Katibu Mkuu Kiongozi Dk Abdulhamid Yahya Mzee akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar akitowa Taarifa ya Ukaguzi wa Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar. kuhusiana na uchuguzi waliofanya, kushoto Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Ikulu Zanzibar Ndg Hassan Khatib. mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.04.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein katika kuimarisha utendaji Serikalini na kukuza Utawala Bora
alimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa
matumizi ya fedha za mishahara katika Wizara na Taasissi za Serikali na
kubainika mambo mbali mbali ambayo Serikali imeahidi kuyachukulia hatua.
Akitoa taarifa kwa
Waandishi wa Habari, Ikulu mjini Zanzibar, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa baada ya Rais
kukabidhiwa ripoti hiyo, alisema kuwa Rais Dk. Shein ameagiza wajuulishwe
wananchi juu ya mambo yaliobainika katika ukaguzi huo na hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali.
Dk. Abdulhamid alisema
kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya ukaguzi huo maalum
kuanzia mwezi wa Juni, 2016 hadi Novemba, 2016 na kuwasilisha ripoti yake kwa
Rais wa Zanzibar kama alivyoagizwa na kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria.
Alisema kuwa katika
ukaguzi maalum uliofanyika, mambo mbali mbali yalibainika ikiwa ni pamoja na
kuwepo wka tofauti baina ya fedha zilizoingizwa kwa ajili ya mishahara na fedha
halisi zilizotumika kulipwa mishahara hiyo katika baadhi ya taasisi za
Serikali.
Jengine ni kubainika
kwa watumishi ambao wamechukua likizo bila ya malipo ingawa bado wanaendelea
kupokea mishahara, kubainika kwa watumishi ambao wameacha kazi au kustaafu
lakini bado mishahara yao inaendelea kulipwa.
Aliongeza kuwa
kutojitokeza kwa baadhi ya wafanyakazi katika zoezi la uhakiki na kushindwa
kufika kuhakikiwa, kubainika kwa watumishi ambao wamefikia umri wa kustaafu kwa
lazima lakini bado wanaendelea na utumishi wa umma na kulipwa pamoja na
kubainika kwa watumishi ambao hawahudhurii kazini kwa muda mrefu na bado
wanapokea mishahara.
Aidha, alisema
kuwa jambo jengine lililobainika ni kwa
watumishi ambao hawawezi kufanya kazi kutokana na maradhi ya muda mferu lakini
bado hawajastaafishwa kwa mujibu wa sheria na wanaendelea kulipwa, kubainika
kwa fedha za mihshara zinazotumika kwa ajili ya matumizi mengine.
Pamoja na kubainika
kwa wafanyakazi waliokwenda masomoni kwa muda mrefu na hawajarudi tena makazini
lakini bado wanalipwa mishahara na Serikali.
Kufuatia hali hiyo, Dk.
Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa pamoja na mambo mengine Serikali inafanya
uchunguzi wa kina dhidi ya wale wote waliodaiwa kuchukua fedha za umma kinyume
na utaratibu ili endapo itathibitika hatua za kinidhamu na kisheria
zitachukuliwa.
Alisema kuwa Serikali
imeziagiza taasisi zinazohusika kusitisha mara moja malipo kwa wafanyakazi
walioacha kazi, kustaafu au kuchukua likizo bila ya malipo lakini bado
wanaendelea kulipwa mishahara na maslahi mengine.
Pia, Katibu Mkuu huyo
wa Baraza la Mapinduzi alisema kuwa Serikali itahakikisha kuwa fedha zote
zilizochukuliwa kinyume na taratibu zirejeshwe na inawataka wale wote
waliolipwa au kuchukua fedha za umma kinyume cha utaratibuwazirejeshe mara moja
na vyenginevyo hatua kazi za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi yao
ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
Aliongeza kuwa
Serikali itawapeleka wagonjwa wa muda mrefu katika Bodi ya Uchunguzi wa Afya
(Medical Board) na endapo watathibitika kwamba hawawezi kuendelea na kazi
watastaafishwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.
Pamoja na hayo,
Serikali itafanya uhakiki maalum kw awatumishi walioko masomoni kwa muda mrefu
ili kujiridhisha kama bado wanaendelea na masomo au vyenginevyo na hatua
muafaka kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma zitachukuliwa dhidi
ya watumishi watakaobainika wameshamaliza masomo lakini bado hawajaripoti
makazini.
Serikali pia,
itawastaafisha kwa mujibu wa Sheria wafanyakazi wote ambao wameshapita umri wa
kustaafu lakini bado hawajastaafishwa na wanaendelea na kazi pamoja na kufanya
uchunguzi juu ya matumizi tofauti ya fedha zinazozidi wakati wa zoezi la kulipa
mishahara ili kujua namna zinavyotumiwa na Taasisi za Umma na kama zinatumiwa
kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha au vyenginevyo.
Sambamba na hayo,
alisema kuwa Serikali itawachukulia hatua muafaka kwa mujibu wa Sheria na
Kanuni za Utumishi wa Umma wafanyakazi ambao hawahudhurii kazini kwa muda mrefu
bila ya udhuru ama sababu zinazokubalika kisheria.
Pia, alisema kuwa
Serikali itahakiki upya mishahara ya wafanyakazi ambao hawakujitokeza kabisa
kuhakikiwa na kujiridhisha endapo wafanyakazi hao wapo kiuhalisia au
vyenginevyo na kujua sababu zilizowazuia kutojitokeza kuhakikiwa wakati zoezi
la uhakiki lilipofanyika.
Aliongeza kuwa
Serikali itafanya uchunguzi wa kina kwa watumishi wote waliohusika kwa namna
moja au nyengine ama kwa uzembe au makusudi katika kusababisha matumizi ya
fedha za umma kinyume na ilivyostahiki na kuchukuliwa hatua kazi za kinidhamu
wale wote watakaothibitika kuhusika.
Katika mkutano huo na
waandishi wa Habari, Dk. Abdulhamid alisema kuwa taarifa hiyo ni ya awali na
matarajio ya kuwepo taarifa nyengine ambayo itataja kiasi cha fedha zilizopotea
na itatolewa kwani bado uhakiki unaendelea katika Mawizara.
Alizitaja miongoni mwa
Wizara ambazo zimegundulika kwa kiasi kikubwa na kadhia hiyo kuwa ni Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Afya na Wizara ya Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment