamba kwa kuwa suala la dawa za kulevya linazikumba pembe zote za Dunia, mafanikio ya vita hivyo yatahitaji mashirikiano ya Taasisi za ndani na nje ya nchi ambazo zinajihusisha moja kwa moja na dawa hizo thakili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein mwa imani aliyokuwa nayo kwake  kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.

Aidha Balozi Seif aliwapongeza Wajumbe wote walioteuliwa kushirikiana naye katika utekelezaji wa jukumu hilo zito ambalo anaimani kwamba kila mjumbe analiweza licha ya uzito uliopo mbele yao.

Balozi Seif  aliwakumbusha Wajumbe wa Tume hiyo  wajibu wao kwa Mujibu wa Kifungu cha 4 {1} cha Sheria  wa kusimamia mambo Tisa akiyataja baadhi yake kuwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mpango wa Taifa za Udhibiti wa Dawa za kulevya.

Nyengine alisema ni kupitia sheria na kanuni za Udhibiti wa dawa za kulevya, kuimarisha na kuendeleza jitihada za kuzuia matumizi ya dawa za kulevya, kuanzisha mfumo wa ukusanyaji na uchambuzi wa Taarifa za matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa sheria nambari 9 ya mwaka 2009  kifungu cha 4 {1} Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya  Wajumbe wake wana wajibu wa kukutana Mara Mbili kwa Mwaka.
                                          

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.