STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 23.04.2017
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewasisitiza
WanaCCM na wananchi kuwachagua viongozi wazalendo walio mstari wa mbele katika kuwaletea
maendeleo sambamba na kutekeleza ahadi zao kwa vitendo.
Dk. Shein ambaye pia, ni
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo leo katika
sherehe ya uzinduzi wa gari nane za abiria za Jimbo la Mfenesini zilizotolewa
na Mbunge wa Jimbo hilo Kanali Mstaafu, Masoud Khamis, sherehe zilizofanyika
katika ukumbi wa Hoteli ya Z Ocean Bububu Kihinani Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika hotuba yake, Dk.
Shein alisema kuwa ni wajibu wa kiongozi kuhakikisha pale anapotoa ahadi yake
basi huitekeleza, na kusifu moyo wa Mbunge huo kwa kutoa kiasi cha fedha
zipatazo Tsh. Milioni 192,000,000 kwa ajili ya kununua gari hizo.
Dk. Shein alimpongeza
Mbunge huyo kwa kuendeleza na kudumisha mashirikiano ya dhati kati yake na
wananchi wa Jimbo hilo sambamba na mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Mbunge
na Mwakilishi wa Jimbo hilo.
Aliongeza kuwa kiongozi
ni lazima apende kuwasikiliza wananchi wake pamoja na kufanya kazi na watu na awe
mbunifu, anaependa kusikiliza watu, kuwaona watu na hatimae kutekeleza kwa
vitendo hasa yale anayoyaahidi na kuwataka wanaCCM na wananchi kuwaunga mkono
viongozi kama hao.
Makamo Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar aliwataka WanaCCM na viongozi wa Chama hicho pamoja na wananchi
wa Jimbo hilo kuendelea kuwaunga mkono na kuwanao viongozi hao wa Jimbo hilo
ili Mfenesini iwe mpya na izidi kunawirika na kuwaeleza kuwa hawakufanya kosa
kumchagua Mbunge huyo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa gari hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la
ajira kwa vijana na kueleza imani yake kuwa gari hizo zitaendeshwa vizuri na
zitatunzwa na kueleza kuwa jambo hilo liwe mfano kwa viongozi wa Majimbo
mengine hapa nchini.
Katika sherehe hiyo Dk.
Shein nae kwa upande wake alimuunga mkono Mbunge huyo wa Jimbo la Mfenesini kwa
kuahidi kuzilipia Bima gari hizo zote nane ambazo zilikuwa bado hazijalipiwa
Bima lakini tayari taratibu nyengine zote zilikuwa zimeshafanyiwa kazi.
Aidha, Dk. Shein
aliwaeleza wananchi wa Jimbo hilo kuwa barabara za ndani zilizopo katika Jimbo
hilo zitatengenezwa huku akieleza juhudi za Serikali katika ujenzi wa barabara
kuu Unguja na Pemba sambamba na ufumbuzi wa tatizo la maji kwa Mkoa wa Mjini
Magharibi na kusema kuwa karibuni tatizo hilo litakuwa historia.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliendelea kuwaeleza viongozi wa CCM kuyaeleza mafanikio yaliopatikana
ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar alieleza
mashirikiano mazuri yaliopo kwa viongozi wa chama hicho Majimboni mwao na
kuahidi kufanya kazi kwa mashirikiano na kuwataka WanaCCM wasikubali kusikiliza
kasumba kutoka katika baadhi ya vyama vya upinzani.
Mapema Mbunge wa Jimbo
hilo Kanali Mstaafu Masoud Khamis
alimkabidhi kadi zote nane za gari hizo na kueleza kuwa kuazia leo gari hizo
sio zake ni gari za CCM kupitia uongozi wa Jimbo hilo na matawi yake yote chini
ya Bodi ya udhamini ya Jimbo hilo huku akisisitiza kuwa kwa dereva yeyote
atakaekiuka taratibu zilizowekwa ajue hana kazi.
Mbunge huyo alieleza
kuwa kukabidhi kwa gari hizo ni kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoahidi
wakati akitafuta ridhaa ya wananchi kumchagua katika uchaguzi Mkuu uliopita
huku akisema kuwa ni kawaida yake kutoa ahadi kwa yale anayoyamudu ambayo yamo
katika uwezo wake na kuchelea kuahidi mambo ambayo hana uwezo nayo
Nao viongozi wa CCM,
Mkoa, Jimbo, Wilaya pamoja na WanaCCM wa Jimbo hilo katika maelezo yao walitoa
pongezi kwa Dk. Shein kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho
ya mwaka 2010-2020 ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato.
Katika maelezo yao
viongozi hao walitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kutekeleza ahadi
yake kwa vitendo ya kuwapandisha mshahara wafanyakazi wa sekta ya umma kuazia
mwezi huu wa Aprili ambapo tayari ameshatekeleza na wafanyakazi wamepongeza
hatua hiyo.
Gari hizo nane
yaliotolewa na Mbunge huyo ni kwa ajili ya Matawi Manane ya CCM yaliyomo katika
Jimbo hilo lkiiwemo Tawi Chuini, Tawi la Kihinani, Tawi la Mfenesini, Tawi la
Bumbwisudi, Tawi la Mwakaje, Tawi la Mwachalale, Tawi la Kitundu na Tawi la
Kama.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment