Habari za Punde

Balozi Seif Awaasa Wafanyakazi Wanapaswa Kujituma Katika Majukumu Yao ya Kazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Cheti Maalum Mama Asha Suleiman Iddi aliyekuwa Katibu Muhtasi  wa Waziri Kiongozi ambae amefikia umri wa Kustaafu Utumishi wa Umma hapo Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi wa Zamani Kikwajuni Zanzibar.
Mstaafu wa Idara ya Upigaji chapa Bibi Kiboga Suleiman Mohamed akipokea cheti Maalum kutoka kwa Balozi Seif  baada ya kumaliza muda wake wa Utumishi wa Umma Serikalini.
Katibu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu Bwana Abdulla Ali Abdulla Kitole akipokea zawadi ya Laptop kutoka kwa Bosi wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kama ukumbusho akiwa katika mapumziko yake ya ustaafu Serikalini.
Mhasibu Mkuu Mstaafu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Makame  Mussa Sururu akikabidhiwa zawadi yake ya Jokovu la kuhifadhia vitu baridi kutoka kwa Balozi Seif kwenye hafla ya kuagwa kwao rasmi baada ya kumaliza muda wao wa Utumishi Serikalini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Wizara ya Nchini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na wafanyakazi wastaafu wa Ofisi hiyo walioagwa rasmi hapo Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wake Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi ambae ni Mstaafu na Mkurugenzi Uendeshaji wa Ofisi hiyo Bibi Halima Ramadhan Toufiq.Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wake Mh. Mihayo Juma N’hunga, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Ng. Joseph Abdulla Meza na Naibu wake Nd. Ahmad Kassim Haji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na wasaidizi wake mara baada ya kuiongoza hafla ya kuwaaga wafanyakazi wastaafu wa Ofisi yake hapo Kiwajuni Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wafanyakazi wanapaswa kujitahidi kutekeleza majukumu yao ya Utumishi wa Umma kwa kufanya kazi kizalendo na  ushirikiano uliotukuka ili  kujijengea mazingira bora ya hatma yao ya baadae.

Alisema tabia hiyo njema itawapa  heshima kubwa katika Jamii kiasi wamba wamalizapo muda wao wa Utumishi watajikuta wakiacha athari inayoendelea kukumbukwa kwa wema na watumishi wenzao waliowaacha.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa hafla maalum ya kuwapongeza na kuwaaga Wafanyakazi 13 waliostaafu kati ya Mwaka 2015/2016 na 2016/2017 wa Idara tofauti zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyofanyika ndani ya Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema haipendezi na ni hulka mbaya inayowakumba baadhi ya Watumishi wa Umma hawa wale wenye mardaraka pale wanapofikia muda wao wa kustaafu na walio nyuma  yao wakasherehekea kwa Pilau kutokana na vitendo  vyao vilivyokosa imani kwa kutowatendea haki.

Balozi Seif aliwapongeza Wafanyakazi wote waliostafu  kwa kumaliza Utumishi wao katika njia ya salama na afya njema iliyopatikana kwa wao kuzingatia na kufuata mashauri ya Kitaalamu ya Afya katika mfumo wa kufanya mazoezi baada ya muda wa kazi.

Aliwataka wafanyakazi wanaofikia umri wa kustaafu kuachana na tabia ya kujenga hofu kipindi wanachokaribia kumaliza muda wao wa Utumishi kwani kinaweza kuwasababishia msongo wa mawazo yanayoishia kupata maradhi.

Balozi Seif alitanabahisha wazi kwamba kustaafu sio mwisho wa maisha lakini kinachotakiwa  kwa wastaafu hao ni kujipanga vyema ili kukabiliana na mabadiliko ya maisha mapywa wanayoyaingia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wafanyakazi wapya na wale wanaoendelea na utumishi wao kutumia maarifa, uzoefu, ujuzi na hata mbinu zilizokuwa zikitumiwa na watangulizi wao waliostaafu ili kupata ufanisi mzuri kwa Wizara na Taifa kwa ujumla.

Mapema akitoa Taarifa fupi ya wafanyakazi hao wastaafu, Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bibi Halima Ramadhan Toufiq alisema Utumishi wa Wafanyakazi hao wastaafu katika Taasisi za Umma umesaidia kizazi kipya katika kuendeleza gurudumu waliloliacha.

Bibi Halima alisema licha ya wastaafu hao kuwa na uwezo kamili wa kuwajibika zaidi lakini Kifungu cha 68 {1} cha Utumishi wa Umma kimeweka bayana kuhusu kumaliza kwa Mkataba wa ajira.

Mkurugenzi huyo wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wastaafu hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi wapya ili kuwapa maarifa yatakayowasaidia kumudu vyema kutekeleza kazi zao.

Bibi Halima aliwataja Wafanyakazi hao 13 wastaafu kuwa ni pamoja na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi aliyekuwa Katibu Muhtasi wa Waziri Kiongozi na Ndugu Abdulla Ali Abdulla Kitole aliyekuwa Katibu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Wengine aliowataja ni Nd. Khatib Said Khatib aliyekuwa Mkurugenzi Uratibu, Bibi Shinuna Idara ya Faradha, Nd. Makame Mussa, Nd. Hassan Mohamed  Hassan ,  Nd. Tajo Hussein Mawele, Bibi Amina Hussein Haji, Maabad Mlekwa Maabad, Siende Khatib Khamis, Mafunda Khamis Hamad,  Kiboga Suleiman na Aziza Khalef Mohamed.

Wastaafu hao pamoja na mambo mengine walikabidhiwa vyetu maalum, zawadi mbali mbali kulingana na kada zao pamoja na fedha taslim kama ni ukumbusho kwao kutokana na utumishi wao mzuri  uliotukuka.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Wastaafu  wenzake 13 Mstaafu nambari moja katika kundi hilo Mama Asha Suleiman Iddi alikiasa Kikazi kipya kinachoingia katika ajira mpya iwe ya Umma na hata ya Sekta binafsi kuacha tamaa ya kutaka kujilimbikizia mali na utajiri ndani ya kipindi kifupi cha ajira zao.

Mama Asha alisema kitendo hicho ambacho hushabikiwa na baadhi ya watu mitaani kwa kuonekana mjanja na mwenye maarifa mbali ya kuhatarisha ajira zao laikini pia kinakwenda kinyume na kanuni, maadili na heshima ya Kazi.

Akizungumzia suala na viinua mgongo vya watumishi wastaafu Mama Asha aliziomba Taasisi zinazosimamia masuala hayo kufanya juhudi za ziada katika kuona haki za wastaafu hao zinapatikana kwa wakati muwafaka bila ya kuleta kughdha yoyote.

Alisema zipo dalili zinazoonyesha kuwatia hofu baadhi ya watumishi wastaafu kutokana na kucheleweshewa   masurufu yao ambayo tayari wameshalenga kuwaendelesha katika muda wao wa kumalizia maisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.